Jay Z, Beyonce hiyo miaka 17 kama jana

Muktasari:
- Uhusiano wao ulianza mwishoni mwa miaka 1990 ila walipotoa kolabo yao wa kwanza, 03 Bonnie & Clyde (2002) iliyosampo wimbo wa 2Pac, Me and My Girlfriend (1996), ndipo tetesi za kuwa pamoja zilishika kasi ingawa walikanusha wakati huo.
Imetimia miaka 17 tangu Jay Z, 55, na Beyonce Knowles, 43, kufunga ndoa Aprili 4, 2008, hadi sasa harusi yao ni moja ya mambo yanayojadiliwa sana kutoka katika familia hiyo ya The Carters kutokana na jinsi walivyotekeleza jambo hilo.
Uhusiano wao ulianza mwishoni mwa miaka 1990 ila walipotoa kolabo yao wa kwanza, 03 Bonnie & Clyde (2002) iliyosampo wimbo wa 2Pac, Me and My Girlfriend (1996), ndipo tetesi za kuwa pamoja zilishika kasi ingawa walikanusha wakati huo.
Beyonce ambaye awali alivuma na kundi la Destiny’s Child, alisema alikutana na Jay Z akiwa na umri wa miaka 18 na mwaka mmoja baadaye wakaanzisha uhusiano ila kuhusu ni wapi walipokutana kwa mara ya kwanza imebaki kuwa siri yao.
Mnamo Novemba 2006 Beyonce, mshindi wa Grammy 35 akiongea na Jarida la Cosmopolitan alisema katika maisha yake hajawahi kujiona kama Bibi harusi ingawa aliwahi kufikiri kuhusu aina ya harusi anayoitaka ambayo sio kubwa.

Ndivyo ilivyokuwa, harusi yao waliifanya kwa faragha huku ikiwa na wageni takribani 40, miongoni mastaa walioalikwa ni wasanii wa Destiny’s Child, Kelly Rowland na Michelle Williams, pamoja na marafiki zao, Gwyneth Paltrow na Chris Martin.
Pia walijumuika na wanafamilia kadhaa wakiwemo wazazi wa Beyonce, Matthew na Tina pamoja na mdogo wake Solange, vilevile mama yake Jay Z, Gloria Carter, bibi, dada na mpwa wake walihudhuria.
Kulikuwa na mavazi ambayo wageni walipaswa kuvaa, wanawake walivalia nguo nyeupe huku wanaume wakivaa nyeusi. Kubwa zaidi simu zote za wageni zilikusanywa kabla ya shughuli kuanza ili kuhakikisha hakuna anayepiga picha wala kuchukua video.

Tarehe yao ya kufunga ndoa, yaani Aprili 4 ilikuwa na maana kubwa kwao na muhimu kwa sababu wana uhusiano wa karibu na namba 4, uhusiano huo unakuja kwa maana Beyonce alizaliwa Septemba 4 huku Jay Z ikiwa ni Desemba 4.
Kutokana na hilo, badala ya kuvishana pete, wote wawili walichora tattoo yenye alama ya nne (4:4) katika vidole vyao vya pete lengo likiwa ni kuonyesha kuheshimu namba hiyo ambayo wanaitaja kama ya bahati katika maisha yao.
Ilifuatia harusi ya kifahari iliyofanyika nyumbani kwa Jay Z jijini New York katika kitongoji cha TriBeCa, huku DJ Cassidy akialikwa kupiga muziki maana alikuwa na ukaribu na familia hiyo kwa muda mrefu.
DJ Cassidy akiongea na podikasti ya Drink Champs hapo Juni 2024 alisema alikuwa amepiga muziki katika hafla nyingi za mastaa hao ikiwemo uzinduzi wa klabu za usiku za Jay Z, 40/40 huko Atlantic na Las Vegas ila mwaliko wa harusi hiyo ilikuwa wa kipekee.

Alisema Beyonce na Jay Z hawakutumbuiza kabisa katika usiku huo mkubwa, hivyo alikuwa na jukumu la kupiga muziki kwa kipindi chote cha harusi hiyo ambayo ilimalizika saa 11 alfajiri.
“Ilikuwa ni mimi tu kupiga muziki kuanzia mwanzo hadi mwisho, sidhani kama kulikuwa na mazungumzo yoyote kuwa nicheze nyimbo gani kwa sababu nimekuwa nikifanya nao hivi kwa miaka mingi, hivyo walijua ni kitu gani anaweza kufanya,” alisema DJ Cassidy.
Hata hivyo, chanzo kimoja cha ndani kiliuambia mtandao wa People wakati huo kuwa orodha ya muziki ilijumuisha Hop Hip pamoja na aina nyingine za muziki wa zamani kutoka kwa wasanii kama The Jackson 5 na Whitney Houston.
Mwaka 2011 ndipo Beyonce alifichua picha ya kwanza ya vazi lake la harusi katika video ya Live at Roseland, kisha miaka mitatu baadaye, Jay Z alionyesha video fupi katika ziara yao ya pamoja ya dunia, On The Run.
Wakati Jay Z na Beyonce wakibadilishana viapo vyao vya ndoa mbele ya wageni wao, walikuwa wenye hisia kali za furaha, machozi ya mbali na muunganiko wa kiroho kama inavyoonekana katika video ya wimbo wao, Die with You (2017).

Katika hafla ya tuzo za MTV VMAs 2011, wakati Beyonce akitumbuiza wimbo wake, Love On Top (2011) alitangaza kuwa ana ujauzito wa mtoto wao wa kwanza, na kufikia Januari 7, 2012 akajifungua mtoto wa kike ambaye alipewa jina la Blue Ivy Carter.
Juni 13, 2017 familia yao iliongezeka baada ya Beyonce kujifunga watoto pacha, Rumi na Sir Carter. Rumi ni wa kike na amekuwa akionekana na wazazi wake mara kwa mara katika mitoko yao ila huyo wa kiume, Sir huwa anafichwa sana mbele ya macho ya umma.
Ikumbukwe Jay Z na Beyonce alikataa kuhudhuria harusi ya Kanye West na Kim Kardashian iliyofanyika Mei 24, 2015 huko Florence, Italia kwa sababu hawakutaka kuonekana katika reality show ya Kim, Keeping Up With The Kardashians.
Harusi hii nayo ilikuwa ya faragaha zaidi, waalikwa hawakuruhusiwa kuingia na simu na baadaye mastaa hao walikataa ofa ya Dola 11 milioni kutoka kwa majarida makubwa ambayo walitaka picha zao kwa sababu za kibiashara. Hata hivyo, ndoa hii ilivunjika rasmi kwa talaka Novemba 2022.