R Kelly akimbizwa hospitali kwa kuzidishiwa dawa gerezani

Muktasari:
- Inaelezwa kwamba mwanamuziki huyo alipatiwa dozi kubwa ya dawa na mfanyakazi mmoja wa Gereza la FCI Butner Medium I lililopo North Carolina, kwa mujibu wa wakili wake katika hati ya mahakama. Hata hivyo, mawakiliki wa serikali ya Marekani wamekanusha madai hayo.
NORTH CAROLINA, MAREKANI: MWANAMUZIKI mkongwe wa R&B, Robert Kelly maarufu kama R Kelly alikimbizwa hospitali baada ya kuzidishiwa matumizi ya dawa akiwa gerezani, wakili wake amedai.
Inaelezwa kwamba mwanamuziki huyo alipatiwa dozi kubwa ya dawa na mfanyakazi mmoja wa Gereza la FCI Butner Medium I lililopo North Carolina, kwa mujibu wa wakili wake katika hati ya mahakama. Hata hivyo, mawakiliki wa serikali ya Marekani wamekanusha madai hayo.
Kwa sasa, R. Kelly anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya uhalifu wa kingono na biashara ya binadamu kwa ajili ya ngono kutokana na matukio aliyoyafanya miaka mingi kwa watu mbalimbali wakiwamo wanaume na wanawake.
Kwa mujibu wa wakili wake, Juni 10, mteja wake huyo aliwekwa katika chumba kimoja cha gereza akiwa peke yake na kupewa dawa ambazo zilimfanya kuwa na wasiwasi huku akiweweseka.
Siku hiyohiyo inadaiwa kwamba alipewa dawa nyingine na kutakiwa azimeze na siku tatu baadaye Kelly aliripoti kujisikia dhaifu na kichwa kumuuma, huku akianza kuona madoa meusi eneo la juu la macho kabla ya kupoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Duke University iliyopo karibu na gereza.
Katika maelezo ya hati hiyo ya wakili wake, Kelly inadaiwa kwamba alisikika akimwambia mfanyakazi wa gereza, "(tatizo) hili litafungua mzigo mpya wa matatizo.”
Inaelezwa nyota huyo wa muziki alikaa hospitali kwa siku mbili akipatiwa matibabu, na mawakili wake wanadai kwamba wafanyakazi wa gereza walimpa kiasi cha dawa ambacho kingeweza kumuua.
Kwa mujibu wa mawakili hao, Kelly amekuwa akifanyiwa vitendo vya ukatili na wafanyakazi wa gereza na hajapewa matibabu muhimu ya mishipa ya damu iliyoziba tatizo ambalo aliliwasilisha kwao muda mrefu.
Wakati alipopelekwa hospitali, inadaiwa kwamba madaktari waligundua alikuwa na matatizo katika mfumo wa damu na pia kwenye miguu kulikuwa na tatizo ambalo la kiafya linalohitaji afanyiwe upasuaji. Hata hivyo, hakufanyiwa upasuaji na aliondolewa hospitali baada ya siku chache.
Tukio hilo limetokea wakati Kelly akihaha kuomba msamaha wa rais kutoka kwa Rais Donald Trump akidai kuwa analengwa kwenye njama ya kutaka kumuua inayomhusisha kiongozi wa genge la ubaguzi wa rangi gerezani.