Albamu ya Dogo Janja kuchochea usawa wa 50/50 kuelekea 2030

Sunday May 30 2021
janja pic
By Mwandishi Wetu

Msanii wa Bongofleva, Dogo Janja ameachia albamu yake ya pili iitwayo ‘Asante Mama’ ambayo ni sawa na mpango wa kuelekea kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika nyanja zote ifikapo mwaka 2030 kama ilivyobainishwa na Umoja wa Mataifa.

Kwa zaidi ya karne moja sasa, dunia imekuwa ikiadhimisha siku ya wanawake duniani ili kuweka usawa wa kijinsia kwa mustakabali bora wa hali ya mwanamke kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Dogo Janja ametoa albamu hii yenye nyimbo 11 kwa ajili ya kumshukuru mama yake na wanawake wote duniani na ndio sababu amewashirikisha wasanii wa kike kwa asilimia 90, yaani ni wimbo mmoja tu ndio hajamshirikisha mwanamke.

Wasanii wa kike walioshirikishwa ni Lady Jaydee, Maua Sama, Mimi Mars, Khadija Kopa, Rosa Ree, Nandy, Linah Sanga, Patricia Hillary na Lulu Diva. Lengo la kufanya hivi ni kuonyesha kuwa wanawake wanaweza na kutoa motisha kwa wengine kutoa nafasi kwa wanawake katika nyanya mbalimbali.

Dogo Janja anakuwa msanii wa kwanza wa Bongofleva kufanya kitu kama hicho miongoni mwa waliowahi kutoa albamu kwa mwaka huu, ambao ni Rayvanny, Lady Jaydee, Mbosso na Weusi.

Moja ya nyimbo ambazo Dogo Janja anajivunia katika albamu hiyo, unaitwao ‘Mayo’ ambao amemshirikisha gwiji wa muziki wa taarabu Afrika Mashariki, Patricia Hillary. Katika wimbo huo Janja anataka baadhi ya watu kuondoa fikra ya kumuona mama wa kambo kama mtu mbaya katika malezi.

Advertisement

“Mama wa kufikia ni mama, ubaya au uzuri wa mtu ni yeye mwenyewe hivyo tusiwavike wote ubaya, kwenye wimbo nimeeleza pendo la mama wa kufikia. Kwa heshima ya mama zetu naomba ukasikilize wimbo huo,” alisema msanii huyo kutoka mkoani Arusha.

Ikumbukwe albamu hiyo inakuja mara baada ya Dogo Janja kutimiza miaka 10 kwenye muziki ambayo ni sawa na siku 3,650 alizozitumia vizuri na kufanikiwa kurekodi nyimbo 421, na kufanya shoo 1,562.

Advertisement