DJ Khaled, kibonge mpambanaji

MIAMI, MAREKANI. HIVI karibuni Khaled Mohammed Khaled ama DJ Khaled kama watu wengi wanavyomfahamu, alishika vichwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari duniani baada ya kufichua katika albamu yake mpya anayotarajia
kuitoa mwaka 2024, itakuwa na wimbo aliomshirikisha supastaa Drake.
Ukiondoa hii, kipande cha video cha staa huyu kwenye wimbo wa Hold you down kilichomuonyesha anampa mwanamke pesa bila ya kufikiria kilifurahisha.
Licha ya wimbo huo kutoka muda mrefu lakini kipande hicho kilisambaa sana katika siku za hivi karibuni hususani
wakati wa dirisha lililopita la usajili ambapo watu walikuwa wakifananisha tukio hilo na jinsi timu za Saudia
zinavyoshawishi mastaa wa Ulaya. Leo tumekueletea hapa uone jinsi jamaa anavyoishi kibosi na anavyoingiza pesa.
ANAPIGAJE PESA
Kwa ujumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 75 milioni. DJ Khaled kwanza alianza kuzikunja kwa
kutengeneza ngoma za wasanii mbalimbali wa Marekani kama Jay-Z, Lil Wayne, na Kanye West.
Ukiondoa ngoma hizo, Khaled pia ametengeneza albamu zake zisizopungua mbili na albamu yake iliyowahi
kuuza vizuri zaidi ni ile ya ‘Major Key’€ iliyotoka mwaka 2016 ambayo ndani ya Marekani tu, ilinunuliwa mara 3 milioni.
Kwa ujumla inatajwa kuwa ilimlipa kiasi kisichopungua Dola 20 milioni kutokana na mauzo yake.
Mtaalamu huyu pia amekuwa akipewa kazi ya kuwa DJ kwenye matamasha ambako amekuwa akikunja zaidi ya Dola 1 milioni kwenye kila shoo.
Pia, ana kipindi chake binafsi kiitwacho The Khaled Khaled Show ambacho kinaruka kupitia App ya Apple Music.
Kwa mwaka anadaiwa kukunja Dola 10 milioni kupitia kipindi chake na U Dj.
Anapata kiasi kisichopungua Dola 30 milioni kupitia mikataba ya udhamini na biashara zake binafsi.
Khaled ni balozi wa kampuni za Apple, Ciroc na Weight Watchers.
Anamiki kampuni yake ya mavazi iitwayo ‘We the Best’.€ Amewahi pia kuandika vitabu viwili ‘The Keys’ na ‘The Gift’ ambavyo vimempatia zaidi ya Dola 7 milioni kwenye mauzo.
MITANDAO YA KIJAMII
Kupitia mitandao yake ya kijamii huwa anatumia kutangaza muziki na biashara zake kwa ujumla na kwa mujibu wa taarifa ni kwamba anakunja Dola 5 milioni kwa mwaka kupitia akaunti yake ya Instagram.
NDINGA
Gari anazomiliki ni 2017 Rolls Royce Wraith Coupe Dola- 285,000 Cadillac Escalade Dola 76,990
2017 Rolls-Royce Dawn Dola 346,000, 2018 Rolls Royce Phantom VIII Dola 450,000, 2017 Rolls-Royce Phantom Drophead Coupe Dola 533,000, 2012 Maybach 57S Dola 417,400, 2012 Maybach 62S Landaulet Dola 1,300,000
MJENGO
Januari 2017, alinunua nyumba ya zamani ya Robbie Williams iliyopo huko Mulholland Estates, Los Angeles kwa Dola 9.9 milioni na akaiuza Aprili, 2021 kwa 12.5 milioni, ikiwa ameingiza faida ya Dola 1.5 milioni.
Mwaka 2018, alinunua mjengo wa kifahari uliopo kwenye fukwe huko Miami kwa Dola 25.9 milioni.
MAISHA NA BATA
Amekuwa kwenye uhusiano wa muda mrefu Nicole Tuck ambaye huwa anamwita ‘My Queen’, wawili hawa wamekuwa pamoja kwa muda mrefu sasa na wamebahatika kupata watoto wawili pamoja mbao ni Asahd na Aalam. wote wakiume.