Prime
DOGO JANJA: Kuhusu mapenzi, ngoma mpya huu ndo ukweli

Muktasari:
- Ni kweli mrembo huyo inaelezwa anatoka katika familia yenye pesa na wengi wanaamini ndiyo maana Dogo amerilaksi lakini mwenyewe anapinga vikali na anafunguka kila kitu.
MBONA kimya. Hili ni swali kwa mkali wa Hip Hop kutoka Arusha, Dogo Janja ambaye baada ya kuangukia kwenye penzi la mrembo Queen Linah, wengi wanaamini ndiyo sababu za kutokutoa nyimbo na maisha kwake ni murua kutokana na mwanadada huyu kuwa na pesa.
Hata hivyo kama ilivyo mitazamo ya wengi kutokana na ukimya wa Dogo Janja, Mwanaspoti kupitia ukurasa huu wa Dakika 5 Na... lilimnasa na kutaka kujua ukweli kuhusu maisha yake na mitazamo ya watu.
Ni kweli mrembo huyo inaelezwa anatoka katika familia yenye pesa na wengi wanaamini ndiyo maana Dogo amerilaksi lakini mwenyewe anapinga vikali na anafunguka kila kitu.

KUHUSU KUACHA MUZIKI
Mkali huyo wa nyimbo kama 'Kidebe' Ngarenaro' 'My Life', 'Banana' na nyingine anasema kamwe hawezi kuacha muziki na ukimya wake una maana kubwa kwake.
"Weee hapana, sijaacha muziki bado nipo kwenye game bana. Usione nipo kimya hivi, ni ubize tu wa majukumu ya hapa na pale, nakosa muda wa kuingia studio, ila 'soon' nitatoa kitu kwa mashabiki zangu."
"Mimi maisha yangu ni muziki ukitoa tu kuimba, nafanya biashara ya muziki, naweza kuwa kimya nisitoe nyimbo lakini nazalisha muziki, niimbe nisiimbe mie naishi, wanamuziki wasiniige mimi maana nina siri kubwa ya maisha yangu kwenye muziki na bado nipo sana hata nikizieka sitaacha muziki."
KUNA DUDE LINAKUJA
"Niwaambie tu mashabiki zangu wasiwe na shaka juu suala la mimi kutotoa nyimbo, nina staili yangu katika hii game. Nina tabia ya kusikilizia wimbo nilioutoa unaenda kwa umbali gani kwa mashabiki zangu ndipo natoa nyingine. Ndiyo maana unaweza kukuta mwaka au miezi sijatoa nyimbo mpya sababu nausikilizia wimbo ninaoutoa uishi kwanza."

Mbali na muziki unafanya nini?
"Ohh! we jua tu mimi ni mfanyabiashara, ila usitake kujua nafanya biashara gani na mtu akitaka kujua lazima atapotea, mie ni mwekezaji wa vitu vingi, kiufupi sina ndoto ya kufa masikini."
Ni kweli mwanamke amekupiga pini?
"Mimi nampenda sana mwanamke wangu, Kunipiga pini ki vipi? (kicheko), kama watu hawajui labda, mimi katika maisha yangu sijawahi kufikiria kumtegemea mwanamke kuendesha maisha yangu, bali nimekuwa nikipambana mwenyewe kupigana na maisha. Sijawahi kuamini kupitia pesa ya mwanamke, hata nikiwa na mwanamke akinipa hela huwa namuacha kwa sababu sijawahi kupenda kuitwa king'asti au kufugwa. Mimi naamini kula nguvu yangu, naamini kula jasho langu kwa hiyo hilo la kulelewa halipo, najimudu mimi."

Kabla ya ustaa ulikuwa ni mtu wa aina gani?
"(Akicheka). Mie nadhani ningekuwa muhuni, mtukutu na mtu wa fujo za ajabu ajabu. Dunia ingenifahamu kwa hivyo, ila nashukuru sana niko hai hadi sasa kwani wenzangu niliokuwa nao kundi moja walishafariki dunia, wengine wemechomwa moto, wengine wamepigwa mawe hadi kufa kwa sababu ya utukutu, unyang’anyi, Mungu ni mwema sana."
Bifu na Uwoya
"Kwa sasa sina tatizo na Irene Uwoya, mimi na yeye tulishamaliza bifu letu, tumepatana kitambo tu na tunaongea kama kawaida japo kila mtu sasa hivi ana maisha yake, pia nampongeza kwa kubadilisha maisha yake na kuwa mtu wa Mungu, amefanya jambo jema sana na Mungu atamsaidia kufika mbali kwenye safari yake hiyo."
Dogo Janja ni mtu wa namna gani?
"Dogo Janja ni mtu ambaye akijua humpendi yeye ndio anakupenda, halafu sio mtu wa kuweka kinyongo na wala sio mtu wa mabifubifu, naelewana na kila mtu."

Kuhusu kuwa na dharau
"Yaah watu wengi ambao hawako karibu na mimi huwa wananiambia nina dharau sana, lakini siko hivyo. Mimi naheshimu kila mtu, sema kinachoniponza ni uchangamfu wangu wa kuongea sana. Naongea sana nikiwa na watu niliowazoea."
"Unajua mimi maisha yangu ya sanaa yalikuwa Arusha, Arusha ni mji ambao naishi kwa muda mrefu, sasa mwanzoni nilipokuja Dar es Salaam nikawa naongea na watu na hii lafudhi yangu basi watu wa Dar walidhani mimi ni mtu wa dharau, hadi sasa wapo wanaosema hivyo ila mimi nipo freshi kinoma."
Ushauri kwa wanamuziki wa sasa
"Nashauri tu baadhi ya wasanii wa sasa wawe na nidhamu ili wafanikiwe kati kazi zao. Mimi hadi leo nina nidhamu sababu ya kufundishwa na Madee. Sasa wanamuziki wa sasa hivi wanaweza kuropoka chochote hadi unasema hee! huyu msanii ana nidhamu kweli? Yuko sawa kweli, anausimamizi kweli? Kiufupi waache umachinoo wapige kazi kwa nidhamu."