King Kiba alipa deni kwa wasanii kimtindo

Muktasari:

  • Staa wa Bongofleva kutoka Kings Music, Alikiba ameamua kutumia nguvu yake ya ushawishi katika tasnia kwa kufanya kazi na baadhi ya wasanii wa ndani, tofauti na mastaa wengi wakubwa kwa lengo la kusukumu muziki wao mbele.

Staa wa Bongofleva kutoka Kings Music, Alikiba ameamua kutumia nguvu yake ya ushawishi katika tasnia kwa kufanya kazi na baadhi ya wasanii wa ndani, tofauti na mastaa wengi wakubwa kwa lengo la kusukumu muziki wao mbele.

Staa huyo akitoa shavu kwa wasanii mwaka huu hajatoa wimbo wowote mpya tangu Oktoba 4, 2021 alipoachia albamu yake ya tatu, ‘Only One King’ yenye nyimbo 16 alizoshirikisha wasanii kutoka nchi tano tofauti.

Kwa wengine wanatazama mpango huo kama kulipa deni baada ya albamu yake, ‘Only One King’ kuwashirikisha wasanii wa Bongofleva walio chini ya lebo yake pekee ambao ni Abdukiba, K2ga na Tommy Flavour.

Mpango huo unatarajiwa kumuondoa Alikiba katika lawama kuwa wasanii wakubwa wenye rekodi lebo Bongo wamekuwa wabinafsi kwa kupendelea kufanya kazi na wasanii walio chini ya lebo zao pekee.

Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Alikiba na Kings Music kwa ujumla, Aidan anasema kuwa huo sio mpango wa menejimenti, bali ni uamuzi wa Kiba kuwapa shavu wasanii wenzake.

Anasema wasanii wengi wanapenda kufanya kazi na Kiba, ila kuna wakati anakuwa na ratiba ngumu inayombana, wakati huu amepata nafasi ndiyo maana amefanya nao.

“Huo ni mpango wake wa kujaribu kuwashika mkono wasanii wa Bongo kuwasogeza alipo. “Hii hafanyi tu kwa wasanii wa ndani, akija msanii wa nje naye anataka washirikiane kuusogeza muziki mbele atafanya hivyo,” anasema Aidan.

Ikumbukwe Alikiba chini ya Kings Music anawasimamia wasanii watatu, Tommy Flavour, Abdukiba na K2ga, huku Cheed na Killy wakiachana na lebo hiyo na kujiunga na Konde Music Worldwide yake Harmonize.

Mei 5, 2022 Alikiba alishirikishwa na Hamadai katika ngoma ‘Niamini’ ambayo imefanya vizuri na kumpatia msanii huyo dili ambazo mwenyewe amesema ni mapema kuziweka wazi.

Hamadai ni miongoni mwa wasanii waliounda kundi la The Mafik.

“Ukubwa wa Alikiba hakuna ambaye haujui, mashabiki wake wamenipokea kwa kishindo, wameipokea ngoma hii kama ambavyo huwa wanapokea ngoma za Alikiba.

“Kwa hiyo imekwenda mbali zaidi ya vile nilivyotarajia, wakati mwingine wasanii waliotutangulia kwa mafanikio ni muhimu kufanya nao kazi kwanza kupata mashabiki wao, pili kupata dili za matangazo na shoo kwa sababu unafahamika na wengi,” anasema Hamadai.

Video ya wimbo huo iliyotoka Mei 5, 2022 imevutia watazamaji zaidi ya milioni 1.1 YouTube na ndio video ya kwanza kwa msanii huyo kufanya peke yake (nje ya kundi) kufikia mafanikio hayo.

“Hii kwangu ni kubwa sana, imenifungulia vitu vingi, moja ya milango iliyofungua ni kupata namba kubwa kama hizo kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali,” anasema na kuongeza:

“Kitu kingine ilichoniongezea ni kwamba Alikiba hana mashabiki Tanzania pekee, ana mashabiki ndani na nje, kwa hiyo imebadilisha kwa kiasi fulani hatua zangu za ukuaji tangu nilipokuwa hadi nilipo sasa, ameongeza zaidi ya mashabiki wapya”.

Utakumbuka Hamadai aliunda kundi la The Mafik akiwajumuisha Phino King na Mbwalamwezi, aliyefariki Agosti 2019. Walikuja kwa kishindo chini ya King Empire na ngoma yao ‘Niwaze’ wakimshirikisha Ruby.

Mei 20, 2022 Alikiba akawa miongoni mwa wasanii wawili walioshirikishwa katika Extended Playlist (EP) ya Maua Sama, ‘Cinema’ iliyotoka na nyimbo saba.

Alikiba alishirikishwa na Maua Sama katika wimbo ‘Nioneshe’, video yake iliyotoka Julai 13, 2022 imeshafikisha watazamaji milioni 1.1 kwenye mtandao wa YouTube, huku Maua akiwa msanii wa pili Bongo kumshirikisha Alikiba ndani ya miaka miwili baada ya Nandy.

Julai 20, 2022 Nay wa Mitego alimshirikisha Alikiba katika ngoma yake ‘Nikikuona’. Video ya wimbo huo ilitoka Julai 28, 2022 na mpaka sasa imefikisha watazamaji zaidi ya 320,000 kwenye mtandao wa Youtube..

Alikiba pia mapema mwezi huu ameshirikishwa na Prodyuza Mocco Genius katika wimbo ‘Napendwa Remix’ baada ya Prodyuza huyo kutengeneza ngoma kadhaa kubwa za CEO huyo wa King Music.

Akizungumza na gazeti hili, Mocco anasema kuwa Alikiba ni miongoni mwa watu waliomsaidia sana tangu mwanzo, ikiwamo kumpigia simu na kumpa ushauri. “Haikuwa kazi ngumu nilipohitaji kufanya naye kazi, ni kama alikuwa anafurahia mafanikio yangu kupitia kwake, hivyo aliniunga mkono na ngoma ikabamba kama nilivyokusudia.

“Kufanya kazi na Kiba ni kitu kizuri, ni mtu ambaye ana mawazo mengi sana, ni miongoni mwa watu waelewa, ana mzuka wa kazi na kufanya kile ambacho wote mnakipenda,” anasema.

Kuhusu mwaka huu Kiba kushirikishwa na wasanii wengi kwenye ngoma zao, Mocco anasema: “Ninachoona ameamua kuwashika mkono vijana wenye utashi wa kufanya muziki na wanaojituma, unaweza kuangalia aliofanya nao kazi siyo waliobweteka, ni wanaopambana kujikwamua kiuchumi kupitia muziki na wenye kiu ya mafanikio hasa. Kwa hiyo kwa ukubwa wake akikupa hata robo ya kile alichonacho kinaweza kukusogeza zaidi,” anasema Mocco.

Mocco Genius kutoka studio za Imagination Sound amefanya nyimbo za mkali huyo wa ngoma ‘Utu’, nyingi, zikiwamo ‘Mshumaa’, ‘Mwambie Sina’ na ‘Toto’ za Kings Music.

Kwa upande wake mtangazaji wa vipindi vya burudani kutoka EFM Radio, B Dozen anasema anachofanya Kiba ni kukuza tasnia kwa kuwapaisha zaidi wasanii ambao wapo na kutanua wigo wa kufahamika.

“Ukimuuliza Hamadai atakuambia hakuna wimbo una mafanikio zaidi kwake kama aliofanya na Kiba, hivyo hii itawezesha watu wengi kufahamu kuhusu vipaji vilivyopo nchini kwa sababu Kiba tayari anajulikana na amefanya kazi na lebo kubwa kama Sony Music.

“Kwa hiyo kwa nafasi yake kufanya kazi na wasanii wa ndani inatoa fursa kwao kufanya kazi na lebo kubwa na wasanii wakubwa Afrika na duniani,” anasema Dozen.

Dozen anasema tofauti na mawazo ya wanaotazama kutoka nje kuwa ameacha kutoa ngoma badala yake anashirikishwa: “Hii ina mchango mkubwa katika tasnia, ili ufanye vizuri lazima kuwe na watu wanaofanya kazi kama yako, utawatumia kujipima na kusonga mbele zaidi.

“Hivi anachokifanya Kiba ni kuinua tasnia na asiishie kwenye kolabo pekee, afanye hivyo hadi kwenye shoo kubwa anazopata.

“Wasanii wakubwa wawape nafasi wasanii wadogo kwenye shoo zao, mfano mtu kama Diamond anaenda kufanya shoo Canada, akimchukua msanii yeyote mdogo akaenda naye kule kama ambavyo wanafanya Wanigeria, tutaikuza hii tasnia yetu sana na kuonyesha kuna wasanii wengine nje ya hawa wakubwa tunaowasikia,” anasema B Dozen.

Kuhusu Alikiba kutoachia kazi yake yoyote tangu kuanza mwaka huu, Meneja wake, Aidan anasema ni kwa sababu albamu ilitoka na nyimbo 16 na haijatimiza hata mwaka tangu itoke, kwa hiyo muda utafika ataachia kazi zake.

Ukiachana na wasanii wa Bongo, Alikiba amefanya kazi na wasanii wa kimataifa kama Sarkodie (Ghana), R Kelly (Marekani), Blaq Diamond (Afrika Kusini), Patoranking, M. I, Rudeboy na Mayorkun (Nigeria), Sauti Sol, Nyashinsksi, Khaligraph Jones (Kenya) na Maud Elka (DR Congo).