Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikii kuzikwa leo, Fredy Aliza

Maziko Pict
Maziko Pict

Muktasari:

  • King Kikii alikumbwa na mauti Ijumaa iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu akiwa ameacha alama kubwa katika muziki wa dansi tangu alivyotua nchini miaka ya 1970 na kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Joseph Kikumbi akizungumza na Mwanaspoti alisema, mwili wa gwiji huyo utazikwa kwenye makaburi ya Kinondoni.

MWILI wa gwiji wa muziki wa dansi nchini, Boniface Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ unatarajiwa kuzikwa leo saa 10 jioni jijini Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni, huku safari ya mwigizaji nyota wa filamu na tamthilia, Fredy Kiluswa ikiwaliza wengi.

King Kikii alikumbwa na mauti Ijumaa iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu akiwa ameacha alama kubwa katika muziki wa dansi tangu alivyotua nchini miaka ya 1970 na kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Joseph Kikumbi akizungumza na Mwanaspoti alisema, mwili wa gwiji huyo utazikwa kwenye makaburi ya Kinondoni.

“Baba tutampuzisha kesho (leo) saa 10 katika makaburi ya Kinondoni, jana (juzi) mwili ulifikishwa nyumbani jioni kutoka hospitalini, tukafanya dua na ukalala hapa nyumbani, leo (jana) mwili utapelekwa Leaders kwa ajili ya ibada na kuagwa baada ya hapo utapelekwa makaburini kwa ajili ya maziko,” alisema Joseph.

King Kiki aliyeugua kwa muda mrefu, amefariki usiku wa kuamkia  Novemba 15 akiwa nyumbani kwake Mtoni kwa Aziz Ali alipokuwa akiendelea kuuguzwa.

Msiba uko kwa Aziz Ali jijini Dar es Salaam, na baadhi ya watu waliofika msibani hapo ni wamekuwa watu wa kukesha kwa kuimba na kucheza nyumbani hapo.

Mkongwe huyo aliyezaliwa Januari Mosi, 1947 amewahi kutamba na bendi mbalimbali tangu akiwa DR Congo, zikiwamo Orchestra Fauvette, Safari Sound (OSS), Marquis du Zaire, King Kiki Double O na La Capitale, Wazee Sugu na nyingine na moja ya vibao vinavyomtambulisha zaidi ni Kitambaa Cheupe.

Nyingine ni Nimepigwa Ngwala, Krismas - Bonne Annee, Kyembe, Mwaka wa Watoto, Mimi Msafiri, Haruna Kaka, Ni Kweli, Mama Kabibi, Kitoto Chaanza Tambaa na kadhalika.

Fred
Fred

Wakati huo huo, wasanii mbalimbali wa filamu nchini wameonyesha kukuguswa na msiba wa mwigizaji maarufu wa tamthilia na filamu kutoka kiwanda cha Bongo Movies, Fredy Kiluswa, aliyefariki dunia juzi, ambapo hadi tulipokuwa tukiingia mitamboni ilikuwa haijafahamika mwili wa staa huyo utahifadhiwa lini na wapi, kwani kikao cha kifamilia kilikuwa kikiendelea eneo la msiba, Tabata Maji Chumvi.

Fredy aliaga dunia juzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila alipokuwa akipatiwa matibabu, ikielezwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na wasanii mbalimbali wa tasnia ya filamu wamemlilia kwa pengo waliloachiwa na msanii huyo.

Fredy ametamba na filamu na tamthilia mbalimbali ikiwamo ya Mzani wa Mapenzi, Koneksheni zinazoonyeshwa katika channel ya Sinema Zetu ya Azam TV, na pia alishawahi kutamba na Tamthilia ya Ripoti iliyoandaliwa na msanii JB aliyesema ameguswa na msiba huo mzito.

Filamu na tamthilia nyingine alizotamba nazo ni Lawama, Ripoti, Slay Queen, Mzani wa Mapenzi na nyinginezo.

Ameliliwa na wasanii wenzake waliotumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuandika namna walivyoshtushwa msiba huo huku wengi wao wakimininika msibani.