Majizo: Wafuasi wengi mitandaoni si kigezo cha ubora kwa msanii

Monday April 19 2021
youtube pic
By Nasra Abdallah

Mfanyabiashara na mmiliki wa kituo cha redio Efm  na Tv E, Francis Ciza ‘Majizo’ amesema wasanii wanaojiona kuwa wakali kutokana na kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, wanajidanganya.

Majizo amesema hayo leo Jumatatu Aprili 19, 2021 alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Joto la asubuhi kinachurushwa na redio ya Efm.

Majizo ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mtangazaji kama anapendezwa na mambo ya wasanii yanayoendelea sasa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo kuitumia mitandao hiyo kusukuma muziki wao kwa kufanya kick na mambo mengine.

Akijibu, mfanyabiashara huyo amesema wasanii kwanza wanapaswa kuelewa kufuatiliwa na watu wengi kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram na youtube, haimaanishi kuwa ni  wasanii wakali au wakubwa kwa kuwa mitandao hubeba kila kitu na ndio maana kuna waliokuwa maarufu na sio wasanii.

“Mnaodhani kuwa na wafuasi wengi huko youtube au Instagram ndio kuwa wasanii wakubwa mnajidanganya, mitandao imekuja kwa ajili ya kuongezea tu thamani kazi zenu.


Advertisement

“Mfano uko wazi kwa msanii wa singeli Mzee wa Bwax, wimbo wake huko youtube hauna hata watazamaji 800,000 lakini leo hii ni maarufu na ni msanii mkubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Mwingine ni msanii Msaga Sumu, hata Instagram alikuwa hana, mpaka nilipomfungulia hivi majuzi. Wasanii wengine kama Profesa J, Pico na wimbo wake wa Bibi Kikongwe, Daz Baba na wimbo  wake wa mrembo namba nane, Feruzi na wimbo wake wa Starehe zote hizi ziliwika bila ya kick.”.

Kutokana na hilo, ameishauri Serikali kuchukua hatua mapema kwa wasanii wanaotumia kick kwa lengo la kusukuma muziki wao kwa kueleza watu kama hao wanarudisha ile dhana kwa wazazi kuona kazi ya muziki ni uhuni.

Kwa upande wa Basata, amesema wanapaswa wasimuonee mtu aibu katika kumuwajibisha, bila kujali ukubwa wa jina alionao kwa kuwa wasanii wanaochipukia wataona ni kawaida ili kutoa muziki lazima ufanye kick.

 “Vyombo vya dola navyo  vitekeleze wajibu wake kwa kuwa si kila kitu kinaweza kufanywa na Basata, kwani makosa mengine yanaangukia kwenye sheria ya makosa ya jinai,”amesema.

Mfanyabiashara huyu ambaye pia amewahi kuwa DJ, amesema anaamini mbali na wadau wa muziki kuumia akiwemo yeye, wapo walioupigania muziki huo hadi kufika kuwa biashara.

“Kuna watu wamekuwa na mchango mkubwa katika muziki wetu hadi kuifika hapa  watu kujipatia ajira wakiwemo watayashaji muziki waliobadili nyumba zao kuwa studio kama akina P Funk Majani, Enrico Records na Master J ambaye alikuwa akikesha studio,” amesema.

Advertisement