Lil Wayne na mfumo wa 4:4:2 katika familia

MFUMO unaotumiwa na makocha wengi wa soka uwanjani, 4:4:2 ndio huo ameutumia rapa maarufu duniani, Lil Wayne, 40, tangu mwaka 1998 katika kuipangilia familia yake akiwa ni baba wa watoto wanne kwa sasa.

Utakumbuka Lil Wayne alivuma baada ya kuachia albamu yake ya nne, Tha Carter (2004), albamu yake ya sita, Tha Carter III (2008) ilimpa heshima zaidi kufuatia kushinda Tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Rap.

Albamu ya Tha Carter III ilikuwa na nyimbo kali kama A Milli, Got Money na Lollipop ambao uliandika rekodi kama wimbo wake wa kwanza kushika nafasi ya kwanza chati za Billboard Hot 100.

Mfumo wa 4:4:2 kwa Lil Wayne unatafsiriwa kwa kitendo chake cha kuzaa watoto wake hao wanne na wanawake wanne tofauti ambao wote ameachana nao kwa sasa, huku watoto wake wawili wakizaliwa ndani ya mwaka mmoja, 2009.

Lil Wayne ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Young Money Entertainment katika watoto wake wanne ana binti mmoja tu, Reginae Carter, 24, ambaye ndiye wa kwanza na alimpata akiwa shuleni.

Katika mahojiano na Jarida la Ozone mwaka 2010, Lil Wayne alifunguka kuhusu uhusiano wake na mama wa watoto wake na ukosoaji ambao anakumbana nao kama mtu aliyezaa watoto wanne na wanawake wanne tofauti.

“Sidhani kile ambacho watu wanafikiri kinapaswa kuwa wasiwasi wa mtu yeyote, kwa hakika sio jambo langu. Ningekuwa na wazimu kama ingekuwa hivyo na wewe ni wazimu ikiwa unafikiria hilo, sijali kile ambacho watu wanafikiri au kusema.” anasema Lil Wayne.

Lil Wayne, mshindi wa tuzo tano za Grammy na 11 za BET huku akiuza rekodi zaidi milioni 200 duniani, ni lini na kina nani hao ambao amewatumia katika mfumo wake wa 4:4:2?, makala haya yanakudadavulia zaidi;.


1. Reginae Carter - 1998

Mtoto wake wa kwanza, Reginae Carter alizaliwa Novemba 29, 1998 wakati huo Lil Wayne akiwa na miaka 16, alikuwa bado ni mwanafunzi wa sekondari, alizaa na Toya Johnson ambaye walifunga ndoa mwaka 2004 na walichana kwa talaka mwaka 2006.

Kwa sasa Reginae ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Clark Atlanta na anafuata nyayo za wazazi wake kama mwigizaji, mwanamuziki na mwandishi, amecheza filamu kama Dear Santa, I Need a Date and Pride and Prejudice: Atlanta n.k.

Ameshiriki vipindi vya televisheni kama Growing Up Hip Hop Atlanta na T.I. na Tiny: Friends and Family Hustle ambacho mama yake pia anaigiza, ameandika kitabu kimoja, Paparazzi Princesses, huku akiwa sehemu ya Kundi la Muziki, OMG Girlz.


2. Dwayne Carter III - 2008

Lil Wayne akiwa na uhusiano na Mtangazaji, Sarah Vivan ambaye alifanya kazi vituo vya redio, Streetz 94.5 na iHeartMedia, walijaliwa mtoto wao, Dwayne Carter III aliyezaliwa Oktoba 22, 2008.

Wawili hao ambao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye moja ya matamasha za rapa huyo, kwa kupendeza wamempa mtoto wao jina lingine la utani, Lil Tuney, kubwa zaidi alionekana katika mixtape baba yake, No Ceilings 3 (2020).

“Ninavutiwa sana na wewe, endelea kuwa mtu halisi na kuongoza njia yako mwenyewe, ninakupenda na sijali una umri gani, hivyo sitaacha kamwe kukupiga mabusu,” aliandika Sarah Instagram katika siku ya kuzaliwa Dwayne.


3. Kameron Carter - 2009

Kipindi ana uhusiano na Mwigizaji, Mwanamitindo na Mtangazaji wa TV, Lauren London, Lil Wayne alijaliwa kumpata mtoto wake wa kwanza wa kiume, Kameron Carter aliyezaliwa Septemba 9, 2009.

Lauren aliliambia Jarida la Essence hapo Oktoba 2020 kuwa licha ya uhusiano wao kuvunjika, wawili hao wanabaki kwenye uhusiano mzuri wanapomlea mtoto wao baada ya hapo awali kujaribu kufufua penzi lao ila ikashindikana.

“Tulikuwa kwenye uhusiano ambao haukufanikiwa, tulichumbiana kwa muda mfupi miaka iliyopita, lakini hatimaye tuliachana, baba wa mwanangu ni mtu mwenye akili, mwenye upendo na anayependwa na ambaye atakuwa rafiki siku zote.” alisema Lauren.

Kameron ambaye naye alionekana kwenye mixtape baba yake, No Ceilings 3, katika siku yake kuzaliwa alipotimiza miaka 12, mama yake alimtaja kama mtu  shujaa, mwenye nguvu na aliyejaa uadilifu.


4. Neal Carter - 2009

Ndiye mtoto wa mwisho wa Lil Wayne, Neal Carter alizaliwa Novemba 30, 2009, mama yake ni Nivea, mwimbaji anayejulikana kwa vibao kama Don’t Mess With My Man, Laundromat na Complicated.

Neal Carter naye alikuwepo katika mixtape ya No Ceilings 3, katika siku yake ya kuzaliwa ya 11 mwaka jana, Nivea aliandika ujumbe mtamu Instagram kumusu Neal au Young Carter.

“Kwa muda wote umekuwa mzuri, nafurahi sana kumuona mwanaume ambaye unakua, utakuwa mtoto wangu daima, nakupenda upendo usio na kikomo.” anaandika Nivea.

Ikumbukwe Lil Wayne alianza muziki mwaka 1997 baada ya Rapa Birdman kumsanini Cash Money Records na kuwa msanii mdogo zaidi katika lebo hiyo kwa wakati huo.

Chini ya Cash Money jina lake lilitambulika duniani hadi mwaka 2018 walipoachana rasmi akiwa tayari ameanzisha Young Money Entertainment.