Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Banza Stone: Miaka 20, sauti ileile

Muktasari:

  • Wanamuziki wengi wanatunga zaidi nyimbo za mapenzi na kusahau kero za jamii. Hali ni tofauti kwa mwanamuziki Ramadhan Masanja maarufu Banza Stone ambaye baadhi ya nyimbo zake zinaendelea kutamba katika muziki wa dansi nchini.

MWANAMUZIKI aliyekamilika ni yule anayeimba katika sauti yake kwa muda mrefu na  anayetunga nyimbo zinazodumu muda mrefu katika jamii.

Muziki ni kipaji, lakini vijana wengi huingia katika sanaa hiyo kwa kufuata fedha na umaarufu matokeo yake huishia kutunga nyimbo zinazoelezea mapenzi kila kukicha na kusahau mambo ya kijamii.

Bado Tanzania ina matatizo mbalimbali ikiwamo ufisadi, umaskini, elimu duni na ukosefu wa huduma mbalimbali za jamii.

Wanamuziki wengi wanatunga zaidi nyimbo za mapenzi na kusahau kero za jamii. Hali ni tofauti kwa mwanamuziki Ramadhan Masanja maarufu Banza Stone ambaye baadhi ya nyimbo zake zinaendelea kutamba katika muziki wa dansi nchini.

Mtu Pesa, Angurumapo Simba, Mtaji wa Maskini, Elimu ya Mjinga ni baadhi tu ya nyimbo za Banza alizoimba katika bendi tofauti za African Stars ‘Twanga Pepeta’ na TOT Plus, lakini hadi leo zinaweza kutumika  katika matukio tofauti tofauti katika jamii.

Tungo za Big G

Katika mahojano na Mwanaspoti, Banza anasema tungo nyingi za wanamuziki vijana zinaelemea katika mapenzi na kusahau mambo mengi katika jamii, hivyo hawawatendei haki wananchi.

“Muziki wa dansi unakua na kushuka kutokana na tungo nyingi kuwa za muda mfupi, watu wanatunga nyimbo laini sana kila mmoja anaimba mapenzi na kusahau mambo mengine katika jamii.

“Mimi naita tungo za Big G, yaani unasikiliza kidogo tu utamu unaisha ni kama unavyotafuna Big G.

Hakuna anayeumiza kichwa katika kuhakikisha zinapatikana nyimbo zenye ujumbe wa maana kwa jamii,” anasema Banza anayemudu kupiga gitaa, tumba na dramu.

Banza ambaye sasa anafanya shughuli zake za muziki katika Bendi ya Extra Bongo, alianza harakati za muziki miaka ya 1990 wakati huo akisoma elimu ya dini ya Kiislamu katika madrasa.

“Nilikuwa mwimbaji mzuri wa kaswida na pia nimesoma kwa kiasi elimu ya dini, lakini nikaanza kujiingiza taratibu katika muziki wa dunia kwa kucheza disko katika kumbi mbalimbali.

“Nilipewa jina Banza Mchafu kutokana na mitindo yangu ya uchezaji kuwa ya kusisimua watu na sikuwa najali nitakuwaje zaidi ya kila siku kubuni aina za mitindo hiyo. Wazazi wangu mwanzo walichukia kuona naacha mambo ya dini naenda kufanya mambo ya muziki wa kidunia, ila baadaye walinielewa,” anasema Banza.

Baada ya kujishughulisha na kucheza disko, Banza aliingia katika muziki wa dansi katikati ya miaka ya 1990 akiwa na Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, lakini nyota yake iling’ara zaidi mwaka 1999 baada ya bendi hiyo kutoa kibao cha Kisa cha Mpemba.

“Kwa kweli hapo ndipo mapinduzi ya muziki wa dansi yalipofanyika na watu wakaanza kutufuatilia, tulikuwa na mtindo wa Twanga Pepeta ambao mimi niliuanzisha na hadi leo natembea kifua mbele na si wa bendi kwani haujasajiliwa popote.

“Naweza kuutumia mtindo huo popote nitakapoimba na hakuna mtu anayeweza kunizuia, japokuwa siwezi kuwakataza wengine kutumia,” anasema Banza.

Tabia za kuhamahama

Wanamuziki wengi wana tabia za kuhamahama katika bendi na Banzastone ni mmoja wao, amewahi kufanya kazi na bendi za Twanga Pepeta, TOT Plus, Bambino na sasa Extra Bongo. Aliwahi kurejea Twanga Pepeta na kuondoka tena.

“Tunahama kufuata masilahi lakini wapo wengine hizo ni hulka zao tu, masilahi ya muziki ni madogo mno sasa ukipata nafasi ya kuitwa sehemu yenye fedha unaenda wala hakuna tatizo.

“Mambo ya uongozi katika bendi pia huchangia wanamuziki kuhama hata kama watalipwa vizuri, maana watu wengi ambao si wanamuziki wanapoanzisha bendi huwa hawawezi uongozi na kumuongoza mwanamuziki unatakiwa uujue muziki kwanza,” anasema Banza.

Akizungumzia kuhusu wingi wa wanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Banza anasema wengi wao hawana jipya katika muziki lakini wapo wanaofanya vizuri na kuongeza changamoto katika muziki wa dansi.

Banza na Mafahari Watatu

Banza ni miongoni mwa wanamuziki watatu wa muziki wa dansi wanaounda kundi lisilo rasmi la Mafahari Watatu, wengine ni Mwinjuma Muumin na Ali Choki.

Kundi hilo kwa sasa lipo jikoni kupika albamu yake ambayo itakuwa na nyimbo sita huku kila mwanamuziki atakuwa na nyimbo mbili ndani yake.

“Sisi ni kama ndugu katika muziki, tumeona ni vyema tukaungana kufanya kazi ya pamoja kwa muda mfupi ili mashabiki wetu wapate kitu kizuri kutoka kwetu, nadhani ni wazo zuri na tutafanikiwa,” anasema Banza.

Japokuwa wapo katika mkakati wa kuzindua albamu ya Mafahari Watatu, Banza anasema bado anapiga mzigo na bendi ya Extra Bongo lakini hana mkataba na ‘wanamalizana kishkaji’ na Choki ambaye ni mkurugenzi wa bendi hiyo. Mwanamuziki huyu anasisitiza bendi yake ya Bambino Sound bado ipo isipokuwa kwa sasa mambo hayajakaa vizuri. “Bambino ni bendi yangu na haijafa isipokuwa kuna mambo hayajakaa vizuri, haikuwa na uongozi mzuri kwa ngazi nyingine lakini muda wowote itarudi.”

Muziki na uhuni

Jamii inaamini idadi kubwa ya wanamuziki wanajihusisha na vitendo vya kihuni kutokana na umaarufu na kupata fursa ya kukutana na watu wengi, lakini Banza anapingana na hilo.

“Si kweli kwamba wanamuziki ni wahuni, uhuni ni tabia ya mtu tangu awali isipokuwa anakuwa hajapata mahali pa kuonyesha tabia hiyo sasa anapokuja katika muziki anafungua makucha.

“Wapo wanamuziki wengi si wahuni na hadi leo wana heshima zao, hii ni kazi kama zilivyo kazi nyingine tatizo tunafuatiliwa sana na vyombo vya habari kutokana na aina ya kazi yetu,” anasema Banza.

Anasema hata katika kazi nyingine uhuni unafanyika kwa nafasi kubwa lakini wanamuziki wanafuatiliwa kwa kuwa ndilo kundi linalowakusanya watu wengi katika jamii.

Banza bado analia na masilahi ya wanamuziki na anaweka wazi kuwa akipata bahati ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete atamsisitizia kuweka mkazo katika kuhakikisha haki za wasanii haziibiwi.

“Nikipata bahati ya kukutana na Rais, neno langu litakuwa moja tu, asimamie haki zetu, watu wanatuibia kupita kiasi na matokeo yake wengi tunakufa masikini, tunabaki na umaarufu.

Sauti ya Banza

Sauti ya Banza ni maarufu miongoni mwa mashabiki wa muziki wa dansi, hawahitaji kuambiwa pindi wanapomsikia iwe ni jukwaani au kwenye redio, ni rahisi kuitambua sauti hiyo ambaye haijabadilika miaka nenda rudi.

Banza ambaye ni baba wa mtoto mmoja anasema kutobadilika kwa sauti yake ni mambo ya kiasili kwani huwa hafuati miiko ya kutunza sauti ikiwamo kutokunywa maji baridi na mengineyo.

“Sauti yangu ni ya asili, sifuati masharti yoyote ya kuitunza. Lakini sipendi kuona mwanamuziki ambaye hatumii sauti yake,” anasema Banza.

Na ingawa kwa sasa anafanya kazi Extra Bongo, Banza bado anasisitiza kwamba hajafika katika bendi hiyo kwani anaweza kwenda kufanya muziki na bendi yoyote nchini hata Twanga Pepeta kama watakubaliana katika masilahi.

Akizungumzia mafanikio yake katika muziki anasema miongoni mwa mafanikio hayo ni kutembea katika nchi kadhaa duniani zikiwamo Ubelgiji, Sweden na Muscat.