Hamisi Maya abadilishiwa mpinzani

Sunday January 03 2021
bondia pic
By Imani Makongoro

BONDIA Mtanzania, Hamisi Maya amebadilishiwa mpinzani, sasa atazichapa na Alvin Omondi wa Kenya.

Awali Maya ilikuwa azichape na Ahmed Alhady wa Misri Februari 14 jijini Dar es Salaam pambano la raundi nane lisilo la ubingwa.

Mbali na kubadilishiwa mpinzani, pambano hilo limesogezwa hadi April 2 mwaka huu ambapo litapigwa kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba.

Kama ilivyokuwa kwa mpinzani wa awali, kwa Omondi pia Maya anapaswa kuhakikisha anashinda ili kuendelea kulinda rekodi yake.

Endapo atapigwa, itakuwa ni faida kwa Mondi ambaye tangu Desemba 26, 2018 alipochapwa kwa TKO nchini Uganda na Charles Mulindwa hajawahi kurudi ulingoni.

Omondi mwenye rekodi ya kucheza mapambano manne na kushinda matatu, endapo atashinda, ataongeza pointi na itakuwa ni fursa kwake kupata nyota kwenye ubora wa ngumi kulinganisha na Maya bondia wa nyota mbili.

Advertisement

Maya atapanda ulingoni akibebwa na uzoefu wa mapambano 13 aliyowahi kucheza kulinganisha na mpinzani wake.

Mratibu wa pambano hilo Chaurembo Palasa amesema pambano hilo ni mahususi kwa Maya kurudi upya kwenye ngumi baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.

Amesema pambano hilo litafanyika chini ya Super D Boxing Promotion na mashabiki wa Maya watamshuhudia bondia wao katika ubora wa hali ya juu, baada ya kutoonekana ulingoni tangu 2019.

Amesema sababu za kumbadilishia mpinzani Maya ni umbali wa nchi ya Misri anakotoka Alhady kulinganisha na Omondi kutoka Kenya.

Amesema, Maya na Omondi watasindikizwa na mabondia wengine 10 watakaozichapa siku hiyo.

Vicent Mbilinyi atazipiga na George Onyango na Fransic Miyeyusho atacheza na Gabriel Chola wakati Hamidu Kwata atazipiga na James Kibazange, Juma Abdul ataonyeshana ubabe na Hamza Mchanjo huku Bakari Magona akitoana jasho na Emmanuel Mwakyembe.

Hamisi Maya aliyewahi kutwaa ubingwa wa GBC, ana historia ya kumchapa kwa KO, James Onyango wa Kenya aliyekuwa nyumbani na kutwaa ubingwa wa Afrika.

Advertisement