Februari Ulikuwa mwezi wa mahaba, skendo na kazi

Sunday February 28 2021
february pic
By Kelvin Kagambo

TUNAIMALIZIA Februari leo; mwezi ambao mandhari yake ilikuwa ni mapenzi na mahaba. Mwezi ambao kwa mujibu wa kalenda ya Gregori ndiyo mwezi mfupi zaidi ukiwa na siku 28 tu ndani ya mwaka huu. Yaani wale wote waliozaliwa Februari 29, mwaka huu hawana chao mjue!

Lakini, licha ya ufupi wake mambo kibao yametokea ndani ya mwezi huu kwenye upande wa burudani kiasi kwamba ilikuwa ni rahisi sana mfuatiliaji kupotea njiani na huenda hata wewe ulipitwa kwenye baadhi ya matukio.

Ngoma mpya zimeachiwa, albamu pia zilikuwepo, skendo, kiki na habari kubwa kubwa za burudani zilikuwa za kutosha jumlisha fujo katika Siku ya Wapendanao. Kwa kifupi, Februari ulikuwa na ujazo wa kutosha na leo tunamulikia kwa uchache matokeo yote makubwa ya burudani ya mwezi huu.


VALENTINE ILIKUWA PAMBE

Valentine ya mwaka huu ni ya kukumbukwa kwa sababu ilikuwa na sapraizi kibao kutoka kwa wasanii. Msanii wa muziki wa Bongofleva, Harmonize alichapisha kwa mara ya kwanza picha akiwa na mpenzi wake mpya muigizaji Kajala Masanja. Kabla ya kuposti picha hiyo Harmonize na Kajala walikuwa wanatajwa kuwa wanachangia kopa moja lakini mara zote walipinga.

Advertisement

Naye staa asiyeishiwa vituko, Gigy Money pia aliposti video akipigana mabusu na mpenzi wake mpya ambaye hakuwahi kumuonyesha huko nyuma. Na kabla ‘valentine day’ haijamalizika ambayo ilikuwa ni tarehe 14, aliyekuwa mpenzi wa Diamond Platnumz, Mganda Zari The Boss Lady aliposti sura ya mwanaume wake mpya ambaye kabla ya siku hiyo alikuwa akimposti kwa kumficha sura.


SKENDO NA STORI KUBWA

Skendo iliyotawala mwezi huu wa pili ilikuwa ni video inayomuonyesha msanii wa muziki kutoka WCB, Rayvanny akipigana mabusu ya kimahaba na mtoto wa muigizaji Kajala Masanja, binti anayefahamika kwa jina la Paula.

Video ambayo baadae ilisababisha joto mjini baada ya Kajala kumtuhumu mwanamitindo Hamisa Mobetto kuwa ndiye aliyempeleka binti yake kwa Rayvanny, wakamnywesha pombe na kumrekodi video zisizokuwa na maadili. Hata hivyo Hamisa alipinga tuhuma hizo.

Mwisho wa mchezo skendo hiyo ilimalizika kwa Hamisa na Rayvanny kuitwa kituo cha polisi na kuhojiwa. Hata hivyo, inadaiwa huenda pande mbili hizo ziliamua kumaliza suala zima kirafiki.

Lingine lililobamba kwenye mitandao ya kijamii kwa mwezi huu ni pamoja na lawama alizoshushiwa Harmonize kutoka kwa mzazi mwenzake, mrembo anayefahamika kwa jina la Shanteel kwamba alikuwa anazungumza na mtoto wao mdogo wa miaka mitatu kwenye maeneo ambayo hayaendani na umri wa mtoto. Sehemu kama vile kumbi za starehe na nje ya mji mbali na mama yake.

Shanteel alirusha tuhuma hizo kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo pia alimtaja Kajala kuwa chachu ya hayo kutokea kwani muda wote huo Harmonize alikuwa anazunguka na mpenzi wake huyo mpya wakiwa na mtoto.

Katikati ya mwezi wachumba wa muda mrefu, muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Mkurugenzi wa EFM na ETV, Francis Ciza ‘Majizo’ walizima kelele zote za mji kwa kufunga ndoa ambayo ilikata kelele za kejeli kwamba wawili hao walikuwa wachumba kwa muda mrefu wa takribani miaka miwili. Ndoa ya Lulu na Majizo ilifungwa tarehe 16 kwenye kanisa la St. Gasper jijini Dar es Salaam.


NGOMA KAMA ZOTE

Kwa upande wa burudani pia mwezi wa pili haukuwa mkavu, albamu tatu zimeachiwa sambamba na ngoma kibao kutoka kwa wasanii A List wa Bongofleva.

Rayvanny wa WCB aliachia albamu yake inayoitwa Sound from Africa iliyo na ngoma 23. Kisha akafuatiwa na mkongwe Lady Jaydee ambaye aliachia albamu yake iliyopewa jina la Ishirini ikiwa ni kama alama yake ya kutimiza miaka 20 kwenye muziki wa Bongofleva.

Na kabla ya mwezi kumaliza prodyuza wa muziki Sweetbert Mwinula A.K.A Abbah Process aliachia albamu yake inayoitwa Abbah The Evolution yenye ngoma 16 tarehe 27. Pia, Lavalava kutoka lebo ya Wasafi naye aliachia EP inayoitwa Promise yenye ngoma nne.

Kwa upande wa ngoma, nyimbo mpya zilizotoka mwezi wa pili na kuvuma ni pamoja na All Night ya Harmonize aliyomshirikisha msanii chipukizi Anjela. Pia wimbo wa Nandy aliomshirikisha Koffi Olomide unaoitwa Leo Leo ulikuwa kwenye orodha ya ngoma kubwa na kali za mwezi wa pili.

Aidha wimbo wa nyongeza wa msanii Rayvanny unaoitwa Valentine ulishikilia nafasi za juu kwenye mitandao ya kusikiliza muziki kama vile Youtube. Pia Weusi waliachia wimbo unaoitwa Penzi la Bando wakimshirikisha malkia wa mipasho Khadija Kopa, kundi la Rostam nalo lilirudi na kibao kinachoitwa Sifa baada ya kutofanya kazi pamoja kwa muda mrefu.


HUZUNI

Kwenye furaha huzuni haikosi, ndivyo ilivyokuwa mwezi huu. Licha ya shangwe zake, pia misiba iliyowahusu wasanii ilitokea.

Msiba uliowagusa wengi zaidi ulikuwa ni wa msanii wa muziki wa dansi wa muda mrefu, Waziri Sonyo ambaye alipoteza maisha Februari 23.

Sonyo alitamba kupitia bendi za Tanzania One Theatre, Tamtam na Chuchu Sound alifariki nyumbani kwao Kibaha mkoani Pwani baada ya kutoka kutazama mechi ya Simba dhidi ya Al Ahly huku familia ikithibitisha kuwa chanzo cha kifo chake ilikuwa ni shinikizo la damu. Mbali Sonyo, pia wasanii Darassa CMG alimpoteza baba yake mzazi na mbunifu wa mavazi Martin Kadinda alimpoteza mama yake mzazi.

Advertisement