Eti Janjaro kuna vitu anapewa

Monday April 05 2021
JANJAROO PIC
By Kelvin Kagambo

RAPA kutoka pande za Arachuga lakini aliyebobea jijini Dar es Salaam, Dogo Janja a.k.a Janjaro amekuwa akishutumiwa na mashabiki zake kwa muda mrefu sasa kwamba, amezima moto wa kufanya kazi na amewekeza muda mwingi kwenye mapenzi kwani kila kukicha amekuwa akionekana akitanua na ‘baby’ anayefahamika kwa jina la Linna Totoo.

Ikumbukwe, wimbo wa mwisho alioutoa miezi miwili iliyopita haukupata mafanikio ya kutosha huku maoni ya baadhi ya mashabiki kwenye Instagram yake yakidai kuwa ni kwa sababu hakuitangaza vya kutosha.

Mwanaspoti lilimvaa baba wa muziki wa Janjaro, yaani Madee na kumtupia swali la kulikoni, mbona mwanao kama amelewa sana na mapenzi. Madee alikuwa na haya ya kusema: “Sidhani kama Janjaro kalewa mapenzi kiasi hicho mpaka akaacha kufanya kazi. Wanaosema anatanua wanaona picha za Instagram na usikute zimepigwa tangu mwaka jana.”

Bosi huyo wa lebo ya Manzese Music Baby, amejazia akidai ni kawaida kwa mtu kunogewa na mapenzi pale anapopata mtu anayeendana naye, ndiyo maana labda watu wanamchukulia Janjaro kama kalewa mapenzi.

“Itakuwa kuna vitu wanapeana. Lakini ni kawaida sana, ukizungukazunguka baadaye ukampata mtu unayependana naye kweli siku zote lazima ulewe mapenzi, nadhani mwanangu anapatia wakati huo kwa sasa.”

Advertisement