ASHA BOKO: Kilo 130 ndizo zimenipa maisha

Muktasari:
- Ni mmoja wa waigizaji waliojizolea sifa kwenye tasnia ya Bongo Movie hasa kutokana na aina yake ya uigizaji na mwonekano wake.
TATU Yusuf. Ukitaji jina hilo sio wengi wanalifahamu, lakini unapotaja Asha Boko, hakuna asiyelifahamu na mhusika wa jina hilo.
Ni mmoja wa waigizaji waliojizolea sifa kwenye tasnia ya Bongo Movie hasa kutokana na aina yake ya uigizaji na mwonekano wake.
Ukilitaja tu jina lake Asha Boko, picha itakujia mwanadada mwenye umbo kubwa na mnene. Ndiye huyo Asha Boko na mwenyewe anasema, anajivunia umbo lake kwani ndilo limemtoa kwenye tasnia ya Bongo Movie hasa kwenye tasnia ya vichekesho.
Ukweli ni kwamba, mwanadada huyu hawezi kuchuja. Ni kwa sababu ya kipaji chake na anavyotumia umbo lake anapovaa uhusika. Hakika atakuvunja mbavu kwa vichekesho.
Mwanaspoti lilifunga safari hadi maskani yake, Goba jijini Dar es Salaam na amefunguka mengi kuhusu maisha yake na sanaa kwa jumla. Ametamba na filamu nyingi kama Mgeni wa Kijiji, Namtoa Mwanangu Suna, Mama Shughuli, Gusa Unase, Nani Chizi na nyingine nyingi.
Mwanaspoti: (likibisha hodi kwa Asha Boko)
Asha Boko: Karibuni. (Mwanaspoti linakaribishwa kwa nyota huyo anayeonekana mchangamfu na kuanza mahojiano.
Mwanaspoti: (Baada ya kuketi na kumtazama Asha Boko) Kwanza tungependa kujua una kilo ngapi?
Asha Boko: Nina kilo 130 hizi ndio mara ya mwisho kupima, hapa nafanya mapambano ya kupungua ili tu mwili uwe mwepesi.

Mwanaspoti: Vipi mwili haukupi kero yeyote?
Asha Boko: Sipati kero yeyote kwa sababu huu mwili wangu ndio ‘Character’ yangu japo ukizidi sana sio mzuri.
Mwanaspoti: Mbona uko kimya muda hujaonekana kwenye kazi mpya ya sanaa?
Asha Boko: Kweli kwenye kutoa kazi mpya nipo kimya japo nipo kwenye maandalizi, nikimaliza nitawajulisha, ila sasa hivi nipo kwenye Tamthilia ya ‘Nuru’.
Mwanaspoti: Asha Boko ni mtu wa aina gani?
Asha Boko: Ni mtu wa watu ambaye anapenda kuishi na watu vizuri, anapenda kukosolewa pale anapokosea.
Mwanaspoti: Tangu umeanza kazi yako ya sanaa, ni changamoto gani umezipata?
Asha Boko: Changamoto zipo nyingi tu, mojawapo unaweza kupatana pesa na mtu ukafanye naye kazi, akakupa ‘Advance’ halafu baadaye mkimaliza anakukimbia location na kukuzimia simu hakumalizii pesa ya malipo.
Mwanaspoti: Kazi ya sanaa imekupa mafanikio gani?
Asha Boko: Namshukuru Mungu nimejenga, pia nimepata umaarufu wa kujulikana na watu wengi hata mtoto mdogo ukimwambia akuelezee Asha Boko anakwambia.

Mwanaspoti: Ni mwigizaji gani aliyekuvutia hadi ukaamua kuingia kwenye uigizaji?
Asha Boko: Ni Mzee Majuto ambaye ni marehemu kwa sasa, nilikuwa nampenda sana na kufuatilia jinsi anavyoigiza. Alikuwa ananivutia kiasi cha kuamua kuanza kuigiza.
Mwanaspoti: Nani aliyekutambulisha kwenye ulimwengu sanaa?
Asha Boko: Muhogo Mchungu ndiye aliyeniingiza kwenye sanaa, alinipeleka Kaole kipindi hicho alikuwa anatengeneza kazi yake ya Tamthilia yake ‘Miss Taswira’ hapo ndipo nikaanza kuonekana.
Mwanaspoti: Muhogo Mchungu haigizi vichekesho, aliwezaje kukutambulisha kwenye fani yako ya uchekeshaji?
Asha Boko: Mimi nilienda Kaole Sanaa Group kama sio mchekeshaji, ila nilijigundua ni mchekeshaji baada ya kila nikiongea maneno watu wanacheka sana, hapo nikasema mimi sanaa naiweza, sasa siku moja nikaenda Magomeni nikakutana na dada mmoja anaitwa Bi Khajida akaniambia hakuna shida Kaole kuna kiingilio, ukifila pale utakutana na Mzee Pwagu na Mzee Kipara ambao sasa ni marehemu.
Basi nikaenda kulipa na kujiunga, nikapata marafiki Bi Mwenda, Bi Khadija, wakawa wananielekeza mbinu za sanaa, sasa ilipoanzishwa hii Miss Taswira ndio nikaonekana mimi sipo kwenye sanaa ya siriaz nipo kwenye vichekesho, mwishowe Pembe na Senga wakasema niwekwe kwenye uchekeshaji maana ndiyo wameona nafaa ndio hadi leo naendelea na sanaa ya uchekeshaji.
Mwanaspoti: Hivi kitambaa cha nguo huwa unashona mita ngapi?
Asha Boko: Mimi nashona mita tatu na sina mshono wa mbwembwe zaidi ya madera au magauni marefu.
Mwanaspoti: Kwa upande wa chakula huwa unakula kiasi gani?
Asha Boko: Iwe wali au ugali nakula nusu kilo, kama chai kikombe kimoja na chapati mbili.
Mwanaspoti: Umeolewa?
Asha Boko: Ndio nimeolewa, hii ndoa yangu ya pili, mume wangu wa kwanza hatukuachana na tulibahatika kupata watoto wawili na wakati tunakaa Kimara tulivamiwa na majambazi na alipigwa risasi na kupoteza maisha, nilikaa miaka 14 ndipo nimekuja kuolewa tena.
Mwanaspoti: Vipi unatarajia kuongeza mtoto mwingine?
Asha Boko: Mmh na uzee huu si nitafia leba jamani? (Kicheko) ila mtoto ni mpango wa Mungu ikitokea nitazaa maana kutoa ni dhambi.
Mwanaspoti: Unashabikia timu gani hapa nchini na unamkubali mchezaji gani?
Asha Boko: Mimi ni shabiki wa Yanga na mchezaji ninayemkubali ni Azizi KI, huyu ndiye namba moja kwangu wengine wanafuata.
Mwanaspoti: Unazungumziaje usajili wa kiungo mshambuliaji, Clatous Chama kuhamia Yanga?
Asha Boko: Nashangazwa na baadhi ya mashabiki wa simba wanamsema vibaya Chama, amekwisha kwenye uchezaji, haya yote ni maneno ya mkosaji kama vile mwanamume akimuoa mwanamke wakija kuachana anatoa mapungufu yake.
Mashabiki wa Yanga tumempokea Chama kwa mikono miwili na tuna imani atatufurahisha kwa kufanya vizuri.