Hao tena! vita ya Zari na Diamond haiishi

BADO kuna safari ndefu kumalizika kwa vita kati ya Zari Tha Bosslady na warembo wanaokuwa na uhusiano na aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenziye, Diamond Platnumz licha ya kuwa kila mmoja sasa ana maisha yake tangu kuachana kwao Februari 2018.

Zari na Diamond ambao wamejaliwa watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016) wamekuwa na matukio ya kuumiza na hata kurushana roho katika mitandao kwa muda mrefu, hilo linatoa picha kuwa vita yao haiwezi kuisha leo wala kesho!.

Baada ya Wema Sepetu, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna, sasa Zari ana vita na Fantana kutokea nchini Ghana ambaye anahusishwa kuwa na uhusiano na Diamond baada ya kuonekana wakijiachia katika reality show inayoruka Netflix, Young, Famous & African.

Katika mchezo huo ambao ni msimu wake wa pili, Diamond anaonekana kuvurugwa haswa na uzuri wa Fantana hadi kufikia hatua ya kuibua madai kuwa Zari alikuwa anataka kuzaa naye mtoto mwingine!.

"Zari alitaka mtoto mwingine na mimi, alitaka kupata mtu wa kumzalia mtoto," alisema Diamond ambaye ni Baba watano kutoka kwa wanawake watatu tofauti, Zari, Hamisa na Tanasha.

Kauli hiyo imeibua vita kati ya Diamond, Zari na Fantana, na sasa Zari na Fantana hawachaguliana tena maneno ya kupeana mtandaoni, kila mmoja anapiga pale anapohisi patamuumiza mwenzake zaidi.

Zari anadai Fantana ni mwanamke wa barabarani aliyemchanganya tu Diamond, huku Fantana akidai Zari amefanya upasuaji (plastic surgery) wa kuboresha muonekano wake kwa mara tano ili aweze kufanana naye!.

Ikumbukwe Fantana (Francine Koffe) ni mwanamuziki wa Ghana, alizaliwa Julai 3, 1997 na kukulia huko Atlanta, Georgia nchini Marekani ambapo alisomea biashara na mitindo. Juni 2019 alitoa wimbo wake wa kwanza 'So What' uliotayarishwa na Mog Beatz na tangu wakati huo amekuwa akifanya vizuri.

Kwa mujibu wa Zari, wakati anaanza uhusiano na Diamond mwaka 2014, Staa huyo wa WCB Wasafi alikuwa hajulikana hata Afrika Mashariki, Zari anadai yeye ndiye alimfanya Diamond kutambulika kwa sababu alikuwa tayari maarufu na tajiri.

Hata hivyo, kauli ya Zari inaacha maswali ikiwa ni kweli mwaka 2014 Diamond alikuwa hajulikani Afrika Mashariki au ndio vita haichaguli slaa!.  Mwaka 2014 ambapo Diamond alikuwa na Wema, alikuwa ameshatoa kolabo na Davido wa Nigeria iliyofanya vizuri sehemu kubwa ya Afrika.

Jina lake lilikuwa limeanza kuvuma Afrika, Juni 2014 Diamond alitumbuiza hafla ya utoaji wa tuzo za MTV MAMA iliyofanyika Durban Afrika Kusini, sio kutumbuiza tu, bali alikuwa anawania vipengele viwili, Msanii Bora wa Kiume na Wimbo Bora wa Kushirikiana (My Number Remix) ft. Davido.

Utakumbuka baada ya wawili hao kuchana, Diamond alianzisha uhusiano na Tanasha Donna kutokea Kenya, huku Zari akitambulisha wanaume wawili, 'King Bae' na 'The Dark Stallion', na sasa ameolewa na Shakib Chams, kijana wa nyumbani kwao Uganda.

Ila hilo halijaleta utuvulivu kati yao, miaka zaidi ya mitano tangu kutengana kwao bado chokochoko haziishi, Diamond akiwa na Tanasha alidai Zari alimsaliti kwa Peter (Mr. P) wa kundi la P Square, Zari naye sasa anadai Diamond anatafuta njia ya kurudiana naye!.

Kipindi penzi la Tanasha na Diamond limeanza kupamba moto, Tanasha aliandika Instagram; "Ndugu wenye chuki nina mengi sana kwenu ya kufanya mchukie, endeleeni kuwa wavumilivu."

Kwa haraka wengi walihisi ujumbe wa Tanasha ameutuma kwa Zari na ndipo akaulizwa iwapo anamfahamu, Tanasha alijibu hamfahamu na kutaka watu waache kuchochea vita visivyo na maana.

"Hapana simjui, lakini nadhani ni Mama wa watoto wawili, najua ni Mama mrembo anayefanya kazi na anajituma sana na watu inabidi waache kufananisha na kuchochea drama ambazo hazina maana na badala yake wawape wanawake nguvu," alijibu Tanasha.

Hata hivyo, Zari aliibuka na kumsikitikia Tanasha kupewa ujauzito na Baba (Diamond) wa watoto watatu asiyewajibika, hiyo ilikuwa Juni 2019 Zari akiwa Kenya kwa mwaliko wa Akothee.

"Kuna mtu anasema Tanasha ni mjamzito, commets zinakuja kila mara, ni vizuri kuwa mjamzito, ni kitu kizuri, lakini ni kitu kingine akiwa ni wa Baba wa watoto watatu asiyewajibika, kwa hiyo inanifanya nihoji vipaumbele vyake," alisema Zari na kuongeza.

"Kwa hiyo hongera nina matumaini (Tanasha) una fedha ya kutosha Benki kwa ajili ya kumtunza mtoto huyu kwa sababu (Diamond) yupo hivyo alivyo," alisema Zari akizungumza Insta Live.

Wakati imeripotiwa kuachana kwa Tanasha na Diamond hapo Machi 2020, Zari hakukaa kimya, aliibuka na kusema; Haijalishi ni mara ngapi nyoka anajivua gamba lake, ataendelea kuwa nyoka pia!. 

Na sasa ni zamu ya Zari na Fantana, huku Diamond akiwekwa mtu kati, huu ni mwendelezo tu miaka yote, hakuna mwanamke ambaye amewahi kuwa na uhusiano na Diamond ambaye Zari hakuwahi kumzungumzia au kuzozana naye mtandaoni. Alianza na Wema Sepetu, kisha Hamisa Mobetto, hawa wote Zari aliwashiana nao moto vilivyo!.