MASTORI YA OSCAR: Mwana FA atatoboa?

Monday May 16 2022
fa pic
By Oscar Oscar

MARA nyingi sana nimekuwa nikimfananisha mwanamuziki Hamisi Mwinjuma na mwanasoka Andres Iniesta.

Kwa nini? MwanaFA sio msanii anayetoa nyimbo mara kwa mara lakini kila akitoa wimbo wake huwa ni gumzo. Hanaga kazi mbaya.


Ni fundi wa kuandika, fundi wa kurapu!

Iniesta sio mchezaji anayefunga mabao kila siku, lakini ndiye mchezaji aliyekuwa anaifanya timu itembee pale Barcelona. Ni mchezaji aliyekuwa anaifanya timu ikimbie. Kwa ufupi huyu Iniesta ndiye aliyekuwa master wa shughuli zote za ushambuliaji hasa pale Barcelona.

Ni mwaka sasa umepita MwanaFA hajaachia wimbo mpya. Gwiji ndiyo ilikuwa ngoma yake ya mwisho. Kuna mengi sana ya kujifunza kwa huyu mtoto wa Muheza mkoani Tanga.

Advertisement

Pamoja na uwezo mkubwa wa kuandika mashairi, MwanaFA ni mmoja kati ya wasanii wachache nchini wasomi kuwahi kupata shahada mbili za chuo kikuu. Sio jambo dogo.

Ni vigumu sana kwa maisha ya usanii kwenda shule. Wapo wachache wa kuhesabau hasa hapa kwetu. Haraka haraka utamuona mtu kama Nikki wa Pili na mwanadada Chemical ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi anafanya PhD.

Kwenda kusoma na kufanya muziki ni jambo gumu sana. Wengi huamua kuacha muziki kwanza na kwenda shule au kuacha masomo na kufanya muziki. Ukiona mtu anafanya vyote kwa pamoja, muogope.

Kumekuwa na shida kubwa kwenye muziki kadri siku zinavyokwenda. Msanii akipotea zaidi ya mwaka kurudi kwake kumekuwa tofauti na wengi hawarudi tena kwenye ubora wao. Baada ya kupata ubunge Profesa Jay alikaa kimya kwa muda mrefu kwenye muziki na aliporejea hakurudi tena kwenye kiwango chake licha ya kuachia ngoma kali kadhaa.

Ndio maana watu taratibu wanaanza kumsahau. Alipotea kwenye game Godfather wa Bongo Fleva, Sugu na aliporejea hakurudi kwenye enzi zake pamoja na kuwa kwa sasa anafanya muziki kwa starehe zaidi.

Nimeona wasanii wetu wengi wakongwe wanapata shida kubwa wanapotaka kurejea kwenye zama hizi. MwanaFA ni mmoja kati ya wasanii wachache walioweza kuhama kizazi cha nyuma kuja kizazi hiki kwa ubora uleule.

Lakini ameanza kukaa muda mrefu bila ngoma mpya. Ni kweli majukumu yameongezeka. Wananchi wa Muheza wanamdai maendeleo. Unadhani akiachia ngoma atarudi kwenye ubora ule ule? Nipe maoni yako kupitia namba ya simu hapo juu.

Tangu amekuwa mbunge hajatoa wimbo wowote. Tangu amekuwa mbunge hata kushirikishwa kwenye nyimbo za watu nako pia idadi imepungua. Ni kweli MwanaFA ni fundi wa mashairi. Ni kweli MwanaFA ni fundi wa kunata na biti, lakini kimya kimekuwa kingi.

Namkumbuka Lady Jaydee alivyokaa kimya na kutaka kurejea mapokezi ya albamu yake ya 20 hayakuwa makubwa sana. Ni mwanadada mwenye heshima kubwa sana nchi hii lakini ukikaa muda mrefu kwa soko la sasa watu wana kusahau.

MwanaFA hajawahi kuwa na kazi mbovu. Ni kama Iniesta anaweza asifunge bao karibu sehemu kubwa ya msimu, lakini siku akifunga anaweza kukupa Kombe la Dunia.

Anaweza kumaliza msimu akiwa na mabao manne tu, lakini yenye uamuzi mkubwa. Kombe la Dunia 2010 hakufunga mabao mengi lakini alifunga bao pekee lililowapa ubingwa wa Dunia kwa mara ya kwanza Hispania.

Ndivyo MwanaFA alivyo. Anaweza kukaa kimya muda mrefu, lakini akarejea kwa kuachia bonge la ngoma. Changamoto hapa ni muda tu aliokaa kimya.

Muziki wa sasa unaonekana unahitaji mtu kuwa masikioni mwa watu mara kwa mara. Wasanii wameongezeka sana teknolojia nayo imekua sana. Ukikaa kimya muda mrefu watu wanakusahau. Ukikaa kimya muda mrefu inakuwa ni kama unataka kuanza upya. Muziki ni moja kati ya kazi ngumu sana kwa sababu wakati mwingine sio tu ishu ya kutoa na wimbo bora.

Unahitaji muda wa kutosha wa kufanya promosheni. Unahitaji muda wa kutosha wa kufanya shoo. Unapokuwa na majukumu mengine kama MwanaFA muziki unakuwa ngumu sana.

Ni kazi inayohitaji mtu wa kuifanya kwa saa 24. Ni kazi inayohitaji mtu anayelala na kuamka kila siku akiwaza muziki. Sio rahisi kwa watu kama Nikki wa Pili ambaye kwa sasa ni mkuu wa wilaya. Sio rahisi kwa mtu kama MwanaFA ambaye ni mbunge.

Bado kwangu MwanaFA ataendelea kubaki kama msanii mwenye uwezo mkubwa wa kuandika. Ataendelea kubaki kwenye orodha ya wasanii wasomi na ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengi wa kizazi hiki.

Unadhani itakuwa rahisi kwake kutamba tena kwenye muziki akiwa mbunge? Nitumie maoni yako kupitia namba ya simu hapo juu. Tuendelee kumsubiri GWIJI. Tuendelee kumsubiri Iniesta wa Bongo Fleva.

Advertisement