Mambo 4 yanayombeba Shilole kwa wanaume

Muktasari:
- Hata hivyo, wawili hao waliachana na Shilole akaanguka kwa Ashrafu Uchebe, nayo ndoa hiyo ikavunjika, akaja kuolewa na mpiga picha maarufu Rommy 3D ndipo Rich akaokoa jahazi na mwanadada huyo ameyataja yanayomfanya apendwe kwa staili ya kata mti panda mti.
MSANII na mfanyabiashara, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ameifichua mambo manne yanayombeba kiasi cha kupendwa na wanaume.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shilole ambaye anaigiza na kuimba muziki wa kizazi kipya, ameyataja mambo hayo yanayombeba na yanayomfanya apendwe sana, akirejelea safari yake ya uhusiano baada ya hivi karibuni kuvishwa tena pete mara baada ya kuachana na Rommy 3D.
Shilole alivishwa pete ya uchumba Desemba 23, 2024 na mpenzi wake wa sasa, Rich, lakini kabla ya huyo alishawahi kuolewa na dereva wa malori enzi akiwa na umri wa miaka 17 na kuja kuishia naye Dar es Salaam wakitokea Igunga Tabora.
Hata hivyo, wawili hao waliachana na Shilole akaanguka kwa Ashrafu Uchebe, nayo ndoa hiyo ikavunjika, akaja kuolewa na mpiga picha maarufu Rommy 3D ndipo Rich akaokoa jahazi na mwanadada huyo ameyataja yanayomfanya apendwe kwa staili ya kata mti panda mti.
1. Kujiamini
Hii ndiyo sababu kubwa ya kwanza aliyoitaja Shilole. Anasema hamna kitu kinachowavutia watu, hasa wanaume kama kujiamini. Mwanamume anapenda msichana anayejiamini. “Hamna kitu nachoweza kusema zaidi ya kujiamini mahala popote.”
2. Kujitegemea
Shilole anasema hamna kitu kinachowaboa wanaume kama mwanamke ambaye anapenda vitu vya kupewa. Ukimwonesha mwanamume unapenda kutafuta vya kwako basi jua atakupenda sana. “Najivunia kwa hili mie ni mpambanaji najiweza kujitegemea.”
3. Kupendeza
Shilole alisema ni muhimu kwa wadada kuvaa nguo nzuri ambazo zitakupendeza kulingana na mwili wako hasa hasa nguo zenye rangi ya kuonekana.”
Ukiniangalia mavazi yangu ninayovaa huwa napendeza sana na yanavutia kwa mwanamume yeyote yule, hicho ni kigezo kingine cha kupendwa na wanaume.”
4. Tabasamu
Tabasamu kila saa, kwani linakufanya unaonekana mzuri zaidi.
“Muda wote mimi napenda kutabasamu kitu ambacho kinawavutia wanaume kunipenda, ukiwa na tabasamu muda wote unaonekana una mvuto,” alisema Shilole na kufafanua kwa sababu hizo, zimechangia kuwa na nyota ya kupata mwanamume haraka pale anapokuwa amemwagana na mwingine, kwa vile sifa hizo hazipo kwa wadada wengi wa mjini.
“Haya nimekupa hiyo, maana watu wanasemaga ooh kwa nini napenda kuolewa kila wakati au kupata mchumba kwa muda mfupi, hizo ndio sababu zangu ambazo ninazo mimi na hutazipata kwa mwanamke yeyote zote hizo,” alisema Shilole.