BONGO MUSIC FACT: Ibraah na Harmonize kila mwaka wana jambo

Muktasari:
- Akiwa ametoa EP mbili, Steps (2020), Karata 3 (2021) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022), Ibraah a.k.a Chinga amejizolea umaarufu kwa tungo zake zinazohusu mapenzi na starehe. Mfahamu zaidi;.
MIAKA minne aliyonayo ndani ya Bongo Fleva imetosha kuonyesha ukubwa wa kipaji chake, Ibraah kutokea Konde Music Worldwide, lebo yake Harmonize, ni miongoni mwa waimbaji wapya waliofanya vizuri miaka ya hivi karibuni.
Akiwa ametoa EP mbili, Steps (2020), Karata 3 (2021) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022), Ibraah a.k.a Chinga amejizolea umaarufu kwa tungo zake zinazohusu mapenzi na starehe. Mfahamu zaidi;.
1. Ibraah alianza kuimba akiwa shule ya msingi huko Mtwara, kipaji chake kikamfanya kuwa msanii bora wa shule, msanii bora wa kata na mwaka 2014 akawa msanii bora wa wilaya (Tandahimba) kati ya wasanii 36 waliokuwa wanawania nafasi hiyo.
2. Baadaye Ibraah alikuja Dar es Salaam na kuanza kazi ya umachinga na ndio sababu ya kujiita ‘Chinga’, alikuwa anauza CD, huku akiwa na ndoto kubwa ya kufanya muziki ila hakujua wapi pa kuanzia hadi kuja kufanikiwa.
Aliposikia Harmonize amefungua lebo, Konde Music akawa kila mara anaenda kugonga hodi katika ofisi hiyo kuomba nafasi ya kusainiwa ila hakufanikiwa kukutana na Harmonize.
3. Aliyekuwa prodyuza wa Harmonize, Bonga alipokutana na Ibraah alivutiwa na uwezo wake kimuziki, akamshauri akatafute fedha ya kurekodi na mpango wa kuchukuliwa na Konde Music asiufikirie sana.
Ibraah akakubali wazo la Bonga, hivyo akasaka fedha ya kurekodi hadi kuipata na kweli akarekodi, punde tu aliyekuwa DJ wa Harmonize, Seven aliposikia wimbo huo akaupenda na kwenda kumsikilizisha Harmonize ambaye alivutiwa nao na kukubali kumsaini.
4. Hivyo Ibraah ndiye msanii wa kwanza kusainiwa Konde Music Worldwide kisha wakafuata wengine kama Country Boy, Cheed, Killy, Anjella na Young Skales kutoka Nigeria ila sasa amebaki peke yake katika lebo hiyo.
5. Harmonize alimkuta Ibraah amesharekodi wimbo, One Night Stand (2020) akaupenda na kuomba kuongeza vesi yake kitu ambacho Ibraah alikubali na ulipotoka ukafanya vizuri na hadi sasa video yake ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 20 YouTube.
6. Mnamo Aprili 11, 2020 ndipo Konde Music walitangaza kumsaini Ibraah aliyetambulishwa na EP yake, Steps (2020) ikiwa na nyimbo tano, huku akiwashirikisha Harmonize pamoja na wasanii wawili wa Nigeria, Joeboy na Skibii.
7. Tangu ameanza muziki Ibraah hajawahi kushinda tuzo yoyote zaidi ile aliyopewa na kipindi cha Empire cha E FM Radio kama Msanii Bora Chipukizi 2020.
8. Albamu ya kwanza ya Ibraah, The King of New School (2022) haikushirikisha msanii yeyote wa Konde Music, waliopata nafasi ni wale kutoka nje ya lebo hiyo ambao ni Maud Elka, Christian Bella, L.A.X, Waje, AV, Roberto na Bracket.
9. Jina alilopewa na wazazi wake ni Ibrahim Abdallah Nampunga, hivyo hilo la Ibraah amelitoa huko ila kwenye Bongo Fleva alikuta kina Ibraah wenzake wawili.
Kuna Ibra Nation aliyetolewa na Tanzania House of Talent (THT) kupitia wimbo wake, Nilipize (2017), pia kuna Ibra Da Hustler wa kundi la Nako 2 Nako Soldiers.
10. Tangu amejiunga Konde Music mwaka 2020, kila mwaka Ibraah amekuwa anatoa wimbo na Harmonize, tayari wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni One Night Stand (2020), Addiction (2021), Mdomo (2022), Tunapendeza (2023) na Dharua (2024).