Q Chief aomba radhi kwa kumtukana Diamond

Saturday February 27 2021
q chief pic

Q Chief

By Kelvin Kagambo

Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Abubakar Katwila 'Q Chief' ameomba radhi mashabiki na wadau wa muziki wake kwa lugha za matusi alizozitoa kuzielekeza kwa msanii Diamond Platnumz na meneja wake Sallam Sharaff maarufu Mendez.

Kama ulipitwa ni kwamba, mwanzoni mwa mwezi Februari ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Q Chief akiwatukana Diamond na Sallam kwa kutumia jina na picha yake kwenye bango linaloonyesha orodha ya wasanii watakaotumbuiza kwenye shoo ya Wasafi Tumewasha iliyofanyika Januari 31 jijini Dar es Salaam ilihali Q Chief hakuwepo miongoni mwa wasanii waliotumbuiza kwenye tamasha hilo.

Akizungumza na Mwanachi Q Chief ambaye aliwahi kutamba na wimbo wa Ninachokipata alisema yeye ni binadamu na huwa anakasirika anapoudhiwa.

"Mimi sina mbawa, ni binadamu wakaida kwahiyo nakasirika, nachukia na naumia mtu anaponifanyia mambo ambayo siyapendi." Alisema.

Aidha, Q Chief amefafanua kwamba msamaha huo haumaanishi kuwa ameacha kufutuatilia suala lake na kina Diamond.

"Tuliwaandikia barua ya kisheria na wameijibu juzi lakini nisingependa kusema wametujibu nini kwa sababu ni suala ambalo liko mikononi mwa vyombo vya dola kwa sasa." Alisema.

Advertisement

Kwa kuweka kumbukumbu sawa wakati video hiyo 'inatrend' Mwananchi lilimtafuta meneja wa Diamond, Sallam na kumuuliza kama ameona video hiyo lakini alijibu kuwa hajaiona na wala hamfahamu msanii anayeitwa Q Chief.

Advertisement