Kwa hili! Hamonize amemshika Diamond pabaya

Sunday November 21 2021
Harmo PIC
By Kelvin Kagambo

NI kama vile Diamond ndiye msanii anayeongoza kwa kuwa na maadui wengi kwenye muziki Bongo Fleva. Tunaposema maadui, sio lazima yeye na msanii anayedaiwa adui yake wawe maadui kweli, mara nyingi mashabiki hutengeneza uadui baina ya msanii na msanii kisha vyombo vya habari na wasanii wenyewe hukuza uadui huo na mwisho wa siku unakuwa uadui kweli. Kwani ni shi ngapi!?

Diamond amewahi kutajwa kuwa na uadui na Alikiba kwa zaidi ya nusu muongo sasa. Pia ametajwa kuwa na uadui na Rich Mavoko, Ommy Dimpoz, Harmonize, Belle 9, Davido, H Baba, Pasha, Marehemu Ruge, bosi wa redio EFM, Majizzo. Pia amewahi kuwekwa ulingo mmoja na Darassa CMG, amewahi kupambanishwa na Aslay hadi Marioo.

Hata hivyo, licha ya kuwa Diamond ana list ndefu ya maadui, lakini wengi ameonekana kuwashinda, tena sio tu kuwashinda, bali kuwashinda mapema kweupe isipokuwa adui mmoja tu ambaye ni Harmonize.

Harmonize ameendelea kuwa adui mgumu zaidi kati ya wengi aliopambanishwa nao Diamond. Uadui huu umedumu kwa miaka mitatu sasa, tangu Harmonize ajitoe kwenye lebo ya WCB mwaka 2019.

Tofauti na maadui zake wengine ambao wengi hawamalizi hata mwaka wakiwa wanashindanishwa naye.

Hadi leo hii, wawili hao, Diamond na Harmonize wanaendelea kutupiana madongo kitu ambacho kinadhihirisha kweli wawili hao wana uadui. Lakini swali la muhimu ni Je, kwa nini Harmonize anaonekana kuwa adui mwenye nguvu zaidi kwa Diamond kiasi uadui wao umedumu kwa kipindi kirefu hivi bila kupoa hata kdiogo? Hizi hapa sababu tatu.

Advertisement


MARAFIKI

Kwenye kitabu cha 48 Laws of Power mwandishi Robert Greene anasema adui hawezi kuwa adui hatari sana ikiwa hajawahi kuwa rafiki yako.

Ni sawa na Fid Q alivyoandika kwenye wimbo wake wa Sihitaji Marafiki; ‘Hakuna adui mbaya kama rafiki yako mwenyewe’.

Kabla ya kivumbi chao tunachokiona leo, Harmonize na Diamond walikuwa marafiki wa muda mrefu sana, kwa mujibu wa Konde Boy mwenyewe anasema urafiki wako ulifikia kiwango cha hadi kuvaliana nguo. Aisee, wanaume wakifikia hatua hiyo, hao ni marafiki hadi wamepitiliza.

Kwa maana hiyo Harmonize anajua karibu kila kitu alichokuwa akikifanya Diamond, yote, mabaya na mazuri. Hivyo ni wazi hata kama Diamond atajitahidi kumshambulia Harmo kwa kiasi gani lakini bado ataacha nafasi kwa sababu anajua kama akizidisha, Harmonize anaweza kuja na bomu zito na likamchafua Diamond mazima.

Mfano mfupi ni juzi, Diamond aliandika kwenye Instagram yake akimsifia Rayvanny kwa kufanya shoo kwenye steji ya kimataifa ya tamasha la MTV EMA lakini kwenye kile alichokoandika akaongeza na sentensi ambazo Harmonize alizipokea kuwa ni dongo lake, kwamba eti Konde Boy anatumia mihadarati.

Hata hivyo, baada ya muda kidogo Harmonize naye akajibu tuhuma hizo kwa kupiga dongo ambalo wanazengo walitafsiri kuwa ni la Diamond, aliandika bila kutaja jina kwamba jamaa anakula ngada.


HARMONIZE ANAAMINIKA

Watu wengi wanamuamini Harmonize kila anaposema jambo kuhusu Diamond, hiko ndicho unachoweza kukisema kupitia data za kama vile maoni yanayotolewa na watu kwenye mitandao ya kijamii kila Harmonize anapomzungumzia Diamond, nyingi zinaonekana kumuunga mkono na kumuamini.

Kwa mfano, mahojiano yake aliyofanya wiki hii, alizungumzia figisu alizofanyiwa na lebo yake ya zamani tangu ameachana na lebo hiyo.

Hata kama stori hiyo ni ya upande mmoja, kwamba inaweza ikawa ni uongo, lakini watu wameona kwa mujibu wa maoni yaliyokuwa yakitolewa kwenye video za mahojiano hayo.


WANAFANANA KIMUZIKI

Muziki wa Diamond na Harmonize hauna tofauti sana, hapa tunazungumzia kisanii, vitu kama vile uandishi na uimbaji.

Harmonize anaandika kwa kiwango sawa au cha kukaribiana na Diamond, anaimba kwa kiwango cha kukaribiana na Diamond, ni msanii mwenye matukio ya mtindo wa kukaribiana na Harmonize, mara maskendo, mara wanawake.

Kwa hiyo ni mtu ambaye ukimuweka kwenye ulingo mmoja na Diamond katika nyanja hiyo Diamond atapata tabu.

Hiyo ni tofauti na watu wengine waliowahi kushindinishwa na Diamond. Kwa mfano Alikiba anafanya muziki tofauti kabisa na Diamond, kuanzia uandishi, uimbaji hadi aina ya video anazotengeneza.

Advertisement