Diamond Platnumz awaburuza mastaa Afrika

HADI sasa mwanamuziki kutokea visiwa vya Puerto Rico, Luis Fonsi kupitia video ya wimbo wake, Despacito iliyotoka Januari 13, 2017 anashikilia rekodi ya video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube duniani ikiwa na 'views' zaidi bilioni 8.3.
Je, barani Afrika mambo yapo vipi hasa ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara? hizi ni video 15 za wasanii kutoka eneo hilo ambazo zimetamzwa zaidi YouTube hadi kufikia Februari 2024.
Wasanii wa Nigeria na Afrika Kusini ndio wanatawala, huku Diamond Platnumz kutokea Tanzania akiwa msanii pekee Afrika Mashariki aliyefanikiwa kuchomoza katika orodha hii.

1. Rema, Selena Gomez - Calm Down (Mil. 788+)
Staa wa Nigeria, Rema alitoa toleo (version) lingine la wimbo wake, Calm Down (2022) na kumshirikisha Selena Gomez, uamuzi huo umekuwa na matunda mengi maana wimbo huo umefanya vizuri duniani hadi kuteuliwa kuwania Grammy.
Huu wimbo umeandika rekodi kama wimbo wa kwanza barani Afrika kusikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, na umeshinda tuzo ya MTV Video Music Awards Marekani katika kipengele cha Afrobeats.
Sasa video yake iliyotoka Septemba 7, 2022 ina 'views' zaidi ya milioni 788, huku lile toleo la awali likiwa na 'views' zaidi ya milioni 568, ndio wimbo pekee Afrika uliotazamwa zaidi YouTube Afrika kwa kipindi kifupi.
Utakumbuka Rema alianza kupata umaarufu baada ya kutoa wimbo wake, Dumebi (2019), na baadaye D'Prince alimsaini katika rekodi lebo ya Jonzing World ambayo ni kampuni tanzu ya Mavin Records inayomilikiwa na Don Jazzy.

2. Master KG ft. Nomcebo - Jerusalema (Mil. 595+)
Wimbo huu ulitoka Novemba 29, 2019 na kupata mapokezi makubwa Afrika Kusini, video yake ilifuata Desemba 12, 2019 na sasa ndio video iliyotazamwa zaidi Afrika YouTube ikiwa na 'views' zaidi ya milioni 595. Huu wimbo alikuja kuuweka kwenye albamu yake ya pili, Jerusalema (2020).
Wimbo huu una remix mbili, ya kwanza ilitoka Juni 2020 akimshirikisha Burna Boy wa Nigeria, ilifanya vizuri na kuingia chati za Billboard huko Marekani. Remix ya pili ilitoka Septemba 2020 ambapo aliwashirikisha Venezuela Micro TDH na Greeicy kutokea Colombia.
Ikumbukwe Master KG ambaye ni mwanzishili wa dansi maarufu 'Bolobedu', kupitia albamu yake, Skeleton Move aliweza kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) katika kipengele cha Best Artist/Group in the African Electro.

3. Ckay - Love Nwantiti (Mil. 457+)
Agosti 30, 2019 msanii kutokea Nigeria, Ckay aliachia Extended Playlist (EP) iitwayo 'Ckay' yenye nyimbo nane chini ya Chocolate City na Warner Music Group, ndani yake ndipo kuna ngoma, Love Nwantiti iliyochiwa Agosti 29, 2019.
Video ya ngoma, Love Nwantiti ilitoka Februari 14, 2020 na tayari ina 'views' zaidi milioni 470 ikiwa ndio inaongoza Nigeria, huku ikishika nafasi ya tatu Afrika. Hii ni remix akiwashirikisha Joeboy na Kuami Eugene.
Wimbo huu umechangia sehemu kubwa ya mafanikio ya EP hiyo ambayo aliweza kuingia kwenye chati za Billboard nchini Marekani, Canada na Uholanzi, pia iliingia kwenye chati za Ufaransa (SNEP).

4. Magic System ft. Chawki – Magic in the Air (Mil. 450+)
Kundi la Magic System lilianzishwa mwaka 1996 huko Abidjan nchini Ivory Coast, wasanii wake ni Salif 'Asalfo' Traore, Narcisse 'Goude' Sadoua, Étienne 'Tino' Boué Bi na Adama 'Manadja' Fanny.
Mwaka 2014 waliachia wimbo wao, Magic in the Air wakimshirikisha Chawki kutokea Morocco, ni miongoni mwa nyimbo zilitoka kwa ajili ya kusherehesha fainali za Konde la Dunia zilizofanyika nchini Brazil mwaka 2014.
Video yake ilitoka Machi 17, 2014 na hadi sasa ina 'views' zaidi ya milioni 450 YouTube na kuzidi kuliweka kundi hilo katika ramani baada ya kufanya vizuri Afrika Magharibi na mtindo wa dansi 'Zouglou' hadi kutambulika kama miongoni mwa wasanii wakubwa Ufaransa kutokea Afrika.

5. Burna Boy – On the Low (Mil. 369+)
Ngoma yake, On The Low ambayo ni mchanganyiko wa Afrobeat na Dancehall imempatia mafanikio makubwa mwimbaji huyo kutokea Nigeria ambaye alivuma zaidi mwaka 2012 baada ya kuachia ngoma, Like to Party kutoka kwenye albamu yake, L.I.F.E (2013).
Video ya wimbo huo uliyotayarishwa na Kel P ilitoka Novemba 16, 2018 ikiongozwa na Meji Alabi, tayari imefikisha 'views' zaidi ya milioni 369. Vilevile video ya wimbo wake, Last Last iliyotoka Mei 13, 2022 tayari ina 'views' zaidi ya milioni 255.7.
Ikumbukwe Burna Boy ambaye mwaka 2017alisaini na Bad Habit/Atlantic Records ya Marekani na Warner Music Group, ameshinda tuzo nne za BET na moja ya Grammy kupitia albamu yake ya tano, Twice As Tall.

6. Ayra Starr -Rush (Mil. 303+)
Ndio video ya kwanza ya msanii wa kike solo kufikisha 'views' zaidi ya milioni 300 YouTube nchini Nigeria, ilitoka rasmi Septemba 26, 2022 chini ya Mavin Records ambayo inamsimamia Rema pia.
Wimbo huu kutoka katika albamu yake, 19 & Dangerous (2021) ulianza kuvuma TikTok na baadaye kila sehemu, umepa Ayra Starr nafasi ya kuwania tuzo za Grammy 2024 ambapo anachuana na Asake, Burna Boy, Davido na Tyla wa Afrika Kusini.

7. Davido - Fall (Mil. 280+)
Mwimbaji huyo wa Nigeria alianza muziki katika kundi la KB International, Davido alipata umaarufu mwaka 2011 alipoachia ngoma yake, Dami Duro ambayo ni ya pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo.
Mwaka 2017 baada ya kurekebisha mkataba wake na Sony Music, Davido alitoa nyimbo tano ukiwemo 'Fall' ambao ulifanya vizuri hadi chati za Billboard, video yake iliyotoka Juni 2, 2017 na imefikisha 'vies' milioni 280.
Kupitia X (Twitter) mwaka 2016 Davido alitangaza kusaini mkataba na Sony Music, miezi michache baadaye alianzisha lebo yake, Davido Music Worldwide (DMW) na kuwasaini Dremo na Mayorkun.

8. Die Antwoord – Baby On Fire (Mil. 272+)
Ni kundi la muziki wa Hip Hop kutokea Afrika Kusini lililoanzishwa mjini Cape Town mwaka 2008 na Marapa wawili, Ninja na Yolandi Visse, mwaka 2009 walitoa albamu yao ya kwanza, $O$ bila malipo mtandaoni na kuwatangaza vilivyo.
Kufika Juni 2, 2012 waliachia video ya wimbo wao 'Baby On Fire' ikiongozwa na Ninja na Terence Neale, hadi sasa huko YouTube imefikisha 'views' zaidi ya milioni 272.
Mwaka 2011 Die Antwoord walianzisha lebo yao wenyewe, Zef Recordz na kufuatia mfululizo wa albamu zao kali kama Ten$Ion (2012), Donker Mag ("Dark Power"; 2014) na Mount Ninji and da Nice Time Kid (2016).

9. Wizkid - Joro (Mil. 265+)
Ni mwimbaji kutokea Nigeria, ameshinda tuzo zote kubwa Afrika, pia ameshinda BET na Grammy kupitia wimbo, Brown Skin Girl aliyopewa shavu na Beyonce katika albamu yake, The Lion King: The Gift.
Hapo Septemba 30, 2019 aliachia video ya wimbo wake, Joro na hadi sasa ina 'views' milioni 265, ikifuatiwa na video ya wimbo wake 'Essence' akimshirikisha Tems ambayo ina 'views' zaidi ya milioni 175.2 tangu itoke rasmi hapo Aprili 9, 2021.

10. Sinachi – Way Maker (Mil. 251+)
Ni mwimbaji wa muziki wa Injili kutokea Nigeria na kiongozi wa kanisa la Loveworld, ametoa nyimbo maarufu kama 'I Know Who I Am', 'Great Are You Lord', 'Way Maker', 'Jesus is Alive', 'Rejoice' n.k.
Video ya wimbo wake, Way Maker iliyotoka Desemba 30, 2015 imefikisha 'views' zaidi ya milioni 251 YouTube, ndio video namba mbili ya msanii wa kike yenye mafanikio zaidi Afrika.
Ikumbukwe Sinachi anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kuongoza kwenye chati za Billboard Christian Songwriter kwa wiki 12 mfululizo. Septemba 2019 alikua msanii wa kwanza wa Injili kutoka Afrika kuzuru India na kuongoza matamasha makubwa.

11. Innoss'B ft. Diamond Platnumz – Yope Remix (Mil. 223+)
Hadi sasa Staa wa Bongofleva kutoka WCB Wasafi, Diamond Platnumz ameshiriki katika video nne zilizofikisha 'views' zaidi ya milioni 100 YouTube, video hizo ni Yope Remix, Inama, Waah! na Time To Party.
Video ya Yope Remix ambayo Diamond kashirikiana na Innoss'B kutokea DR Congo ilitoka Septemba 7, 2019 na hadi sasa ina 'views' zaidi milioni 223 YouTube na ndio video inayoongoza Afrika Mashariki.
Ikumbukwe Diamond ambaye ametoa albamu tatu, EP moja, huku akishinda tuzo zaidi 40, ndiye msanii pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye video zake zote zimefanikisha kufikisha jumla ya 'views' zaidi ya bilioni 2 YouTube.

12. Tekno - Pana (Mil. 207+)
Mwimbaji huyo wa Nigeria alianza muziki chini ya K-Money Entertainment, mwaka 2013 akasaini tena Made Men Music Group na kutoa nyimbo kama Dance na Anything zilifanya vizuri hadi kuwania tuzo za Nigeria Entertainment 2014.
Mwaka 2015 Tekno alitoa wimbo wake maarufu 'Duro', kisha ukafuata, 'Pana' ambao video yake ilitoka Agosti 22, 2016 na hadi sasa ina 'views' zaidi ya mara milioni 207 YouTube.
Kufika Julai 2019, Tekno alishirikishwa kwenye wimbo uitwao 'Don’t Jealous Me' kutoka katika albamu ya Beyonce, The Lion King: The Gift, pamoja na Yemi Alade na Mr. Eazi.

13. Die Antwoord – Ugly Boy (Mil. 201+)
Inashikilia redodi ya kuwa video ya tatu ya muziki iliyotazamwa zaidi nchini Afrika Kusini, ilitoka Novemba 2, 2014 na hadi sasa imepata 'views' zaidi ya milioni 201 YouTube.
Vile vile, video ya wimbo wao, I Fink u Freeky iliyotoka Januari 31, 2012 imefikisha 'views' zaidi milioni 188, ndio kundi lenye mafanikio makubwa zaidi katika mtandao wa YouTube barani Afrika.

14. Davido - If (Mil. 176+)
Ikumbukwe awali hii ndio ilikuwa video ya Davido iliyotazamwa zaidi YouTube lakini ikaja kuzidiwa na 'Fall' iliyotoka miezi minne baadaye ndani ya mwaka 2017. Video ya wimbo, If ilitoka Februari 17, 2017 na imeweza kufikisha 'views' milioni 176.

15. Yemi Alade - Johnny (Mil. 161+)
Ni mwimbaji wa Nigeria, alianza muziki mwaka 2009, alingoja hadi 2013 alipofanikiwa kutoa wimbo wake maarufu Afrika, Johnny kisha ikafuata albamu yake ya kwanza, King of Queens (2014) chini ya Effyzzie Music Group.
Video ya wimbo wake, Johnny iliyotoka Machi 3, 2014 na tayari imejikusanyia 'views' zaidi ya milioni 161 YouTube.
Ikumbukwe hadi mwanzoni mwa mwaka 2019 Yemi Alade alikuwa ndiye mwimbaji wa kwanza wa kike Afrika kuweza kufikisha 'views' milioni 100 YouTube, pia akiwa ni msanii wa pili Nigeria baada ya Davido.
