Harmonize aja ‘Muziki wa Samia’

Muktasari:
- Katika nyimbo zake na video msanii huyo ameonyesha maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii nchini ili kuhamisasha wageni kuitembelea Tanzania.
MWANAMUZIKI wa Bongo flava, Rajab Abdul maarufu Harmonize, Mei 25, mwaka huu anatarajia kuzindua albumu ya tano aliyoipa jina la ‘Muziki wa Samia’ katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo, Harmonize amesema lengo ni kupongeza na kusupoti harakati za Rais Samia na ametengezeneza nyimbo 10 ambazo zote zinamlenga Rais na baada ya albumu hiyo atahitaji kupumzika huku akiwa anaachia wimbo mmoja mmoja.
Albamu nne za Harmonize zilizopita zilikuwa na ladha tofauti ambazo ni Afro East (2020) yenye maudhui ya maisha yake, muziki (burudani) na mahusiano ya mapenzi.
Kwenye ladha amechanganya kutoka miziki mbalimbali ikiwamo singeli, amapiano huku akitumia lugha tofauti ikiwamo Kiingereza.
Kwenye High Scholl ya 2021 kulikuwa na ladha iliyobeba maudhui au ujumbe wa burudani zaidi na huko ametumia amapiano zaidi na ilifanya vizuri kabla ya kuachia nyingine ya 'Made for Us' mwaka 20222.
Ndani ya 'Made For Us' inakimbiza na maudhui mchanganyiko pamoja na ladha mbalimbali za muziki na ya nne ni Visit Bongo 2023 iliyobeba maudhui yanayoitangaza nchi na hasa utalii.
Katika nyimbo zake na video msanii huyo ameonyesha maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii nchini ili kuhamisasha wageni kuitembelea Tanzania.
Kwa sasa Harmonize anakuja na albamu hiyo inayolenga kupongeza Rais Samia na kuunga mkono kazi nzuri inayoendelea kufanywa na kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Hii inaleta ladha nyingine tofauti katika albamu za mkali huyo aliyewahi kutamba na wimbo ‘Amelowa’ na nyingine nyingi zilizomtangaza nchini na kimataifa.
Na katika kusisitiza Harmonize anasema: "Tunatambua makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na Rais Samia Suluhu na tumeweka kumbukumbu zote katika kitabu kitakachoishi milele na kukipa jina la 'Muziki wa Samia'.
"Nitaitumia siku hiyo kuzindua albumu yangu hiyo ya tano iliyobeba tafsiri ya matendo ya uongozi ya Rais."
Harmonize ameeleza kuwa hakuna atakachoimba zaidi ya kile ambacho kipo kwenye albumu hiyo, akisema humo ameweka hisia zote za uimbaji na uwezo wake na hiyo ndio albuma yake ya mwisho.