Kisa utajiri, Diamond awacharukia Forbes

Muktasari:
Wiki moja baada ya jarida la Forbes kutoa orodha ya wanamuziki tajiri zaidi barani Afrika, staa wa bongo fleva Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ameibuka na kukanusha taarifa za utajiri wake zilizoainishwa.
Dar es Salaam. Wiki moja baada ya jarida la Forbes kutoa orodha ya wanamuziki tajiri zaidi barani Afrika, staa wa bongo fleva Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ameibuka na kukanusha taarifa za utajiri wake zilizoainishwa.
Kwa mujibu wa jarida la Fobers, mwanamuziki huyo anashika nambari 20 yenye thamani ya dola milioni 5.1 (Sh11.8 bilioni).
Akijibu suala hilo, Diamond aliandika akisema jarida hilo linapaswa kufanya uchunguzi kwanza wakati mwingine kabla ya kumuweka kwenye orodha hizo.
Siku ambayo alifanya makubaliano yake rasmi ya Mzikii, mwimbaji ambaye alionekana kukasirishwa sana na Forbes aliandika kwenye ukurasa wake wa instagram, 'FORBES: wakati mwingine kabla hamjaniandika tafuteni taarifa hata kupitia google itanijulisha ninafaa kabla ya kuniweka kwenye orodha yenu ya wasanii wajinga matajiri zaidi wa Afrika.”
Kauli ya nyota huyu imewaibua mashabiki wake ambao wametoa ushauri mbalimbali kwa nyota huyo.
Cleo Maungo amesema, “Atumie akili! Forbes wao ni wakadiliaji tu kupitia mali unazomiliki na streams unazopata katika platform za muziki. Pia maisha unayoishi.”
Brandy Charles, “Usitumie nguvu kuingia forbes, namba hazidanganyi hawa Forbes hawajaanza leo na wanajua nini wanafanya labda waandae orodha ya hapa kwetu bongo halafu ndio ulalamike lakini kwa Afrika kwanza hiyo waliyokupa wamekupendelea sababu bado unatakiwa kuendelea kukazana achana na Forbes.”
Zakwetu Artists kaandika, “Inamaana Simba huna mpunga unaozidi $ 1M. Hii ni hujuma hii. Eti hadi Akothee kakuzidi. Forbes wameanza siasa. Simba sasa kama vipi weka data wazi Tanzania tutambe.”
Zimba Magari, “Usipige kelele kwa vitu vidogo, list ya forbes haiathiri wewe kupata endorsments mpya, haiathiri wewe kukuwa zaidi. Ile ni kama wake up call tuu acha iwe vile vile wewe wekeza zaidi.”
Darmakazi, “Hapa kinacho angaliwa ni Net worth =Asset - Liabilities, na sio Cash unayo miliki. Na kama ungenunua ile private jet basi ungejitoa rasmi kwenye hiyo top 30 na kuhamia top 100 maana ungekua na nafasi kubwa.”