Kajala ajiandae kisaikolojia na haya kwa Harmonize

Kajala ajiandae kisaikolojia na haya kwa Harmonize

MWANDISHI Darren Hardy katika kitabu chake, The Compound Effect kilichouza nakala zaidi ya milioni 1 tangu mwaka 2010, ameeleza kile alichoita ‘Law of compound effect’ ambacho ndicho kimemuwezesha Harmonize kurejesha penzi lake na Kajala.
Law of compound effect inasema; jitihada ndogo zinazojirudia kila wakati zinaweza kuleta matokeo makubwa maishani katika mazingira na rasilimali zile zile.
Ndivyo alivyofanya Harmonize, tangu alipoachana na Kajala alitumia muziki wake kahakikisha anampata tena, akatoa nyimbo nne kwa ajili yake ambazo ni; Vibaya, Mtaje, You na Deka.  
Baada ya nyimbo hizo akaona bado haijatosha kumshawishi Kajala, hivyo akaamua kumnunulia vidani vya dhahabu na gari jipya aina Range Rover. Hii ni kanuni nyingine, The Law of focus.
Ikumbukwe uhusiano wao ulianza Februari 2021 baada ya ndoa ya Harmonize kuvunjika, mwezi mmoja tu wa penzi lao wakaachana kwa ugomvi mkubwa hadi kufikishana Polisi, hiyo ilikuwa Aprili 2021.
Harmonize akawa na Briana kutoka Australia ambaye waliachana Machi 2022, baada ya hapo moyo wake ukamtuma kurejea kwa Kajala, hakusita kufanya hivyo. Hii ni kanuni nyingine, ‘The Law of Diminishing Intent’, inayosema; unavyozidi kusubiri kufanya jambo ambalo unatakiwa kulifanya sasa, ndivyo uwezekano wa kutolifanya unaongezeka.
Kwa sasa Kajala yupo katika himaya ya Harmonize, hata hivyo, kuna mambo anapaswa kujiandaa kukumbana nayo kwani kuna uwezekano mkubwa yakamkuta. Je, ni yapi na kwa namna gani?

MOSI; Hakuna uhusiano wa Harmonize ambao hajawahi kutuhumiwa kwa usaliti na mwenzake au kukumbwa na madai ya usaliti, hiyo imekuwa ni sehemu ya maisha yake.
Wolper aliwahi kudai kuwa Harmonize alianzisha uhusiano na Sarah wakati bado wapo pamoja, alidai sababu ya kufanya hivyo ni kutokana alifuata fedha kwa Sarah ila bado yeye ndio alikuwa anapendwa.
Hata alipokuwa na Sarah, yaliibuka madai kuwa amempa ujauzito msanii wa Kenya, Nicah The Queen kufuatia kuonekana pamoja nchini humo. Licha ya hilo kutokuwa na ukweli wowote, ila kilichokuja kuvunja ndoa yao ni huo usaliti pia.
Ikumbukwe Sarah alitangaza kuachana na Harmonize baada ya mwimbaji huyo kuisaliti ndoa yao na kwenda kuzaa nje, Harmonize alikiri kosa hilo mbele ya umma na kusema hawezi kuikana damu yake hata mara moja.
Alipokuwa na Kajala, huku nako uhusiano wao ukafunikwa na tukio la aibu mara baada ya kuvuja video mtandaoni inayodaiwa ya Harmonize ‘akimtongoza’ mtoto wa Kajala, Paula, hivyo alikuwa anataka kumsaliti Kajala. Hili ndio liliwaachanisha awali.


PILI; Hadi sasa Kajala ndio mwanamke pekee wa Harmonize ambaye hajapelekwa nyumbani kwao Tandahimba, Mtwara kwa ajili ya kumtambulisha kwa wazazi wake. Wolper, Sarah na Briana, wote walifanyiwa hivyo.
Juni 2016 Harmonize alimpeleka Wolper kwa wazazi wake Mtwara na hapo watu wengi wakaamini kuwa kitakachofuata ni ndoa kwani Wolper hata alisema alikuwa tayari kubadili dini. Lakini wapi! Wakaachana.
Sarah alitambulishwa kwa wazazi wa Harmonize Mtwara Machi 2019, wakaja kufunga ndoa Septemba 2019, baada ya mwaka mmoja ndani ya ndoa wakaja kuachana Desemba 2020.
Kwa upande wake, Briana, yeye alipelekwa Mtwara Novemba 2021, huyo utambulisho wake ulikuwa wa aina yake, kwani Briana alipandishwa jukwaani kwenye show ya Ibraah wa Konde Music na kuvishwa khanga na mama mzazi wa Harmonize lakini kufika Machi 2022 wakaachana.
Kwa muktadha huo ni kwamba endapo Harmonize atampeleka Kajala nyumbani kwao Mtwara bado kuna shughuli ipo, bado ana kazi ya kubwa ya kufanya mbele yake kuhakikisha anaendelea kushikilia moyo wa Konde Boy.


TATU; Harmonize amekuwa na utaratibu kwamba kila mwanamke anayeingia naye kwenye uhusiano na kudumu naye kwa muda fulani ni lazima atokee kwenye video za nyimbo zake, alifanya hivyo kwa Wolper na Sarah.

Machi 16, 2017

Harmonize aliachia video ya wimbo wake, Niambie ambayo ilifanyika Afrika Kusini, Wolper ndiye aliyetokea kama video vixen akiwa na uzoefu katika eneo hilo akifanya kazi na wasanii kama Mr. Blue, Quick Rocka, Ben Pol na wengineo.
Hata hivyo, siku kadhaa mbele, Wolper alisema kuwa ameachana na Harmonize miezi mitatu iliyopita kabla hata video hiyo haijatoka ila waliamua kufanya siri ili kulinda soko la muziki wao.  
Katika mapenzi yake na Sarah, Harmonize alihakikisha mrembo huyo anatokea kwenye video za nyimbo zake mbili kabla ya kuvunjika ndoa yao hapo Desemba 2020.
Walianza na video ya wimbo, Niteke iliyotoka Machi 26, 2019 ikifanyika visiwani Zanzibar, huu ni wimbo unaopatikana kwenye Extended Playlist (EP), Afro Bongo iliyotoka na nyimbo nne alizowashirikisha Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy.
Haikuishia hapo, Sarah alitokea tena kwenye video ya wimbo wa Harmonize, My Boo Remix ambao alishirikiana na Q Chief, hii ilitoka Julai 23, 2019 ikiwani kati ya nyimbo tatu zinazopatikana kwenye EP ya Q Chief, The Return of Chilla.
Kwa mtitiriko huo ni wazi kuwa Kajala lazima kuna siku ataonekana kwenye video ya Harmonize na pengine hasa video ya wimbo wake mpya, Deka ambao Kajala mwenyewe anaupenda.
Kina Diamond, Jux washafanya hii pia.