Mastaa waliosaka tobo kimataifa kisha Bongo

Muktasari:
- Wapo ambao waliotafuta fursa baada ya kuona milango ni migumu Bongo na ambao mazingira ya kikazi au elimu yalichangia kuvuka boda hadi ughaibuni na kufanikiwa kwa kiasi fulani.
Kuna baadhi ya mastaa kutoka kiwanda cha muziki, filamu, urembo na mitindo nchini ambao umaarufu na kazi kwa kiasi kikubwa umeanzia nje ya mipaka ya Tanzzania ambapo walikwenda kusaka fursa za ndoto zao.
Wapo ambao waliotafuta fursa baada ya kuona milango ni migumu Bongo na ambao mazingira ya kikazi au elimu yalichangia kuvuka boda hadi ughaibuni na kufanikiwa kwa kiasi fulani. Hawa ni baadhi yao:
1. Heriet Paul - Marekani

Ndoto yake ilikwiva baada ya mama yake aliyekuwa balozi kuhamishiwa nchini Canada akiwa na umri wa miaka 14. Huyu alikuwa na ndoto ya kuwa muigizaji ila ikagundulika anaweza kuwa mwanamitindo (model) wakapiga picha zikatumwa New York, Marekani kesho yake akaitwa.
Akaanza kuishi New York akifanya kazi na agency ya Women Management, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni Vogue Italy ambapo ndipo na maisha ya kuwa model wa kimataifa ikiwemo kazi ya kupigwa picha yalianzia.
Hadi sasa ameshatokea kwenye kava ya majarida kibao maarufu duniani kma Vogue Italy, Teen Vogue, Glamour, Elle Canada, Arizona Muse, Dress to Kill, Freja Beha, Marie Claire na mengineo.
2. Idris Sultan - Afrika Kusini

Umaarufu wake Tanzania ulikuja baada ya kushinda shindano la Big Brother Africa Hotshorts 2014 nchini Afrika Kusini, kabla ya hapo Idris alikuwa ni mpiga picha katika kampuni ya I-View Studio.
Ushindi huo ulimfanya Idris kupata kitita cha Dola300,000, wastani wa Sh763.4 milioni kwa sasa, na kama unajua mwenye fedha tena akiwa kijana lazima awe maarufu na ndicho kilichotokea kwa Idris.
Idris ambaye sasa anacheza filamu anatajwa kama Mtanzania wa kwanza kwa filamu yake kuwekwa kwenye jukwaa la Netflix, na ni Mtanzania wa pili kushinda Big Brother baada ya Richard Dyle Bezuidenhout mwaka 2011.
3. Mayunga - Kenya

Mwimbaji huyu wa Bongofleva aliibuka mshindi katika shindano la Airtel Trace Music Star barani Afrika Machi 2015 katika fainali zilizofanyika Nairobi nchini Kenya. Shindano lilikutanisha washiriki kutoka nchini 12.
Na hapo umaarufu wake akachomoza Tanzania, Mayunga alifanikiwa kufanya kolabo na Akon, msanii wa Senegal mwenye makazi yake Marekani ikiwa ni sehemu ya zawadi ya shindano hilo.
Ikumbukwe wimbo waliorekodi pamoja unaitwa 'Please Don't Go Away', Mayunga aliachia ngoma hiyo Mei 2016 lakini tayari ulikuwa umerekodiwa tangu mwaka 2015, baadaye alifanya kazi nchini ya Universal Music Group (UMG) kwa muda mfupi.
4. Nandy - Nigeria

Alianza muziki akiwa bado ni mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE), akaamua kushiriki katika shindano la kwanza la karaoke barani Afrika, Tecno Own The Stage 2016 nchini Nigeria na kushika nafasi ya pili nyuma ya Shapeera wa Nigeria.
Kwa ushindi huo Nandy alipata kitita cha Dola15,000, wastani wa Sh38.1 milioni kwa sasa, huku akipata nafasi ya kujengewa uwezo na lebo ya Chocolate City ya Nigeria lakini kubwa zaidi alipata kuwa maarufu Bongo ndio mafanikio yake kumuziki yalipoanzia.
Nandy aliporejea Bongo akaanza kufanya muziki nchini Tanzania House of Talent (THT) kwa usimamizi wa karibu wa Ruge Mutahaba na kuachia nyimbo kama 'Nagusagusa' na 'One Day' ambazo ndizo zilimtoa kimuziki na sasa mengine ni historia.
5. Hemedy PHD - Kenya

Baada ya kumaliza kidoto cha sita mkoani Tanga, Hemed PHD aliamua kushiriki mashindano ya umbaji ya Tusker Project Face msimu wa pili nchini Kenya mwaka 2008 ambapo ushindi ulienda kwa Esther Nabaasa wa Uganda.
Kwenye shindano hilo ndipo jina lake likaanza kuwa maarufu Bongo na kuanza kusikika kwenye Bongofleva kwa kufanya kazi na wasanii kama Mr. Blue, Ray C, Gelly wa Rhymes, Bella Combo, Mabeste na kadhalika.
Hata hivyo, uwezo wake mwingine ulikuja kuoneka upande wa filamu ambapo amepata umaarufu mkubwa na sasa amejita katika ulimwengu huo akicheza tamthilia mbalimbali maarufu Bongo.