Harmonize apita njia za Burna Boy

Muktasari:
- Mwimbaji wa Bongofleva kutokea Konde Music Worldwide, Harmonize anapita njia za Burna Boy baada ya kuachia albamu yake ya tatu, ‘Made For Us’ yenye nyimbo 18, ikiwa ni albamu yake ya pili ndani ya mwaka mmoja.
Mwimbaji wa Bongofleva kutokea Konde Music Worldwide, Harmonize anapita njia za Burna Boy baada ya kuachia albamu yake ya tatu, ‘Made For Us’ yenye nyimbo 18, ikiwa ni albamu yake ya pili ndani ya mwaka mmoja.
Utakumbuka Novemba 2021 Harmonize alitoa albamu yake ya pili ‘High School’ yenye ngoma 20 na kuwashirikisha wasanii sita, wakiwamo Sarkodie, Busiswa na Naira Marley.
Albamu ya kwanza ‘Afro East’ ilitoka Machi 2020, ikiwa na ngoma 18 alizowashirikisha wasanii wengi wa nje wakiwamo Burna Boy, Mr Morgan Heritage, Khaligraph Jones, Phyno, Skales, Mr Eazi, Falz na Yemi Alade.
Harmonize anakuwa msanii wa kwanza Bongo kutoa albamu miaka mitatu mfululizo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ingawa mtindo huo umekuwa ukikosolewa kwa madai ya kutozipa nafasi ngoma zake kufanya vizuri na hata nafasi ya promosheni inakuwa ni ndogo ila yeye anapita mulemule kwa Burna Boy.
Msanii Burna Boy wa Nigeria naye amekuwa na mtindo wa kuachia albamu mara kwa mara miaka ya hivi karibuni, albamu yake ya kwanza, ‘L.I.F.E’ ilitoka Agosti 2013 ya pili ‘On a Spaceship’ ilitoka Novemba 2015.
Mwaka 2017 baada ya kusainiwa na Bad Habit/Atlantic Records ya Marekani na Warner Music Group, Burna Boy aliachia albamu ya tatu ‘Outside’ iliyotoka Januari 2018, ilifanya vizuri hadi kushika nafasi ya tatu kwenye chati za Billboard Reggae.
Julai 2019 aliachia albamu ya nne aliyoiita ‘African Giant’, ambayo ilishinda tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka kutoka All Africa Music Awards (AFRIMA) na ilichaguliwa kuwania tuzo za Grammy.
Kufika Agosti 2020 akatoa albamu ya tano, ‘Twice As Tall’, iliyochaguliwa kuwania Grammy na kushinda kipengele cha Albamu Bora ya Muziki Duniani (Best World Music Album), huku akiweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Nigeria kuchaguliwa kuwania tuzo hizo mfululizo.
Sasa anafanya vizuri na albamu yake ya sita ‘Love Damini’ iliyotoka Julai 2022 ikiwa na ngoma kali kama ‘Last Last’ iliyofanya vizuri kwenye chati za Billboard Marekani, Uholanzi, Uingereza na Ufaransa.
Hivyo kwa miaka mitatu mfululizo (2018 -2020) Burna Boy alitoa albamu tatu kama alivyofanya Harmonize, lakini za kwake zimeshinda tuzo za Afrima, kuchaguliwa Grammy na kushinda Grammy.
Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 albamu ya Harmonize, ‘High School’ ilichaguliwa kuwania kipengele cha Albamu Bora ya Mwaka, lakini ushindi ilienda kwa Alikiba kupitia albamu yake ‘Only One King’.
Hata hivyo, kwa kulinganisha mtindo wa Burna Boy na kile kinachoonekana ni Harmonize kufuata nyayo, bado mwimbaji huyo wa Konde Music yupo eneo sahihi kwa sababu Burna Boy ameanza kupata mafanikio ya tuzo baada ya kutoa albamu ya nne, tena baada ya kuwa chini ya Bad Habit/Atlantic Records na Warner Music Group.