AY kulala kwenye kontena hadi heshima ya Bongo Fleva

LEO Jiji la Dar es Salaam linaweza likasimama Ghafla, hata ikiwezekana mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali zikasita kwa muda kupisha Tamasha la Bongo Fleva Honors lililoingia msimu wa pili sasa.

Anayepamba tamasha hilo si mwingine ni Ambwene Yesaya ‘AY’ na mwenyewe anasema amewaandalia sapraizi mashabiki wake. Ni ipi hiyo, kwenye Ukumbi wa Ware House, Osterbay.

Akizungumzia shoo hiyo inayohusisha wasanii wakongwe wa Bongo Fleva, AY anasema itakuwa ni ya tofauti.


PUMZI KAMA YOTE LEO

AY anasema amejiandaa kufanya laivu shoo, ambayo mashabiki wataamua aimbe nyimbo ngapi, kwani hata 30 wakitaka ataimba. Unakosaje kwa mfano.

“Nimekuwa nikifanya kazi na wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi tangu mwaka 2000 hadi sasa (2024), hivyo miongoni mwa niliofanya nao kazi watakuwepo siku hiyo na itakuwa na sapraizi kwa mashabiki wangu na wa Bongo Fleva Honors.”


KWENYE KONTENA HADI MZEE WA COMMERCIAL

Hata hivyo, AY hajafika alikofika kwa bahati mbaya. Mengi amepitia. Unajua alishawahi kulala kwenye kontena. Kuoga mabafu ya jumuia. Alikotokea je? Huyu hapa ndiye AY, Mzee wa Commercial’.

Aliingia jijini Dar es Salaam mwaka 1999 akitokea Mbeya alikozaliwa (Julai 5, 1982 ndiyo aliingia duniani), akakulia Dodoma na Dar es Salaam ikamtambua ikampa makazi.

Anasema aliyemsukuma kuingia Dar ni ndugu yake Gzingalize waliyesoma naye Shule ya Sekondari ya Ifunda Technical, Iringa.

Kutokana na kipaji chake cha muziki, ndoto yake ilikuwa kufika Dar na hata alipoambiwa kulala ni kwenye kontena, ilimradi liko Dar, hakuona tabu na ndipo ndoto yake ikaanzia hapo.

Kontena hilo lilikuwa linatumiwa na mafundi wa kushona nguo. Hivyo kila siku ilimlazimu kuamka saa 12 asubuhi kabla Mafundi hawajafika ili kuwapisha na kwenda hadi Mnazi Mmoja kwa ajili ya kuoga kwenye mabafu ya jumuiya ya kulipia.

Baada ya kulala kwenye kontena kwa muda, alihamia kwenye nyumba ya kina Gzingalize, kabla ya kukutana na msanii mwenzake waliokuwa pamoja kwenye kundi la East Coast Team, Gwamaka Kaihula ‘King Crazy GK’.

Aliendelea kujitafuta na ndoto yake ilianza kuonekana pale tu alipokutana na mtayarishaji wa muziki P-Funk Majani na baada ya kumchania mistari safari yake ikaanza rasmi kwenye muziki na ngoma ya kwanza kumtambulisha ikawa ni ‘Raha Tu’.

AY alisifika kwa staili yake ya kuchana na ilimtambulisha kwenye gemu kwa kishindo mwaka 2001.

Baadhi ya ngoma alizozidi kumpaisha ni Miiko 10 ya Rap aliyoimba na GK, Biashara ya Utumwa ikishirikishwa na Sir Juma Nature, achana na zile zake kama Raha Tu Remix akiwa na marehemu Complex, AY ametoa nyimbo nyingi maarufu nchini Tanzania, Raha Kamili, Machoni kama watu, Binadamu, Yule, Zigo,


Ameshirikiana na wasanii wengi wa ndani na nje ya nchi kama Juma Nature, Lady Jaydee, Complex, Sean Kingston, P Square, Jose Chameleone, Ms Trinity, Nyashinski, Victoria Kimani, Wahu, Marco Chali, Avril na wengine wengi.


HAKUKATA TAMAA

Si mtu wa kukata tamaa licha ya pandashuka kipindi anaanza muziki na biashara haikuwa nzuri na mikataba ilikuwa mibovu tofauti na sasa.

Anamiliki albamu kama Raha kamili ya 2003, Hisia zangu 2005 na Habari Ndio Hiyo ya mwaka 2007 aliyoshirikiana na Mwana FA. Ana mke na mmtoto wa kiume na alimuoa Remmy raia wa Rwanda mwaka 2018.


AISHIKA BONGO FLAVA

wengi wanajaribu na kushindwa kwa sababu ya uoga, lakini kwa AY hakuwa anajaribu, bali anafanya na ndio maana ilikuwa rahisi sana kwake kwenda hadi nje ya nchi kujitambulisha huko, mbali na muziki wake kuchezwa huko kabla.

Kama hujui tu, ndiye msanii wa kwanza kutoa video nje ya Tanzania na alitoa alitoa wimbo wake wa Leo pamoja na Ogopa Djz wa Kenya mwaka 2009.

Pia ni msanii wa kwanza Tanzania kufanya kazi na mtayarishaji mkubwa wa video Afrika Kusini Godfather na wa kwanza kufanya kolabo na wa wasanii wa nje kama P Square, Miss Trinity na Sean Kingston.

Kama haitoshi, AY ndiye msanii wa kwanza kushiriki na kushinda tuzo za nje ya nchi na aliwahi kushinda tuzo ya video bora ya mwaka na msanii bora wa mwaka Afrika na wimbo bora, tuzo za Channel O.

TUZO ZA KUTOSHA

Mwaka 2007 alishinda Tanzania Music Awards - Best Hip Hop kwa wimbo wake wa ‘Usijaribu’ na Kisima Music Awards akishinda tuzo ya video bora kutoka Tanzania kwa wimbo huo huo.

Mwaka 2008 alishinda tuzo ya Tanzania Music Awards kwa wimbo wa kushirikiana alioimba na Mwana FA ‘Habari Ndio Hiyo’. Pia alishinda tuzo ya Msanii bora wa kiume kutoka Tanzania, tuzo za Pearl of Africa Music Awards.

Mwaka 2010 kwenye tuzo za Tanzania music awards, alishinda tuzo ya Wimbo bora wa miondoko ya Reggae wa ‘Leo remix’ alioumba na Wahu na nyingine nyingi.

MSIKIE SUGU

Bongo Flava Honors ni tamasha la kuwapa heshima wasanii wakongwe wa Bongo Flava nchini ambalo linafahamika kama Bongo Flava Honors Concert na leo Aprili 26, 2024 ni zamu yake baada ya wasanii kibao kupanda tangu liasisiwe mwaka jana na mratibu wake Joseph Mbilinyi (Mr Two ‘Sugu’).

Sugu anasema tamasha hilo lengo lake ni kuwaenzi wasanii walio hai na walioifanyia makubwa Bongo Flava na kuipa mafanikio na linafanyika kwa msimu wa pili na kila baada ya miezi mitatu tofauti na msimu wa kwanza lilifanyika kila mwezi, ili kuwapa nafasi wasanii/msanii atakayepafomu kujiandaa kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya wasanii ambao walianza msimu wa kwanza ni Dully Sykes, TID, Juma Nature, Jay Mo, Mr Blue, Gangwe Mob, Wagosi wa Kaya na Banana Zoro, huku msimu wa pili walioanza ni Mr Nice, Matonya na sasa ni zamu ya  AY.