KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Wasanii watakaotumbuiza hawa hapa...

DOHA, QATAR. NI miezi imepita tangu wimbo maalumu wa kusherehesha fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar, Novemba mwaka huu, ulipoachiwa rasmi na kwa mara ya kwanza msanii wa Kimataifa kutoka Nigeria, Davido ameshirikishwa kwenye wimbo huo akiungana na wasanii wangine Trinidad Cardona na Aisha. Wimbo huu wa Kombe la Dunia unaitwa Hayya Hayya (Better Together).

Davido ameweka historia Afrika na atatumbuiza kwa mara ya kwanza pamoja na wasanii wenzake walioshirikiana kuimba wimbo huo wenye mahadhi ya reggae na Kiarabu kwa mbali.

Wimbo huu wa Kombe la Dunia umelenga burudani kwa mashabiki na kufurahia fainali hizo ambazo kwa mara ya kwanza zitazofanyika katika Falme za Kiarabu. Wimbo huu utaimbwa mbele ya mashabiki wakati wa ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba 21 na kumalizika Desemba 18 mwaka huu.


LIL BABY, OZUNA KUTUMBUIZA QATAR

Mbali na wimbo huo, msanii wa Kimataifa kutoka Puerto Rico, Ozuna ameshirikishwa katika wimbo mwingine maalumu wa Kombe la Dunia unaofahamika kwa jina la Arhbo. Naye rapa maarufu kutoka Marekani, Lil Baby amethibitisha atatumbuiza kwenye ufunguzi wa Fainali za Kombe la Dunia baada ya kutoa wimbo maalumu wa fainali hizo unaoitwa ‘The World Is Yours To Take’.

Hiyo inakua mara mara ya kwanza kwa msanii kwa rapa huyo kutumbuiza kwenye mashindano makubwa duniani kama Kombe la Dunia.

Msanii huyo amethibitisha rasmi kupitia akaunti zake za kijamii Twitter na Instagram kwamba atatumbuiza katika sherehe za ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Kwa upande wa mashabiki wake wameipokea taarifa hizo kwa furaha na kumtakia kila kheri.

Baadhi ya mashabiki wamekuwa na maswali mengi kuhusu Shakira kwani msanii huyo mpaka sasa bado hajatoa wimbo wa Kombe la Dunia kama alivyozoeleka. Shakira aliwahi kutoa nyimbo mbili za fainali tofauti za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na Brazil mwaka 2014 na kukubalika na mashabiki. Wimbo wa Kombe la Dunia alioimba katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 maarufu ‘Waka Waka’ umeweka rekodi YouTube kwa kutazamwa zaidi ukifikisha views bilioni 3.4.

Imethibitishwa ‘Feel Magic in the Air’ ni wimbo utakaotambulisha rasmi fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka huu, wimbo huo umeimbwa na msanii maarufu kutoka Morocco, Ahmed Chawki. Vilevile kutakuwa na burudani nyingine za kitamaduni zitakazoandaliwa na vikundi mbalimbali kutoka Qatar ambao ni wenyeji wa fainali hizo.


BURUDANI NYINGINE

Mbali na burudani hizo yameandaliwa matamasha mbalimbali ambayo yatafanyika katika ukumbi wa Arcadia wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 15,000 kwa wakati mmoja.

Ukumbi huo utakua na kila aina ya burudani kama chakula na vinywaji ambavyo vitauzwa kuanzia asubuhi hadi usiku. Vilevile mashabiki watapata nafasi ya kuangalia mechi kupitia televisheni kwa wale watakaopenda, imeelezwa pombe kali haitaruhusiwa kuuzwa ndani ya uwanja na imethibitishwa rasmi hivyo mashabiki wamepewa tahadhari.

Tamasha hilo kubwa litakuwa la aina yake na haijawahi kutokea duniani.

Hata hivyo waandaji wa tamasha hilo bado hawajaweka wazi gharama za matumizi kwa mashabiki lakini imeelezwa pombe kali itapatikana kwa Pauni 8.

Lakini tiketi za kuingia ndani ya tamasha hilo itagharimu Pauni 50 kwa mtu. Kiwango hiki cha pesa kimewekwa ili kuzuia mashabiki kurundikana na kusababisha tafrani wakati burudani mbalimbali zikiendelea.