Marlaw alirekodi 'Bembeleza' ili kuimba kwenye mahafali!

KWA miaka mingi Bongofleva imejaliwa vipaji vingi vikali, kimoja wapo ni Marlaw ambaye ametoaa albamu mbili, Bembeleza (2007) na Bidii (2009) na zote ziliweza kufanya vizuri kutokana zilikuwa na ngoma kali.

Marlaw, jina hilo lipo kwenye orodha ya waimbaji wakali Bongo, sauti yake, melodi na uandishi ni miongoni mwa mambo mengi yanayofanya kuwa bora kwa mashabiki wake. Huyu ndiye Marlaw;


1. Wimbo wa Marlaw 'Bembeleza' aliurekodi kipindi yupo kidato cha sita kwa ajili ya kuuimba kwenye mahafali, ulirekodi Juni 2006 na Prodyuza Tuddy Thomas mkoani Iringa (sasa Njombe) na mahafali hayo yalikuwa yafanyike Februari 2007.


2. Baada ya kuja Dar es Salaam Marlaw alitaka kuurudia wimbo 'Bembeleza' kwa Prodyuza Roy, lakini baadaye wakaona hakuna sababu ya kufanya hivyo, mdundo aliotengeneza Roy ndio Marlaw akautumia katika wimbo wake, Busu la Pinki.

Utakumbuka Roy ambaye alifariki mwaka 2008, Mr. Blue anamtaja kama Prodyuza ambaye alikuwa anampatia sana pale alipokuwa anaimba.


3. R. Kelly ndiye alimvutia zaidi Marlaw hadi akaanza kuimba, utakumbuka hadi sasa ni Alikiba pekee Bongo amefanikiwa kufanya kazi na R. Kelly, pia Marlaw alivutiwa na wasanii wengine kama Celine Dion, Boyz II Men na Westlife.


4. Akiwa shule Marlaw alipigiwa na wadau wawili na kuambiwa aje Dar  es Salaam ili kufanya muziki baada yao wao kuukubali zaidi wimbo wake, Bembeleza.

Akatumiwa nauli, alipofika akawaimbia nyimbo ambazo alikuwa hajazirekodi ambazo ni Ritha, Bado Umenunua, Daima na Milele, wakaona uwezo wake, nao hao wadau ndio waliosambaza wimbo, Bembeleza mkoani Dar es Salaam.


5. Mashabiki wanajua kuwa wimbo wa Marlaw, Bembeleza ndio uliomtambulisha Prodyuza Tuddy Thomas, hata hivyo, Tuddy

anaamini wimbo wa Ibranation (Sauti) ndio ulimtoa. Na wakati Ibranation anarekodi wimbo huo alikuwa ni mwanafuni zwa Darasa la saba.


6. Mchora katuni na Mtangazaji, Masoud Kipanya ndiye alimpigia simu Ruge Mutahaba na kumuombea nafasi Marlaw pale Tanzania House of Talent (THT), Ruge alikubali na Marlaw akajiunga THT.

Ikumbukwe Masoud Kipanya ndiye aliyechora 'artwork' ya wimbo 'Vidonge Vyao'  wa kundi la Gangwe Mobb liloundwa na Inspector Haroun na Luteni Kalama kuanzia mwaka 1993.


7. Mke wa Marlaw, Besta ambaye pia ni mwanamuziki aliyetamba na wimbo, Baby Boy, baada ya kumaliza masomo yake nchini Uganda, alimtafuta Dudu Baya ili aweze kumsaidi kusambaza kazi zake kupitia Dar Skendo.


8. Katika wimbo wa Marlaw, Daima na Milele kuna sauti (back vocal) za wasanii wa THT akiwemo Mwasiti, wakati Marlaw anajiunga THT wasanii aliowakuta ambao walikuja ni Mwasiti, Vumi, Barnaba, Amini na Maunda Zorro.


9. Wimbo wa Marlaw, Ritha ni kisa cha kweli ambacho alisimuliwa na mtu mwingine akiwa Iringa kipindi anasoma, katika wimbo huo Marlaw hajaongeza wala kupunguza chochote kutoka kwenye simulizi aliyopewa kutokana haimuhusu yeye.


10. Ruge ndiye alimpigia simu Prodyuza Allan Mapigo na kumuelekeza arekodi nyimbo mbili za Marlaw, Bado Umenuna na Daima na Milele, hiyo ni baada ya Ruge kuona uwezo wake katika mazoezi ya THT. Ruge na Allan ndio walimtafuta Chid Benzi aliyesikika katika wimbo, Bado Umenuna.


WIKI IJAYO > Msanii anayefuata ni Daz Baba.