Kwanini Rayvanny anataka kurudiana na Beyonce?

STAA wa Bongofleva kutoka Next Level Music (NLM), Rayvanny katika Extended Playlist (EP) yake, Flowers II iliyotoka Februari 10, 2022 ikiwa na nyimbo tisa, ndani yake kuna wimbo unaitwa Bonnie & Clyde.
EP hiyo iliyotoka akiwa bado chini ya WCB Wasafi ilishirikisha wasanii sita ambao ni Zuchu, Roki, Ray C, Marioo, Guchi kutoka nchini Nigeria na Nadia Mukami kutoka Kenya.
Wimbo huo, Bonnie & Clyde, kwake Rayvanny ulikuwa unazungumzia mapenzi yake na Paula ambayo yalikuwa yamepamba moto na kuteka mazungumzo hasa mitandaoni, ingawa kabla ya wimbo huo kutoka tayari alikuwa akiita ‘couple’ yao, Bonnie & Clyde.
Ni Paula huyu ambaye alionekana katika video ya wimbo wa Rayvanny ‘Wanaweweseka’ ambao pia upo kwenye EP hiyo (Flowers II). Hii ni kazi ya kwanza ya sanaa kufanya pamoja kama Bonnie & Clyde.
Historia inawataja Bonnie &Clyde kama wapenzi waliopendana sana tena kwa dhati lakini waliishi maisha ya uhalifu hadi kusababisha kufa pamoja katika tukio la uhalifu Mei 23, 1934.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutoka video hiyo Septemba 10, 2021 waliachana, ila wiki hii Rayvanny alichapisha picha ya Paula Instagram na kuweka alama za upendo. Hilo linaweza kutafsiriwa kuwa anataka kurudiana naye. Kwa kifupi, Clyde anataka kurudi kwa Bonnie.
Rapa wa Marekani, Jay Z akiwa kama Clyde, Bonnie wake ni mkewe Beyonce ambaye alimshirikisha katika wimbo wake 03 Bonnie & Clyde aliouachia Oktoba 10, 2002 kutoka kwenye albamu yake ya saba The Blueprint 2: The Gift & The Curse.
Wimbo huu ni sampo ya wimbo wa hayati 2Pac wa ‘Me and My Girlfriend’ unaopatikana katika albamu yake ya tano ya The Don Killuminati: The 7 Day Theory iliyotoka Novemba 5, 1996.
Hata hivyo, Toni Braxton ambaye naye alikuwa amesampo wimbo huo na kutoa wake aliouita Me & My Boyfriend (2002), aliwashutumu Jay Z na Kanye West kama prodyuza kwa kuiba wazo lake jambo ambalo walilikanusha baadaye.
Video ya 03 Bonnie & Clyde ilifanyika Oktoba 2002 huko Mexico ikiongozwa na Chris Robinson, huku Jay Z na Beyonce wakicheza mfano wa tukio la ujambazi katika benki lililofanywa miaka ya 1930 na Clyde Barrow na Bonnie Parker (Bonnie & Clyde).
Mwanzoni Jay Z anaonekana akiendesha gari aina ya Aston Martin Vanquish. Kisa chake kinatokana na filamu ya uhalifu na mapenzi ya True Romance (1993) ambayo wanaigiza Christian Slater na Patricia Arquette.
Jay Z na Beyonce wanapofika hotelini wanafunika gari lao ili kuepuka kujulikana. Wakiwa chumbani wakihesabu fedha, polisi wanabaini walipo na kuwafuata lakini wanakuta wameshatoroka. Polisi wanapoweka kizuizi barabarani ili kuwakamatwa wanaambulia patupu pia.
Mwaka 2003 video hiyo ilishinda Tuzo za MTV kama video bora ya Hip Hop, huku 03 Bonnie & Clyde ikifika namba nne kwenye chati za Billboard Hot 100 ukiwa ni wimbo wa pili wa Jay Z kuingiza 10 bora ya chati hizo na wa kwanza wa Beyonce kama solo.
Kama alivyochana Jay Z kwenye wimbo huo ‘All I need in this life of sin, is me and my girlfriend’ (Jambo ninalohitaji katika maisha haya ya dhambi, ni kuwa na mpenzi wangu), ambaye ni Beyonce, ndivyo ilivyo kwa Rayvanny anayejaribu kurudiana na Paula.
Ikiwa ni zaidi ya miezi mitano tangu kutengana kwao hakuna hata mmoja ambaye amewahi kuweka wazi uhusiano wake mwingine ingawa Paula amewahi kuhusishwa na Jay Melody, huku Rayvanny akihusishwa na Feza Kessy.
Utakumbuka kuanza kwa uhusiano huu haikuwa kazi rahisi maana wakati huo Paula alikuwa ni sehemu ya familia ya Harmonize aliyekuwa na uhusiano na Kajala ambaye ni mama wa Paula.
Kitendo cha Rayvanny kumchukua Paula kilichochea bifu kali kati yake na Harmonize hadi kusababisha kuachana na Kajala kisha kuwaburuza polisi kwa madai ya kumdhalilisha mitandaoni. Ila baadaye Kajala alirudi kwa Harmonize, huku Paula akiwa ameachana na Rayvanny.
Na sasa Rayvanny anataka kumrudisha Paula katika himaya yake. Ni wazi anajua akifanikiwa utakuwa ushindi mwingine kwake dhidi ya Harmonize ambaye ni hasimu wake kimuziki. Jinsi walivyowahi kujitambulisha kama Bonnie & Clyde pengine Rayvanny anajua akiwa na Paula, basi kila pambano kutoka kwa hasimu wake litakuwa rahisi kulishinda na kulishika soko la muziki.