Angel Di Maria na Jorgelina wanamalizia walipoanzia!
Muktasari:
- Moja ya kumbukumbu nzuri za Di Maria kuhusu Rosario, siyo soka tu, bali ni alipokuwa akiichezea klabu hiyo kabla ya kutimkia Ulaya, ndipo alipokutana na mkewe Jorgelina Cardoso, 43, ambaye pia ni wakala wa michezo.
Mshindi wa Kombe la Dunia 2022 akiwa na uzi wa Argentina, Angel Di Maria, 37, wiki hii ameaga rasmi Benfica ikiwa ni mwezi mmoja tangu kurejea katika klabu yake ya zamani huko kwao, Rosario Central iliyobeba historia yake kubwa.
Moja ya kumbukumbu nzuri za Di Maria kuhusu Rosario, siyo soka tu, bali ni alipokuwa akiichezea klabu hiyo kabla ya kutimkia Ulaya, ndipo alipokutana na mkewe Jorgelina Cardoso, 43, ambaye pia ni wakala wa michezo.
“Habari Benfiquistas, imemalizika awamu ya pili ya maisha yangu ya soka katika klabu ambayo imenipa kila kitu tangu siku ya kwanza nilipowasili hadi leo. Zimekuwa awamu mbili nzuri sana katika maisha yangu.” Di Maria aliandika mtandaoni Jumatatu hii na kuongeza.
“Nilipowasili hapa, sikujua nini kingeweza kutokea katika taaluma yangu na leo ninaondoka nikiwa na familia yenye furaha sana. Tumefurahia kuishi katika jiji zuri (Lisbon, Ureno) na nchi ambayo imenikumbatia tangu siku ya kwanza,” alisema Di Maria.
Ikumbukwe Di Maria amejiunga na Benfica mara mbili, awali ni mwaka 2007 hadi 2010 akitokea Rosario Central, kisha 2023 hadi 2025 akitokea Juventus na sasa amerejea kule alipoanzia, yaani Rosario baada ya kusaini mwishoni mwa Mei.
Kipindi Di Maria akiwa na Rosario, klabu aliyoichezea awali kati ya mwaka 2005 hadi 2007, aliwavutia mashabiki wengi na mmoja wapo ni mrembo wa Kiargentina, Jorgelina Cardoso ambaye baadaye alikuja kuwa wapenzi kisha wakafunga ndoa.
Akizungumza na kipindi cha Angel Responde huko Argentina, Jorgelina alisema alimtafuta Di Maria mtandaoni baada ya kuvutiwa na kipaji chake na huo ukawa mwanzo wa uhusiano uliobeba historia na kumbukukumbu nyingi za maisha.
“Tulikutana kupitia mtandao, kwa sababu nilikuwa shabiki mkubwa wa soka, timu yangu ni Rosario Central na nilikuwa nafuatilia kila mechi. Nilihudhuria uwanjani, yeye alikuwa anacheza huko na nikamwandikia ujumbe (DM) kama shabiki tu,” alisema Jorgelina.
Di Maria anayejulikana kwa jina la utani kama ‘Fideo’ ambalo lina maana ya ‘tambi’ kwa Kihispania, kutokana na kuwa mwembamba, tangu wakati huo, Jorgelina amekuwa mtetezi na mfariji wake mkubwa kwenye nyakati za furaha na huzuni katika soka.
Jorgelina alizaliwa Julai 11, 1982 mjini Rosario, Argentina - mji huo huo alikozaliwa Di Maria. Wawili hao ni mashabiki wakubwa wa klabu ya Rosario Central, na walifunga ndoa Julai 30, 2011 katika mji wao wa nyumbani.
Kwa mujibu wa SoccerSouls, mtoto wao wa kwanza, Mia alizaliwa kabla ya wakati (mtoto njiti) mwaka 2013, hivyo Jorgelina alilazimika kukaa hospitalini huko Madrid, Hispania kwa miezi sita na baadaye walijaliwa mtoto mwingine, Pia hapo 2017.
Wakati Mia anazalizwa, Di Maria alikuwa akiichezea Real Madrid kabla ya kuuzwa kwenda Manchester United mwaka 2014 kwa dau la Euro63 milioni ambalo lilikuwa rekodi katika Ligi Kuu England (EPL) wakati huo.
Licha ya kusaini mkataba wa miaka mitano na kupewa jezi namba 7 ambayo ilishavaliwa na wakali kama Cristiano Ronaldo, George Best, Eric Cantona na David Beckham, mambo hayakwenda vizuri kwa Di Maria, kitu kilichomfanya Jorgelina kutema nyongo!.
“Kwa kweli, hatukuwa na furaha. Mwanzoni mambo yalikuwa shwari, lakini baadaye yakaanza kuwa magumu. Maisha ya Uingereza ni magumu kidogo, hasa kwa watu wa Amerika Kusini. Wapo wanaofurahia, lakini wapo wanaoshindwa kabisa kuzoea.” alisema.
“Sikuwa na uhusiano mzuri na kocha wa Man United wakati huo (Louis van Gaal), hivyo nadhani uamuzi wa Di Maria kujiunga na Paris Saint-Germain (PSG) baada ya msimu mmoja, ulikuwa sahihi,” Jorgelina alisisitiza.
Katika mahojiano mengine na televisheni ya LAM, Jorgelina alisema awali baada ya Di Maria kumjulisha kuhusu ofa ya Man United, hakusita kusema ukweli wake kuwa hajapenda mpango huo wa kuhamia Uingereza.
“Siku moja aliniletea ofa hiyo ila sikuipenda, nilimwambia aende peke yake. Ilikuwa fedha nyingi, zaidi ya ile ambayo Wahispania walikuwa wameofa. Kwa hiyo tukaamua kwenda, kama unavyofanya kazi ofisini na mtu akikuahidi mshahara mara mbili, unafuata.”
“Tulikuwa marafiki kama Gianinna Maradona na mke wa Sergio Aguero na tuliwahi kwenda Manchester, kusema kweli sikupapenda. Tuliporudi nyumbani nilimwambia; ‘Kama utahama, hakikisha ni popote duniani isipokuwa Uingereza,” alisema Jorgelina.
Ni kama Jorgelina aliona kitu mbele maana miezi 11 baada ya Di Maria kuitumikia Man United, aliuzwa kwenda PSG kwa ada ya Euro 50 milioni kwa kile kilichotajwa kama mpango wa Louis van Gaal wa kubana matumizi!.
Kuhusu Di Maria kustaafu kuichezea timu ya taifa baada ya kutwaa ubingwa wa Copa America 2024, Jorgelina alisema alimshawishi asifanye hivyo lakini alishikilia msimamo wake.
“Mwanzoni nilimwambia hawezi kustaafu sasa na yuko katika kiwango chake bora na watu wanampenda. Lakini alijibu; Hapana, nataka kuondoka nikiwa vizuri’. Hataki kurudia hali ya awali na hakuitwa kikosini.”
“Kando na hayo, anajua wachezaji chipukizi wanakuja kwa kasi na huu ni wakati mwafaka kwake kuachia ngazi ili kuwapisha, hivyo naweza kusema ulikuwa ni uamuzi wa busara,” alisema Jorgelina.
Licha ya kukumbana na ukosoaji mkali, Jorgelina amekuwa mstari wa mbele kumtetea mume wake, mara nyingi akitumia mitandao ya kijamii kumuunga mkono. Uaminifu na uthubutu wake vimekuwa salaha muhimu kwa Di Maria kuvuka changamoto za maisha ya soka.