Alikiba, Harmonize jukwaa moja Dar

Alikiba, Harmonize jukwaa moja Dar

Dar es Salaam. Wasanii Ally Saleh'Alikiba' na Rajabu Abdil maarufu 'Harmonize' ni miongoni mwa wasanii watakaokuwepo katika tamasha la kufunga mwaka lililopewa jina la 'Xtra Uni Bash 2021'.

 Akizungumza leo Jumatano Desemba 8,2021 Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Pancras Mayala ‘Askofu TZA’, amesema tamasha hilo litafanyika Desemba 11 hoteli ya Jangwani Sea Breeze.

Askofu TZA amesema katika tamasha hilo  wasanii zaidi ya 30 watakuwepo, ukiachia mbali Alikiba na Harmonize, atakuwepo Marioo, Kings Music, Konde Gang, Maua Sama, Sholo Mwamba, Ben Pol, Billnass, Young D, Weusi, Mabantu na wengine wengi.

 "Katika tamasha hili pamoja na mambo mengine wanavyuo watapata nafasi ya kwenda  kufurahi na wanavyuo wenzao lakini watapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao mbele ya wasanii wakubwa watakaokuwepo siku hiyo.

"Aidha tamasha hili ni muendelezo wa ratiba za kipindi cha XXL kufanya kila mwezi Desemba ambapo kwa mwaka huu kabla ya kufanyika Dar tulifanikiwa kupita vyuo kadhaa mikoani ikiwemo CBE Dodoma, Saut na CBE campas ya Mwanza,"amesema Askofu TZA.

Kiingilio cha tamasha hilo kitakuwa Sh9000 kwa kupitia  Nilipe App  na mlangoni ni Sh10,000.

Tamasha hilo limedhaminiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Dstv, Kilimanjaro Premium Lager, COSOTA Tanzania, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Precision Air na Nilipe App.