Harmonize kaondoka na deni kubwa WCB Wasafi

Muktasari:
- Hoja inayotolewa ni video za nyimbo hizo ndizo hadi sasa zimetazamwa zaidi (most viewed) YouTube, hivyo katika miaka yake mitano nje ya WCB Wasafi ameshindwa kutoa video ilizofanya vizuri kama hizo.
Tangu kuondoka WCB Wasafi na kuanzisha lebo yake Konde Music, Harmonize amekuwa akinyooshewa vidole na wakosoaji wake ameshindwa kutengeneza nyimbo kubwa kama Kwangwaru, Happy Birthday, Bado na Aiyola.
Hoja inayotolewa ni video za nyimbo hizo ndizo hadi sasa zimetazamwa zaidi (most viewed) YouTube, hivyo katika miaka yake mitano nje ya WCB Wasafi ameshindwa kutoa video ilizofanya vizuri kama hizo.
Utakumbuka video ya wimbo ‘Kwangwaru’ iliyotoka Aprili 14, 2018 akimshirikisha Diamond Platnumz, ndiyo iliyotazamwa zaidi YouTube upande wa Harmonize ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 119.

Baada ya Kwagwaru video za nyimbo zake zilizofanya vizuri ni Happy Birthday (2017) yenye ‘views ‘milioni 51, kisha inafuatia Bado (2016) milioni 41 na Aiyola (2015) milioni 34, ukiwa wimbo ni wake wa kwanza chini ya WCB Wasafi.
Hili ni deni ambalo Harmonize kaondoka nalo WCB Wasafi, mwaka wa tano sasa hajaweza kulilipa, ili lilipa anatakiwa kuja na wimbo utakaopata namba kubwa kuzidi Kwangwaru, Happy Birthday, Bado na Aiyola.
Akiwa na lebo yake, Konde Music, video ya Harmonize yenye mafanikio makubwa YouTube ni ya wimbo, Single Again (2023), hii imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 34 na ndiyo wimbo wake uliopata namba kubwa hata katika mitandao mingine.
Ikumbukwe wakati anaondoka WCB Wasafi, Harmonize alikuwa ni msanii wa pili Tanzania kuwa na wafuasi (subscribers) na ‘views’ nyingi YouTube baada ya Diamond ila sasa ameshuka hadi nafasi ya tatu upande baada ya kupitwa na Rayvanny.

Kutokana na kuporomoka huko, kuna kipindi kulikuwa na madai Harmonize amekuwa akitumia njia mbalimbali za mkato ili kuhakikisha video zake zinapata views za kutosha YouTube.
Mathalani, video ya wimbo wake, Mdomo iliyotoka Aprili 12, 2022 akimshirikisha Ibraah, iliweza kupata ‘views’ zaidi ya milioni 1 ndani ya sekude 21 tu na kuibua mjadala mkali ni kitu ambacho hakiwezekani!.
Ila mashabiki wake walijitapa kuwa Harmonize amevunja rekodi ya video ya wimbo wa Diamond ‘Waah!’ akimshirikisha Koffi Olomide kutoka DR Congo iliyofikisha ‘views’ milioni 1 ndani ya saa nane pekee.
Wengine walienda mbali na kudai video hiyo (Mdomo) mafanikio yake ni sawa na ile ya bendi kutoka Korea Kusini, BTS ambayo video ya wimbo wao, Butter uliyotoka Mei 2021 ilipata ‘views’ milioni 108.2 ndani ya saa 24.
Hata hivyo, licha ya video za Harmonize kupata ‘views’ milioni 1 kwa muda mfupi hata chini dakika moja, zimekuwa na mwendelezo usio wa kuridhisha na ndipo yanaibuka madai alinunua namba hizo.
Kwa mfano, video ya msanii wa lebo yake, Ibraah, Rara ambayo ilitoka wiki moja kabla ya ‘Mdomo’ ilipata ‘views’ zaidi 600,000 ndani ya dakika tatu lakini ikachukua siku nne kufikisha ‘views’ milioni 1 YouTube jambo ambalo nalo lilibua mjadala.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wanaomini kuwa mwimbaji huyo amekuwa akifanyiwa mchezo mchafu ili kumrudisha nyuma kufuatia mfululizo wa visa wa video za nyimbo zake na za waliokuwa wasanii wake kuondolewa YouTube kila wakati.
Januari 2020 video ya wimbo wa Killy ‘Ni Wewe’ ambao amemshirikisha Harmoninze iliondolewa YouTube kutokana na malalamiko ya hakimiliki (copyrighty claims) kutoka mtu anayetambulika kwa jina la Mutisya Munyithya wa Kenya.

Hiyo ni baada ya Juni 2021 wimbo wa Harmonize ‘Sandakalawe’ nao kuondolewa YouTube kutokana na masuala ya hakimiliki baada ya kampuni ya usambazaji muziki ‘Empire’ kulalamika wimbo huo umechukua baadhi ya maudhui yao.
Kabla ya hapo, Agosti 2020 wimbo wa Harmonize ‘Ameen’ uliondolewa YouTube baada ya msanii mwenziye, Rosa Ree kulalamika ulitumia mdundo wa wimbo wake ‘Kanyor Aleng’ bila idhini yake.
Huo ulikuwa ni wimbo wa pili kwa Harmonize kuondolewa YouTube kutokana na mdundo wake kusikika kunakiliwa kutoka kwenye wimbo mwingine. Wa kwanza ni wimbo wake ‘Uno’ ambao Prodyuza wa Kenya, Magix Enga alipeleka malalamiko yake YouTube na video hiyo kuondolewa ila kwa sasa imerejeshwa.