Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasanii Bongo wanaigana hadi inaboa sasa!

Muktasari:

  • Katika nyimbo hizo mbili, wanamuziki wote wamechomekea maneno matatu ya lugha ya Kiingereza, nayo ni ‘Lord have mercy’ ila cha kushangaza huoni muunganiko wa moja kwa moja kati ya kile wanachoimba na maneno hayo.

HIVI karibuni nilikuwa nikisikiliza nyimbo mpya za Nandy, No Stress (2025) na Harmonize, Furaha (2025), nikagundua tatizo la wasanii wengi Bongo kuigana katika utunzi wa nyimbo na namna wanavyotoa albamu zao bado lipo sana tu.

Katika nyimbo hizo mbili, wanamuziki wote wamechomekea maneno matatu ya lugha ya Kiingereza, nayo ni ‘Lord have mercy’ ila cha kushangaza huoni muunganiko wa moja kwa moja kati ya kile wanachoimba na maneno hayo.

Hata hivyo, wanafanya hayo kutokana ni utamaduni wao kuigana, maneno hayo pia alishayatumia Diamond Platnumz katika wimbo wake, Hallelujah (2017) akiwashirikisha Morgan Heritage, kundi la muziki wa Reggae kutokea Jamaica. 

Wimbo huo ulijumuishwa katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018) chini ya Universal Music Group (UMG), huku lengo la jina la albamu hilo likiwa ni kujitambulisha yeye ni nani na kule anapotokea ni wapi.

Baada ya hapo zilifuata albamu kibao zenye majina yenye maana inayofanana na hiyo, mfano The Kid You Know (2022) yake Marioo, First Born (2022) ya Beka Flavour, Story Of The African Mob (2020) ya kwao Navy Kenzo, Sound From Africa (2021) ya Rayvanny n.k.

Darassa alipotoa albamu, Slave Becomes a King (2020), naye Alikiba akatoa Only One King (2021), Ibraah wa Konde Music akatoa The King of New School (2022), kisha Jux, King of Hearts (2022). Neno ‘King’ limezingatiwa hapo.

Mwasiti alipotoa EP, The Black Butterfly (2021), naye Anjella akatoa yake, The Black Queen (2024), hivyo EP zote zimeanza na maneno ‘The Black’ kama sehemu ya utambulisho wao kwa kile wanachojivunia kama wasanii wa kike.

Pia albamu na EP nyingi Bongo zimekuwa zikianza na neno ‘The’, ukiachana na nilizotaja mwanzo, kuna The African Princess (2018) ya Nandy, The Love Album (2019) ya Jux, The4Some (2020) ya Lulu Diva, The Father (2020) ya Country Wizzy.

Nyingine ni The Gift of Life (2021) ya Best Naso, The Capricorn (2021) ya Izzo Bizness, The Green Light (2022) ya Killy, The God Son (2024) ya Marioo, The Big One (2024) ya Rayvanny n.k.

Haya sasa twende bandika bandua, Weusi walipotoa albamu yao, Air Weusi (2021), Ibraah akaja na Air Piano (2024), Lady Jaydee alipotoa 20 (2021), Abigail Chams akaja na 5 (2023), Harmonize alipotoa High School (2021), Mabantu wakaja na University (2023).

Zuchu alipotoa EP yenye jina lake, I Am Zuchu (2020), Maua Sama naye akaja na yake, Sama (2024), Nandy alipotoa EP ya muziki wa Injili, Wanibariki (2021), naye Mimi Mars akaja na Christmas with Mimi Mars (2021) huku Linex akitoa, My Side B (2022).

Vilevile wanaiga hata vya nje, mfano staa wa Nigeria Wizkid alipotoa albamu zake mbili, Sounds From the Other Side (2017) na Made In Lagos (2020), ndipo Rayvanny akatoa Sound From Africa (2021), na Harmonize akatoa Made For Us (2022).

Cha kushangaza zaidi ni kwamba asilimia 99.9 ya albamu na EP zote nilizozitaja hapo juu, zina majina ya Kiingereza!, wasanii wengi wa Bongofleva wanaona sifa kutoa albamu zenye majina ya aina hiyo wakati nyimbo zote zilizopo ndani yake wameimba Kiswahili.

Hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo wasanii walitoa albamu zenye majina mazuri ya Kiswahili na zikabamba, mfano Juma Nature, Ugali (2003), Professor Jay, Machozi Jasho na Damu (2001), Stara Thomas, Nyuma Sitorudi (2000), TID, Sauti ya Dhahabu (2002).

Bila kumsahu Lady Jaydee, Binti (2003), Jay Moe, Ulimwengu Ndio Mama (2002), Ferooz, Safari (2005), Ray C, Mapenzi Yangu (2003), Bushoke, Barua (2003), Banana Zorro, Mama Yangu (2003), Daz Baba, Elimu Dunia (2004), Kalapina, Kufa Au Kupona (2005) n.k.

Ila leo hii ni msanii gani wa Bongo Fleva hasa hawa wenye majina makubwa anaweza kutoa albamu akaiita ‘Binti’ au ‘Ugali’?, wanataka majina ya Kiingereza kwa kile wanachodai albamu zao zinasikilizwa na watu wengi wa nje ambao hawajui Kiswahili.

Lakini hilo nalo linatuacha njia panda kwa sababu albamu inakuwa na jina la Kiingereza lakini nyimbo zote zimeimbwa kwa Kiswahili!, hata hizo zinazoimba kwa Kiingereza ni vimistari viwili vitatu tena vya kuokoteza.

Hoja hiyo haina mashiko kwa sababu ukitazama katika mitandao ya kusikiliza muziki kama Spotify, albamu za kina TID zina wasikilizaji wengi kuliko hata za baadhi ya wasanii wa sasa ambao wanaamini katika dhana hiyo.

Ukweli ni kwamba wasanii wetu walivutia na jinsi albamu za wenzao wa Nigeria zinavyotoka na majina ya Kiingereza na wao wakapita humo humo bila kujali kuwa wenzao wanatumia zaidi lugha hiyo katika muziki wao na hata kuwasiliana kila siku.

Ndio sababu utamaduni huu wa albamu za Bongofleva kuachiwa zikiwa na majina ya Kiingereza ulianza kushika kasi kipindi kina Davido, Wizkid, Tiwa Savage na Burna Boy muziki wao unaanza kushika kasi Afrika Mashariki katikati mwa miaka ya 2010.