Kidoti, Kuambiana wafunika ZIFF 2015

Jokate Mwegelo 'Kidoti'
Muktasari:
Kwa jumla tamasha la mwaka huu lilifana vilivyo kwa burudani iliyotolewa na wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walioshirikishwa na washindi mbalimbali walitwaa tuzo zilizotolewa kwa msimu wa mwaka 2014-2015.
TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) 2015 limefungwa rasmi juzi Jumamosi katika Ngome Kongwe, Zanzibar na kushuhudiwa aliyekuwa nyota wa filamu nchini, Adam Kuambiana ambaye ni marehemu kwa sasa na mwanadada Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ wakifunika mbaya.
Kwa jumla tamasha la mwaka huu lilifana vilivyo kwa burudani iliyotolewa na wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walioshirikishwa na washindi mbalimbali walitwaa tuzo zilizotolewa kwa msimu wa mwaka 2014-2015.
Kwa upande wa Tanzania, baadhi ya filamu zake zilifanya vyema kwa kunyakua tuzo kadhaa huku wasanii wake nao wakifanya yao, ikiwamo kushuhudia marehemu Kuambiana akiibuka kuwa Mwigizaji Bora wa Kiume wa Ziff 2015.
Kuambiana aliyefariki Mei mwaka jana na Kidoti kila moja alinyakua tuzo ya Mwigizaji Bora kwa msimu wa mwaka 2014/2015.
Kadhalika filamu mbili za Kibongo zilitusua kimtindo katika tamasha hilo kwa kunyakua tuzo zikipenya kwenye rundo la filamu karibu 500 zilizoshiriki kinyang’anyiro hicho kwa mwaka huu.
Filamu hizo ni ‘Mr Kadamanja’ iliyoongozwa na kuigizwa na marehemu Kuambiana ambayo ndiyo pia iliyompa tuzo aliyonyakua na nyingine ni Daddy’s Wedding iliyonyakua tuzo mbili.
Tuzo ya kwanza kwa filamu hiyo ile ya Chaguo la Watu (People’s Choice Award), pia kutoa Mwigizaji bora ambaye ni marehemu Kuambiana, wakati Daddy’s Wedding ilinyakua tuzo ya ‘Best Cinematography’ na ile ya Director Bora ambayo ilikwenda kwa Honeymoon Mohamed.
Mrembo Jokate Mwegelo yeye alinyakua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike kupitia filamu ya ‘Mikono Salama’ iliyoandaliwa na Jacob Steven JB.
Jokate aliandika kwenye mtandao wake kushukuru kwa ushindi huo na kuelezea ni moja ya mafanikio aliyokuwa akiyaota na kuwashukuru wote waliompa sapoti katika sanaa yake.
Nayo filamu ya ‘Samaki Mchangani’ ilishinda tuzo za Best Film in Sound, huku tuzo ya Zuku Best Feature Film ikishinda filamu ya ‘Kutakapokucha’.
Katika upande wa European African Film Festival Awards, tuzo ya Best African Film ilikwenda kwa WAZI? FM – Dir: Faras Cavallo.
Filamu bora za ukanda wa Afrika Mashariki EAC-EAFN zilizotwaa tuzo usiku wa kuamkia jana ni pamoja na ‘Going Bongo’ ambayo imetayarishwa na Dean Matthew Ronalds iliyokuwa filamu bora ya mwaka kutoka Afrika Mashariki.
Filamu makala bora kutoka Afrika Mashariki ni Shadow Fighters iliyotayarishwa na Josefine Heimburger pamoja na filamu bora fupi kutoka ukanda huu Angels Of My Face ambayo pia ilitunukiwa tuzo.
Tuzo za SIGNIS kwa mwaka 2015 zilikwenda kwa filamu za Eye of The Cyclone iliyotayarishwa na Dir Sekou Traore kutoka Burkina Faso, WAZI FM iliyotayarishwa na Faras Cavallo pamoja na Life is Waiting ya Lara Lee.
Kwa upande wa tuzo ya Ousmane Sembene filamu iliyotambuliwa kwa mwaka huu ni Uthando ya mwanadada Tulanana Bohela kutoka Tanzania/Afrika Kusini. Zilizoshinda tuzo hizo ni Houkak ya Youns Yousfi (Morocco), Kwaku ya Akosua Adoma Owusu (Ghana) na filamu ya Soko Sonko ya Ekwa Msangi (Tanzania/Kenya).
Kwa mwaka huu Ziff pia ilitoa tuzo tatu mojawapo ikiwa ni ile ya kumuenzi Bi Kidude ambayo ilikwenda kwa filamu ya Price of Love iliyotayarishwa na Hermon Hailay kutoka nchini Ethiopia.
Filamu ya Lifetime Achievement Award, ilikwenda kwa Fatma Alloo na Hassan Mitawi.
Tuzo za Special Jury Prize kwa mwaka huu zilikwenda kwa filamu ya Every Day is a Small Life ya Albane Fioretti, makala bora ilikwenda kwa Papa Machete ya Jonathan David Kane, Filamu fupi bora ikienda kwa Soko Sonko ya Ekwa Msangi, Filamu bora iliyoonyesha kipaji kutoka Afrika Mashariki ikienda kwa Strength of a Woman ya Gilbert Lukalia.
Silver Dhow Award ilikwenda kwa Simshar iliyoandaliwa na Rebecca Cremona huku Golden Dhow Award ikipata filamu ya WAZI? FM iliyoandaliwa na mwongozaji Faras Cavallo.
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Profesa Martin Mhando alisema kwa mwaka huu, filamu kutoka nchini Tanzania zimeongezeka ubora, hali iliyowafanya majaji kutoa maksi za juu katika ukuaji wa tasnia ya filamu nchini.
“Mwaka huu majaji walipokea kazi nyingi sana hasa kutoka Tanzania ambako awali kulikuwa na mwamko mdogo, walipata shida kwa kuwa zilikuwa na kiwango cha juu cha ubora, lakini zikashinda zile zenye vigezo vyote vilivyowekwa na majaji wenyewe. Filamu nyingi zilizotoka Afrika pia zimekua, zinaelezea visa vinavyoeleweka mwaka huu kulikuwa na vigongo,” alisema Prof Mhando.
Naye Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Mahmoud Kombo aliwasihi wasanii wa filamu nchini kulitumia tamasha hilo ili kuhakikisha kwamba wanakua na kusonga katika kazi zao za kila siku kwa kuzingatia mafunzo yanayotolewa kila mwaka katika kipindi cha siku 10 za tamasha hilo.
“Ni vyema wasanii wetu mkalitumia jukwaa hili kujifunza mambo mbalimbali yanayoendelea hapa, lazima mtambue kwamba si Zanzibar pekee inayotoshelezwa na tamasha kama hili, bali ni Tanzania kwa jumla. Hili ni jukwaa kwa ajili ya watayarishaji filamu, waigizaji, waongozaji filamu, waandishi wa miswada ya filamu na wengineo wanaohusika na tasnia hii,” alisema Kombo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ziff.
Wasanii waliotoa burudani katika kusindikiza usiku wa tuzo, katika Ukumbi wa Mambo Klabu ndani ya viwanja vya Ngome Kongwe ni pamoja na Linah Sanga, Barnaba Elias na Christian Bella.