Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Coleen wa Rooney anakula kivulini

Muktasari:

  • Hiyo ni baada ya ripoti iliyotoka wiki hii kuonyesha bibie kApiga hatua kubwa kiuchumi kuliko mumewe, Rooney. Coleen anaripotiwa kupata faida ya Pauni1.3 milioni kutokana na shughuli zake za biashara na udhamini wa chapa kupitia kampuni yake, CWR 2021.

BAADA ya kuchumia juani, yaani zile panda shuka zilizokaribia kuisambaratisha ndoa yake na Wayne Rooney, 39, sasa mke wa mchezaji huyo wa zamani wa England na Manchester United, Coleen McLoughlin, 39, analia kivulini kwa sehemu. 

Hiyo ni baada ya ripoti iliyotoka wiki hii kuonyesha bibie kApiga hatua kubwa kiuchumi kuliko mumewe, Rooney. Coleen anaripotiwa kupata faida ya Pauni1.3 milioni kutokana na shughuli zake za biashara na udhamini wa chapa kupitia kampuni yake, CWR 2021.

Ripoti mpya ya kifedha kwa mwaka ulioishia Septemba 2024, ilionyesha kuwa mapato yake yameongezeka zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miezi 12, ikiwa ni ongezeko kubwa linaloonyesha nguvu ya miradi yake. Hata hivyo, mapato ya hivi karibuni ya mumewe hayawezi kulinganishwa na mafanikio ya Coleen kwani Rooney aliripotiwa kupata takriban Pauni 500,000 kwa mwaka akiwa kocha wa Plymouth Argyle kabla ya kuondoka Desemba 2024.

Kwa sasa Coleen amekuwa chapa yenye nguvu kupitia jina lake binafsi, umaarufu wake uliongezeka zaidi baada ya kushiriki katika kipindi cha I'm A Celebrity...Get Me Out Of Here kinachorushwa na ITV Uingereza. Inaripotiwa alipokea kiasi kikubwa cha fedha kwa kushiriki katika I'm A Celeb, na vyanzo vya ndani vinadai malipo yake kutoka ITV yalifikia hadi kiwango cha tarakimu saba (yaani, zaidi ya Pauni 1 milioni).

Ni wazi kuonekana katika kipindi hicho kumemuongezea Coleen mvuto mbele ya umma na pia kuimarisha thamani yake kibiashara ambapo anaendelea kushirikiana na chapa ya virutubisho vya mwili, Applied Nutrition. Kwa sasa Coleen ni mtu maarufu kwenye vyombo vya habari Uingereza, kwani aliwahi kuandika safu ya maoni 'Welcome to My World' kwenye jarida la Closer kisha 2008 akaondoka hapo na kujiunga na OK! ambako aliandika safu ya kila wiki kuhusu mitindo.

Je, mrembo huyo ni nani hasa? Wapi anatokea na yapi amevumilia katika ndoa yake na Wayne Rooney iliyodumu kwa miaka 16 sasa licha ya panda shuka kibao? Coleen ambaye familia yake ina asili ya Ireland alizaliwa Aprili 3, 1986 huko Liverpool akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya wanne, huku baba yake Tony McLoughlin akiwa fundi ujenzi na pia alisimamia klabu ya ndondi.

Akiwa na umri wa miaka 12 ndipo alikutana na Rooney wakati huo wote wakiwa wanafunzi wa sekondari huko Croxteth, Liverpool, lakini uhusiano wao rasmi ulianza wakiwa na miaka 16 baada ya kumaliza shule. Mama yake Rooney, Jeanette, alikuwa akifanya kazi ya usafi katika Chuo cha St John Bosco Arts College ambacho Coleen alisomea sanaa ya uigizaji, ila wakati huu ni mlezi wa shirika la hisani la watoto, Alder Hey Children’s Charity lenye makao yake Liverpool.

Rooney na Coleen walifunga ndoa Juni 12, 2008 mjini Portofino, Italia, huku jarida la OK! likiripotiwa kuwalipa wanandoa hao Pauni 25 milioni ili kupata maudhui ya kipekee kama picha kutoka katika harusi hiyo. Wanandoa hao wamejaliwa kupata watoto wanne na wote ni wa kiume - Kai Wayne (alizaliwa Novemba 2, 2009), Klay Anthony (Mei 21, 2013), Kit Joseph (Januari 24, 2016) na Cass Mac (Februari 15, 2018).

Kabla ya ndoa, mwaka 2004, akiwa bado anachumbiana na Coleen, Rooney alikiri kutumia huduma za 'kina dada wa barabarani' jijini Liverpool na alisema tukio hilo la aibu alilifanya kwa sababu alikuwa bado kijana mdogo na mpumbavu. Gazeti la Sunday Mirror liliripoti kuwa Rooney alitembelea 'chimbo' la Liverpool mara 10 na alionekana kwenye CCTV akiingia na kutoka, akihusishwa na wanawake watatu wenye umri wa miaka 21, 37, na 48 – ambaye alisemekana kuwa ni bibi mtu mzima.

Aprili 2006, Rooney alishinda kesi ya kashfa dhidi ya magazeti ya The Sun na News of the World yaliyodai kuwa alimpiga Coleen katika klabu ya usiku. Kufuatia shauri hilo, alilipwa fidia ya Pauni 100,000 aliyokuja kuitoa kama msaada kwa jamii. Coleen akizungumza kwenye kipindi cha I’m A Celebrity...Get Me Out Of Here, alisema ndoa yao imehitaji juhudi na uvumilivu mkubwa kutokana na makosa makubwa aliyowahi kuyafanya Rooney.

Rooney akiwa mcheza soka maarufu alitembelea saluni za usingaji (massage), ili kukutana na 'kina dada wa barabarani', na tabia hiyo iliendelea hata wakati wa taaluma yake ya ukocha, huku akihusishwa na wanawake wengine na kushtakiwa mara kadhaa. Mwaka mmoja baada ya kuzaliwa mtoto wao wa kwanza, Kai (2019), kuliibuka madai mengine ya Rooney kuchepuka. 'Dada mmoja wa barabarani' aitwaye Helen Wood, alidai kutembea na mchezaji huyo kipindi Coleen akiwa mjamzito. Muda mfupi baada ya kuondoka Man United 2017, Rooney alikamatwa kwa kuendesha gari akiwa amelewa. Mbaya zaidi, gari hilo halikuwa lake, bali la mwanamke aitwaye Laura Simpson aliyekutana naye usiku huo.

"Watu wengine wanaweza kufikiri mimi ni mjinga kwa kubaki kwenye ndoa hii. Sijarogwa, najua nachotaka na nahitaji kujaribu kuilinda ndoa yangu kwa sababu nataka maisha ya familia," Coleen aliandika kupitia Facebook.

Agosti 2019, Rooney akiwa Marekani kama kocha wa DC United alionekana akipanda lifti ya hoteli na mwanamke asiyejulikana saa 11 alfajiri. Baada ya picha hizo kusambaa, MailOnline ilidai Coleen alimwamuru kurudi Uingereza na alivua pete ya ndoa. Hata hivyo, katika makala yake ya Amazon, My Account: The Autobiography (2023), Coleen alisema kuwa alimsamehe Rooney lakini yote aliyotenda hayakubaliki. Lakini jambo wakishalizungumza huwa yanaisha mara moja na maisha mengine yanaendelea bila hasira zozote.