Je, Pique kumuumiza Shakira kama mtoto wa Rais?

Summary

  • Wiki hii mwimbaji Shakira amechukizwa na kitendo cha mzazi mwenziye, Gerard Pique kuonyesha wazi mahusiano yake mapya na mrembo, Clara Chia mwenye umri wa miaka 23, ikiwa ni kinyume cha makubaliano yao.

Wiki hii mwimbaji Shakira amechukizwa na kitendo cha mzazi mwenziye, Gerard Pique kuonyesha wazi mahusiano yake mapya na mrembo, Clara Chia mwenye umri wa miaka 23, ikiwa ni kinyume cha makubaliano yao.

Shakira na Pique, walioachana Juni mwaka huu kufuatia ukosefu wa uaminifu ndani ya penzi lao, walikubaliana kila mmoja endapo ataingia kwenye mahusiano mapya asiyaweke wazi hadi mwaka huu uishe.

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2010 huko Madrid, Hispania wakati wakitayarisha video ya wimbo maalumu wa Kombe la Dunia lililofanyika Afrika Kusini, ‘Waka Waka’ (This Time for Africa), na Machi 2011 Shakira alitangaza rasmi wao ni wapenzi.

Mwaka 2010 wakati wanakutana Pique tayari alikuwa mchezaji wa FC Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania iliyoshinda Kombe la Dunia mwaka huo Afrika Kusini, michuano ambayo Shakira alitumbuiza katika ufunguzi wake. Jarida la Forbes liliwahi kuwataja katika orodha ya wapenzi wenye nguvu duniani.

Katika miaka 12 ya kuwa pamoja walijaliwa watoto wawili, Milan (2013) na Sasha (2015) na hawakufunga ndoa kwa sababu Shakira alikuwa anahofia ndoa kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya na 60 Minutes mwaka 2014.

“Niwe muwazi ndoa inanitisha sana, sihitaji anione kama mke, nataka anione kama mpenzi wake,” alisema Shakira, ambaye amemzidi Pique miaka 10 ya kuzaliwa.

Kwa mujibu gazeti la The Sun, Pique alianza kuwa na mahusiano ya siri na Clara Chia kabla hata ya kuachana na Shakira. Chia ambaye ni mwanafunzi wa PR anatumia mahusiano hayo kumrusha roho Shakira kupitia mitandao ya kijamii.

Hivi karibuni Chia alichapisha video Instagram kwa mbali ukisikika wimbo, ‘Te Felicito’ wake Rauw Alejandro na Shakira, ingawa chapisho hilo lilifutwa muda mfupi, watu wa karibu wanasema Shakira alichukia na wa kulaumiwa ni Pique kwa kuruhusu hilo.

Bingwa huyo wa LaLiga kwa mara ya nane sasa moyo wake umetulia kwa Chia, ambaye amemzidi miaka 12 ya kuzaliwa, huku akimuajiri katika ofisi yake ambayo inahusika na michezo.

Pique na Shakira kufuatia kuachana kwao, inaripotiwa watalazimika kugawana mali walizochuma pamoja ambapo ni utajiri wa Pauni 300 milioni, ndege binafsi yenye thamani ya Pauni 15 milioni na jumba la kifahari lenye thamani ya Pauni 6 milioni, huku Pique akitaka kukaa na watoto Hispania, lakini Shakira anataka aishi nao Miami, Marekani.

Shakira na mtoto wa Rais

Kabla ya Gerard Pique, Shakira alikuwa na mahusiano na wakili kutoka Argentina, Antonio de la Rua tangu mwaka 2000 hadi Januari 2011 walipoachana rasmi.

Antonio de la Rua ni mtoto wa Rais wa zamani wa Argentina, Fernando de la Rua ambaye aliongoza nchi hiyo kutoka mwaka 1999 hadi 2001, na alikuwa mshauri wa baba yake kipindi cha urais. Mama yake anaitwa Ines Pertine.

Baada ya miaka 10 pamoja, Shakira na Antonio walitengana hapo Agosti 2010 katika kile walichoeleza ni uamuzi wa pande zote mbili, lakini Antonio ataendelea kusimamia biashara na masilahi ya kazi za sanaa za Shakira kama ambavyo amekuwa akifanya.

Mkali huyo wa ‘Hips Don’t Lie’, kupitia tovuti yake Januari 10, 2011 alitangaza rasmi kuachana kwao na Antonio na kile walichokubaliana kwa pamoja.

“Tangu Agosti 2010 tumekubaliana kuwa mbali na mahusiano yetu ya kimapenzi, katika wakati wote tumeendelea kufanya kazi pamoja, tumebakia kuwa karibu na kuweka faragha masuala yote,” alisema Shakira.

Hata hivyo, Septemba 2012, Antonio alimshtaki Shakira kwa kudai fidia ya Dola 100 milioni, wastani wa Sh233.1 bilioni kwa kile alichodai alichangia sehemu kubwa ya mafanikio ya mwimbaji huyo. Lakini Agosti 2013 Mahakama ya juu huko Los Angeles alitupilia mbali kesi hiyo.

Miongoni mwa dili ambazo Antonio alikuwa anadai kuzileta kwa Shakira ni kampuni ya matamasha, Live Nation yenye thamani ya Dola 300 milioni kwa kipindi cha miaka 10. Lakini kwa wakati wote Shakira alisema alifanya kazi na Antonio kama mshauri wake wa kibiashara na alilipwa kwa kazi hiyo.

Kitendo cha Pique kukiuka makubaliano yake na Shakira mapema, kinatia hofu moyo wa mrembo huyo na pengine kumkumbusha changamoto aliyopitia baada ya kuachana na Antonio kwa makubaliano mazuri, lakini baadaye mambo yakawa ndivyo sivyo!.

Shakira ni nani?

Mwimbaji wa Colombia, alizaliwa Februari 2, 1977, Barranquilla na kupewa jina la Isabel Mebarak Ripoll, anajulikana kama malkia wa muziki wa kilatini, alianza kufanya kazi na Sony Music Colombia akiwa na umri wa miaka 13.