MASTORI YA OSCAR: Zama zinabadilika, lakini Kajala bado anatamba...

Monday June 13 2022
kajala pic
By Oscar Oscar

KAJALA Masanja ni mwigizaji na mrembo aliyedumu kwenye kiwanda cha burudani kwa muda mrefu. Ni zaidi ya miaka 20 sasa Kajala ameendelea kusumbua.

Haiji tu kwa bahati mbaya. Inahitaji kujitunza kwa kiwango cha hali ya juu. Siku hizi wanaibuka warembo kila kukicha kwenye Bongo movie, lakini bado Kajala hana mbadala. Ni miongoni mwa watu wachache ambao zama haziondoki kwao.

Alikuwepo zama za analojia. Sasa tuko naye kwenye dunia ya dijitali. Watu wengi wa kwenye burudani waliochelewa kugeuka kutoka analojia kwenda dijitali wamepoteza mvuto.

Tazama mastaa wetu wa muziki. Tazama mastaa wetu wa soka. Kama ulichelewa tu kugeuka na zama, haupo tena. Hakuna kiwanda kigumu kufanya kazi kama eneo la burudani. Burudani ni mahali ambapo kila siku vinazaliwa vitu vipya.

Ni mahali ambapo ubunifu wa hali ya juu unahitajika. Leo hii nchi nzima inamzungumza Kajala, ni kwa sababu tu bado hana mbadala kwenye ulimwengu wa burudani.

Dunia ya burudani inataka mtu anayejiongeza. Iko kasi sana. Hongera sana Kajala kwa kuweza kudumu kwa miaka mingi. Unamkumbuka mwaka ulioanza kumuona Kajala kwenye ulimwengu wa sanaa na burudani? Nikumbushe kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Advertisement

Pamoja na kukaa kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 20, bado Kajala anabandikwa picha zake kwenye mabango nchi nzima. Bado Kajala anapewa zawadi ya gari mbili - tena Range Rover. Watu wengi walioanza sanaa na Kajala wameshapotea.

Kwenye gemu yupo kwa zaidi ya miaka 20, lakini bado anaheshimu watu. Amekuwapo kwa miaka mingi, lakini bado ni mnyenyekevu kwa yeyote anayepita mbele yake.

Vijana wengi wa kizazi hiki hawana tabia hiyo. Jina likishakua wanajisahau. Jina likishakua wanaanza dharau. Maisha hayataki kiburi. Maisha yanawahitaji kina Kajala. Wanakuja mabinti wadogo kwenye sanaa, lakini wanaondoka na kumuacha Kajala.

Hongera sana Kajala kwa kudumu kwa miaka mingi kwenye ulimwengu wa sanaa na burudani. Heshimu sana watu wanaofanya sanaa kwa zaidi ya miaka 20. Kiwanda cha burudani, maisha yake mara nyingi ni miaka 10.

Kukaa juu kwenye sanaa na burudani kwa zaidi ya miaka 10 sio jambo rahisi. Hata wachezaji wa mpira baada ya miaka 10 ubora unaanza kupotea.

Ni wachache mno waliodumu zaidi ya miaka 10 kwenye ubora. Watu kama kina Cristiano Ronaldo ni wachache sana. Ukishafika juu, kukaa zaidi ya miaka 10 sio jambo dogo.

Tabia ya sanaa, michezo na burudani vinataka watu wapya karibu kila siku. Kila zama inakuletea watu wapya. Usishangae mtoto wa Kajala akaja kwenye gemu na kuondoka, mama akabaki.

Moja kati ya vitu vinavyomtofautisha kwa sasa Kajala na mastaa wengine wa burudani nchini ni kutopatikana kila kona. Huwezi kumuona kila mahali. Huwezi kumuona katika kila shughuli. Ataonekana kwenye maeneo machache. Anafanya mashabiki wake wawe na kiu ya kumuona. Anafanya watu wasimchoke kirahisi.

Mastaa wengi wanazurura sana mjini. Kila shughuli wapo. Kila baa wapo. Inapunguza kwa kiasi kikubwa thamani yao. Hakuna kitu kigumu kama kuwa staa nchini Tanzania. Bado sanaa yetu hailipi kihivyo.

Watu wengi wana majina makubwa kuliko vipato. Ukijifanya unataka maisha ya kupati kila siku hutoboi. Ukijifanya unataka kwenda na fasheni kila siku hutoboi. Lazima msanii awe mjanja wa kubalansi mambo. Kukaa juu kwenye sanaa na burudani kwa zaidi ya miaka 20 sio jambo dogo.

Vijana wengi baada ya kupata umaarufu kidogo, tayari wanawaza nyumba na magari. Kwa vijana wengi bado vitu hivi wanaona kama ni alama ya mafanikio.

Bado watu wengi wana dhana kuwa ukiwa na nyumba na gari, wewe maisha umeyapatia. Wanasahau kuwa hakuna kitu kigumu kukihudumia kama gari.

Kama bado hauna michongo inayoeweleka usianze maisha kwa kununua gari. Jifunze wakati mwingine kupata vitu kwa uwezo wako. Watu wengi kwenye sanaa wanaishi maisha ya watu. Ndiyo maana kina Kajala wanabaki wachache.

Ni vigumu sana kuishi maisha ya mashindamo. Ni vigumu sana kuishi maisha yasiyo ya uwezo wako. Wengi wameangukia pua. Wengi wamewaacha kina Kajala.

Ukimuona popote pale mtu anayefanya kazi ya sanaa, michezo au burudani kwa zaidi ya miaka 20 mpe heshima yake. Wengine unaweza kuwaweka kwenye bango hata miezi sita na watu wasiwe hata na habari nao. Wengine wanaweza kununuliwa hata mtaa mzima wa nyumba na watu wasiwe na habari nao.

Kuendelea kuzungumzwa kwa Kajala kunaonyesha namna ambavyo bado mrembo ana ushawishi mkubwa kwenye dunia ya burudani na sanaa. Hongera Kajala kwa kudumu kwa miaka mingi. Watoto wadogo na hasa kwenye sanaa na burudani wana cha kujifunza kutoka kwako.

Advertisement