Konde Gang wazua balaa, TMK Wanaume shangwe kwa Mkapa

ILIWACHUKUA dakika moja mashabiki wa Yanga kuacha kuangalia kinachoendelea uwanjani, wakigeuzia macho kwa msanii wa bongo flava, Konde Boy.

Konde Boy ameingia Uwanja wa Benjamin Mkapa, dakika ya 43 akiwa ameongozana na mabaunsa wake kwa namna alivyokuwa anozongwa na mashabiki walimpitisha eneo la dharura kukaa VIP B.

Shangwe zilielekezwa kwake, naye hakuwa nyuma kuwapungia, jambo lililozidisha shangwe zaidi huku akisindikizwa na macho yao eneo alilotafutiwa kukaa na wasanii wake.

Baada ya kutafutiwa eneo la kukaa, dakika za kipindi cha pili zikiwa zimeyoyoma ndipo mashabiki wakageuzia macho uwanjani.

Lakini wapo wale ambao waliamua kuendelea kukakomaa naye kushangalia.

Ukiachana na shangwe walizompa Konde Boy mashabiki wa Yanga, amewaweka kwenye wakati mgumu wasanii wa lebo yake Country Boy na Ibra ambao waliovalia jezi ya uzi wa Simba.

Ibra baada ya kuvuliwa jezi yake na mashabiki wa Yanga alivalishwa jezi ya Yanga, huku Country akiigomea uzi huo wa kijani na kubakia kufua wazi.

Upande wa mashabiki wa Yanga wanaongoza kwa bao 1-0 kupitia kwa Michael Sarpong penalti dakika 31, walionekana na shangwe zaidi, Simba imepoa.

Mbali na Konde Gang, kundi la TMK wanaume Halisi, limepagawisha umati wa mashabiki wakati Yanga na Simba, zikipasha misuli kujiandaa na mechi yao ya watani wa jadi.

Wasanii wanaounda kundi hilo ni Juma Nature, Mh Temba, Dolo na KR Mura walipiga nyimbo zao mbalimbali za zamani kama Lazia, Chama Kubwa Temeke, Kamua, Hili Gemu na nyinginezo, zilizofanya mashabiki wapagawe.

Japokuwa upande wa mashabiki wa Yanga ndio unaonekana una shangwe zaidi na nyimbo hizo.

Nature alijaribu kwenda upande wa Simba kuleta amshaamsha ulionekana kukausha kwani alikuwa amevalia sweta la kijani.

Hata baada ya kumaliza shoo hiyo, bado upande wa mashabiki wa Yanga ulionekana bado una hamu ya kutaka mastaa hao waendelee kuimba.

Ukiachana na wasanii hao kupagawisha mashabiki wa Yanga, bado upande wa Simba ulionekana umepoa hata baada ya kuondoka uwanjani.