Maeneo matano ulipo ushindani wa Rayvanny na Harmonize

Monday September 20 2021
maeneo pc
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva toka WCB Wasafi, Rayvanny amemtambulisha msanii wa kwanza aliyesainiwa chini ya lebo yake ya Next Level Music (NLM), Mac Voice tangu kuanzishwa kwake Machi 2021.

Kabla ya kusaini NLM, Mac Voice tayari ameshasikika kwenye Bongofleva kwa kipindi cha nyuma ambapo alikuwa chini ya usimamizi wa Chege.

Rayvanny ambaye anakuwa msanii kwanza kuanzisha lebo akiwa bado chini ya WCB Wasafi, ameweka wazi kuwa Sepemba 24, 2021 ndipo Mac Voice ataachia ngoma yake ya kwanza.

Hata hivyo, tarehe hiyo tayari lebo ya Konde Music Worldwide ya Harmonize walikuwa wametangaza ndio siku ambayo msanii wao Cheed ataachia wimbo wake wa kwanza tangu asaini Septemba 2020.

Utakumbuka Harmonize naye alikuwa WCB Wasafi lakini akajitoa na kwenda kuanzisha lebo yake ambayo hadi sasa ina wasanii kama Anjella, Ibraah, Killy, Cheed, Country Boy na Young Skales wa Nigeria.

Kimeumana

Advertisement

Je, kitendo cha Rayvanny kutangaza naye msanii wake ataachia wimbo siku ambayo tayari Konde Music waliitangaza hapo awali kina maana gani kwao wawili hao? Huu ni mwendelezo wa ushindani kati ya Rayvanny na Harmonize. Kivipi?

1. Majina

Wakati anaanza muziki Rayvanny alitambulika kama Raymond baadaye ndio ikaja hiyo Rayvanny, wakiwa wote WCB bado, Harmonize alipoanza kujiita Konde Boy, ndipo na Rayvanny alipokuja na jina la Vanny Boy. Kama hiyo haitoshi, Harmonize alipokuja na jina la Tembo, naye Ravannny akaja na jina la Chui.

2. Kuandaa Shoo

Mara baada ya kujitoa WCB, Desemba 2019 Harmonize alikwenda kufanya shoo yake ya kwanza nyumbani kwao, Mtwara na kufanyiwa tambiko kwa kupakwa damu ya ng'ombe. Haikuchukua zaidi ya wiki mbili, naye Rayvanny akafanya shoo nyumbani kwao Mbeya katika tamasha alilolipa jina la 'Home Coming' ambalo lilikuwa halina viingilio.

3. Kuimba Singeli

Februari 8, 2020 Harmonize aliachia video ya wimbo wake wenye mahadhi ya Singeli wenye jina la 'Hajanikomoa' na kutamba kuwa ndio ya kwanza ya Singeli kufikisha watazamaji milioni moja katika mtandao wa YouTube, ambapo hadi sasa wamefika milioni 2.8.
Kufika Machi 29, 2020 Rayvanny akaachia video yake ya Singeli yenye jina la 'Miss Buza' ambayo kwa sasa ndio video ya Singeli iliyotazamwa zaidi YouTube ikiwa na watazamaji milioni 8.9.

4. Albamu na EP

Mara baada ya Harmonize kuachia albamu yake ya kwanza ya Afro East yenye nyimbo 18 na Extended Playlist (EP) 'Afro Bongo' yenye nyimbo nne, Rayvanny naye akaja kutoa albamu, Sound From Africa ikiwa na nyimbo 23, pia na EP 'Flowers' yenye nyimbo sita.

5. Tuzo

Mwaka 2016 Harmonize alishida tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) toka Marekani kama Msanii Bora Chipukizi, mwaka mbele, 2017 naye Rayvanny akashinda tuzo ya BET zilizotolea pia nchini humo kama Msanii Bora wa Kimataifa Chaguo la Wengi.

Advertisement