Kumbe Nandy ana kiherehere

Saturday January 15 2022
nandy pic
By Charity James

MWANADADA anayefanya vyema kwenye muziki wa kizazi kipya nchini, Nandera Mfinanga ‘Nandy’ amefunguka kwenye kazi yake ya sanaa yeye ni kiherehere na mshindani kwelikweli.

Nandy amekuwa msanii bora kwenye tasnia ya muziki huku mashabiki wakimlinganisha na Zuchu anayefanya vizuri chini ya leo kubwa inayomsimamia ya WCB.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nandy alisema anakubali kazi za wasanii wenzake na amekuwa mfuatiliaji mkubwa kwa lengo la kujifunza, huku akibainisha kwenye kujifunza anakutana na changamoto ya kutaka kuwa bora zaidi ya mwingine.

“Kwenye kizuri mimi nakubali na hujipanga kufanya kitu kikubwa zaidi ili niweze kuwa juu ya yule aliyefanya kitu bora, ndio siri ya mafanikio ya kuwa vizuri kwenye muziki wangu,” alisema na kuongeza;

“Mbali na kiherehere cha mafanikio pia mimi ni mkorofi sana na ni mkali, napenda mambo yangu yanyooke na yaende vizuri, pia napenda nyimbo za Injili, ni mwanamke niliyelelewa kwenye mazingira ya dini, nimetokea kule hadi kuingia huku,” alisema.

Akizungumzia mipango yake mwaka huu, Nandy alisema kwa upande wake amekuwa akipanda kila mwaka na hadi alipo sasa hajawahi kuelewa amefikaje huku akiweka wazi anatarajia makubwa zaidi mwaka huu kwani ndoto yake ya kuwa msanii mkubwa zaidi anaiona kila anavyozidi kukua.

Advertisement
Advertisement