Johari: Nilifanya mazoezi miaka mitatu bila kuonekana kwa TV

Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini, Blandina Chagula maarufu Johari, amesema wasanii wengi siku hizi hawana uvumilivu katika kufikia ndoto zao za kuwa wasanii wakubwa.

Johari ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 16, 2023 wakati wa uzinduzi wa tamthiliya mpya ya Lawama.

Johari amesema akiwa kama mmoja wa watu wanaomiliki kikundi ameshuhudia msanii akifanya mazoezi mwezi mmoja na kupotea na kutolea mfano yeye alifanya mazoezi miaka mitatu bila kuanza kuonekana kwenye runinga.

"Uvumilivu wangu ule nadhani leo ndio umenifikisha hapa hadi sasa nimekuwa prodyuza ninayezalisha wasanii wengine maarufu wakiwemo wakina Shamsa Ford," amesema Johari aliyeanza sanaa miaka 20 iliyopita na kutamba zaidi kwenye tamthiliya ya Johari.

Katika hatua nyingine, msanii huyo amewataka wasanii wa kike wasipende kubebwa bali kuonyeshwa njia ya kuvuka

"Baadhi ya wasanii wa kike wemekuwa wakiishia njiani kwa kuwa wanapenda zaidi kubebwa kuliko kujibiidisha wenyewe na kuomba kuonyeshwa njia walizopita waliofanikiwa.

"Hivyo kama unapenda kubebwa, badala ya kuonyeshwa njia ni wazi kuwa hautafika mbali, wasanii wa kike naomba mbadilike katika hili," amesema Johari anayemiliki kampuni ya kutengeza filamu ya Empire Likoma.

Akizungumzia kuhusu tamthiliya ya lawama, amesema inaonyesha maisha halisi ambayo watu wanaishi mtaani ikijikita kwenye mgogoro juu ya mume kupewa kulea mimba isiyokuwa yake huku lengo la mwanamke ikiwa kujipatia mali kwa mumewe.

Kwa upande wake Sofia Mgaza ambaye Msimamizi Mkuu wa chaneli ya Sinema Zetu, amesema tamthiliya hiyo ni mwendelezo wa kituo hicho kuwapa burudani watazamaji wao lakini pia kufungua fursa kwa maprodyuza na wasanii wa filamu.

Msanii Jacob Steve 'JB' amesema anamjua Johari ni mtu asiyekata tamaa na kutaka wasanii wasikubali kukatishwa tamaa licha ya changamoto watakazokutana nazo.