Marioo: Kisa Mtoto nimetengana na marafiki

Muktasari:
- Katika pitapita za hapa na pale Mwanaspoti lilipata muda wa kuzungumza na staa huyo ambaye amezaa na mrembo Paula, ambaye ni binti wa prodyuza wa muziki, P-Funk ‘Majani’ na muigizaji Kajala masanja.
MIONGONI mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya walioliteka anga la Bongofleva kwasasa mmojawapo ni Marioo. Mkali huyu ambaye jina lake halisi ni Omari Mwanga, ameutawala muziki vizuri na anatamba na wimbo wake wa 2025 aliomshirikisha msanii wake Stan.
Katika pitapita za hapa na pale Mwanaspoti lilipata muda wa kuzungumza na staa huyo ambaye amezaa na mrembo Paula, ambaye ni binti wa prodyuza wa muziki, P-Funk ‘Majani’ na muigizaji Kajala masanja.
Hapa Marioo anafunguka mambo kadhaa.
Anajiona wapi?
Marioo: Mario wa sasa sio wa zamani, wa sasa tangu nimekuwa baba mambo mengi kwangu yamebadilika, mfano kama matumizi ya pesa yameongezeka, kuwa mbali na marafiki, kwenda club siendi, kuwahi kurudi nyumbani, na vitu vingine na yote haya ili nipate muda wa kuwa na mtoto wangu, yaani kiufupi mtoto amenibadilisha na ndio maana niko kupambana sana kufanya uwekezaji wa namna nyingine ili kupata kipato zaidi.

Mnaishi maisha ya aina gani kiuhusiano na Paula?
Marioo: Maisha yangu na Paula yako tofauti na wanaume wengi kwenye uhusiano, mimi nampa sana uhuru wa kuwa katika maisha yangu, hata password ya simu yangu nimempa, hiki ni kitu ambacho kwa vijana wengi wa sasa hawawezi kukifanya kwenye mapenzi.
Mtoto wako unataka akue katika mazingira gani?
Marioo: Sitaki mwanangu akue katika mazingira niliyokuwa mimi, mimi nimelelewa na mama tu, baba yangu aliingia mitini, hivyo sitaki mtoto wangu aje kukua katika mazingira ya kulelewa na mama tu, nitahakikisha apate malezi ya baba na mama, na atasoma na kumaliza shule, sio kama mimi sikumaliza shule sababu mama yangu hakuwa na pesa ya kunisomesha japo darasani nilikuwa na akili sana, katika mitihani nilikuwa nashika nafasi ya kwanza au ya pili.
Ulishawahi kugombana na Paula?
Marioo: Ndio mara nyingi sana, na hii ni kutokana na mimi nikiwa studio kuchelewa kurudi nyumbani, na wakati mwingine tunakuwa tumeshalala lakini unaona simu inaita unahitajika kwenda studio kwa usiku huo, basi mama mtoto wangu Paula huwa anachukia sana lakini baadae tunayamaliza.

Ulimaliza vipi bifu na Harmonize?
Marioo: Sijawahi kuwa na bifu na Harmonize, zile zilikuwa stori tu za mtandaoni, watu waliunganisha ugomvi wa Harmonize na Paula, na baadaye wakaja kuona nipo kimapenzi na Paula basi wakajua nina bifu na Harmonize, ila mimi na Hamornize tunaelewana sana, sijawahi kugombana naye na wakati mwingine mbali na kufanya naye muziki huwa tunashauriana sana mambo nje ya muziki. Hayo mambo ya Harmonize na Paula yaliyotokea kipindi kile mimi nikiwa bado sijaanza uhusiano na Paula, hivyo kwanini niyabebe kumuwekea bifu? Na hata kama ningekuwa tayari nipo na Paula halafu kitendo hicho kimetokea najua ningemalizana naye vipi Hamornize na tungekuwa freshi tu.
Ni kweli unatendwa ndio maana unaimba nyimbo za mapenzi?
Marioo: Hapana. Mimi sio msanii wa nyimbo za mapenzi na sijawahi kuumizwa kwenye mapenzi wala kutendwa halafu ndio nije kuimba wimbo hapana. Nyimbo zote ninazoimba kuhusu mapenzi au kuumizwa huwa naimba tu, lakini hakuna kitu ambacho kimenitokea halafu ndio nikaimba. Na naimba nyimbo za aina nyingi sana sio mapenzi tu.

Colabo ipi imekubamba sana kati ya ulizofanya?
Marioo: Nimefanya colabo na wasanii wengi sana kama Harmonize, Ali Kiba, Rayvanny, Diamond na wengine wengi, zote ni nyimbo nzuri na zinafanya vizuri, ila colabo ya Harmonize wimbo wa Naogopa umefanya vizuri zaidi na unaendelea kufanya vizuri hadi sasa kuliko zote.
Ndoto yako ni nini?
Marioo: Ndoto yangu ni kutaka kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi na pia kukutana na wanamuziki wakubwa duniani.
Unamzungumziaje dansa wako wa zamani, Chino?
Marioo: Mimi na Chino ni zaidi ya familia, yeye kuacha kufanya kazi na mimi na kuondoka kutoka kwangu sio ndio kama kumezaa uadui. Tena nikupe hii, Chino kaondoka kwangu lakini bado ananiandalia madansa wake kwa ajili ya shoo zangu nyingi tu. Chino ana chuo cha madansa na napenda anavyopambana kwenye kuimba pia.
Ulishawahi kuwa na bifu na msanii yeyote?
Marioo: Mimi sina bifu na msanii yeyote, ila vita yangu iko kwenye kufanya kazi, napambana kutoa kazi nzuri nikiwa studio, maana najua wasanii tupo wengi na kila mtu anatamani kutoa kazi nzuri. Na mimi hata kama ikitokea kuna ugomvi na msanii mwenzangu mimi nitakuwa wa kwanza kulimaliza kwa uwezo wangu, sipendi mabifubifu mimi.

Wewe ni Team Kiba, Diamond au Harmonize?
Marioo: Mimi sina timu kwa kweli hawa wote ni kaka zangu na nafanya nao kazi vizuri tu, sihitaji kujiingiza kwenye matimu naona yatanishusha tu kwenye muziki wangu.
Hivi usingekuwa mwanamuziki saa hizi ungekuwa nani?
Marioo: Kwa kuwa nilianza kuwa fundi gereji kisha ndio nikaingia kwenye muziki, basi isingekuwa muziki ningekuwa fundi gereji tena wa kuchomelea.
Mafanikio gani unajivunia kwenye muziki?
Marioo: Mafanikio yapo mengi tu ukiachana na kufungua lebo yangu yangu ya Bad Nation na tayari nishaanza kusajili wasanii nikianza na Stan niliyeshirikiana kwenye wimbo mpya wa 2025, na bado wataendelea kusajiliwa wasanii wengine tena hapo baadaye. Kikubwa kwasasa napenda watu wajue tu muziki wangu.