Kwaheri Director Khalfan wasanii watakumisi kwa video zako tamu

Muktasari:

  • Khalfan amezikwa leo saa 10 kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na ameacha  mke ambaye ni mjamzito wa miezi saba na mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

ALIFAHAMIKA zaidi kama Director Khalfan, ila majina yake halisi ni khalfan Khamandro. Ni mmoja wa watayarishaji wa video nchini ambaye amefariki dunia leo Jumapili, Mei 5, 2024 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), jijini Dar es Salaam.

Khalfan amezikwa leo saa 10 kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na ameacha  mke ambaye ni mjamzito wa miezi saba na mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MOI, Patriki Mvungi alisema, “Ni kweli amefariki saa sita usiku wakati akiendelea na matibabu, Director Khalfani aliletwa hapa kwetu MOI akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili.”

Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza Khalmandro alifikishwa hospitalini hapo akiwa na tatizo la damu kuvilia kwenye ubongo, lililosababisha changamoto ya kupooza upande wa kulia wa mwili wake.

Enzi za uhai wake, Director Khalfan alijizolea umaarufu kutokana na kazi zake bora alizofanya na wasanii wakubwa kama Ben Pol, Christian Bella, Madee, Aslay, Shilole, Nu Mziwnda, Maua Sama.

Wengine ni Navykenzo, Baby Madaha, Chinbees, Bob Junior, Linah Sanga, Q Chilla, na wengine wengi.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti baadhi ya wasanii hao waliowahi kufanya kazi na Director Khalfan walisema haya:


CHRISTIAN BELLA

Huyu ni mwanamuziki wa Dansi, ambaye amewahi fanya kazi na Director Khalfan enzi za uhai wake, na video  za nyimbo ambazo amefanya naye ni  ‘Amerudi’ Hello’ na nyingine nyingi.

“Nimepokea kwa masikitiko sana kifo cha Director Khalfan, mimi nimefanya nae kazi nyingi sana za video ambazo  zimefanya vizuri sana, hakia kifo chake ni pigo sana  jamaa alikuwa anajua sana.”


BEN POL

Ben Pol ambaye amefanya kazi na Director Khalfan kwenye wimbo wa Sophia alisema, “Khalfan alikuwa mtu msikivu sana kwenye kazi zake, mie nishafanya nae kazi nyingi tu ikiwemo video ya Sophia ambayo inaendelea kufanya vizuri hadi sasa.”


MADEE

Msanii huyu ambaye amewahi kutamba na wimbo wa ‘Hela’ alisema; “Hakika kifo ni fumbo kwetu sote, hapa tupo kwenye kikao cha mazishi yake na anazikwa leo, hivyo nizungumze tu kwa ufupi, Khalfan alikuwa ni mchapa kazi na mimi nimefanya nae kazi nyingi kupitia wasanii walionishirikisha kwenye nyimbo zao, na hata  nyimbo yangu ya ‘Hela’ video yake amefanya yeye.”


SHILOLE

Director Khalfani pia aliwahi fanya kazi na mwanamuziki Shilole kwenye video ya wimbo ‘Nyang’anyang’a’ na kwa masikitiko, msanii huyo alisema;

“Mimi namfahamu siku nyingi sana Khalfan na enzi za uhai wake nilikuwa natamani sana kufanya naye kazi na ukweli nilifanikiwa kwenye wimbo wa ‘Nyang’anyang’a’ na aliweza itendea haki ile video na nitamkumbuka  kila wakati kwani ameacha alama kwangu kwenye muziki wangu.”


ASLAY

Naye ni mmoja wa wanamuziki ambao walishawahi fanya kazi na Director Khalfan  kwenye nyimbo kama ‘Naenjoy’ “Nipo njiani naelekea Mtwara ila nasikitika sitakuwepo kwenye mazishi ya Director Khalfan kwani nimefanya naye kazi kwa ukaribu sana, tumwombee apumzike kwa Amani.”


Navy Kenzo

Kundi hili la wasanii wawili ambao ni wapenzi, Nahreel na Aika ni kati ya waliofaidika na kazi za director huyu ambaye nyimbo zake zimefanya vizuri kwenye mitandao ya kijamii hasa YouTube.

Wimbo ‘I just wanna love you’ ni kazi nzuri kutoka kwa Aika na Nahreel ambayo iliingia sokoni Septemba 27 2014 takriban miaka 10 nyuma.

Audio ya wimbo huu iliandaliwa na Nahreel huku Director Khalfan alihusika katika kutayarisha video.


LINA SANGA

‘No Stress’, Sikukumbuki na Nyota ni video za  Lina Sanga alizofanya na Director Khalfan na alikuwa na mpango wa kufanya naye kazi nyingine na kifo chake kimemsikitisha sana na alisema; “Nimesikitika sana kwa msiba wa Khalfan kwani tulipanga nifanye naye video nyingine. Nimeumia sana.”

Wasanii wengine waliofanya kazi na Khalfan Weusi ‘Bado Hujabalehe’, Q Chila ‘Babyoo’ na wengine wengi.