24 waingia Bingwa msimu wa pili, kukaa wiki 11

Dar es Salaam. Vijana 24 wenye ushawishi mtandaoni rasmi wameingia kwenye kinyang'anyiro cha kumpata mshindi wa kipindi cha Bingwa msimu wa pili ambapo watakaa kwenye nyumba maalum kwa siku 72.

Msimamizi mkuu wa vipindi wa kituo cha luninga cha Tv3, Emmanuel Sikawa amesema kati yao 12 ni wanawake na wengine wanaume ambao watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali.

"Bingwa show imesaidia vijana mbalimbali katika masuala ya elimu, afya ya akili, kujitegemea na kutatua changamoto mbalimbali katika maisha yao ya kila siku," amesema Sikawa  na kuongeza

"Inawasaidia vijana hawa 24 kupata mitaji kuendeleza biashara zao, ndoto zao katika maisha,"

Sikawa amesema vijana hao ni watu wenye ushawishi kwenye mitandao na hivyo elimu ambayo wataipata itaweza kuwasaidia vijana wengine kuwa mfano wa mambo yanayofaa kwenye jamii.

“Kupitia Bingwa msimu huu washiriki watapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kama elimu ya ujasiriamali, elimu juu ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii,” amefafanua Sikawa

Sikawa amesema jumla ya vipindi 65 vitarushwa kuanzia Jumapili hadi Ijumaa kuanzia saa 4 usiku pia kutakuwa na kipindi cha nusu saa kikijulikana kama Bingwa highlight ambacho kitajumuisha matukio yote muhimu.

“Kutakuwa na kipindi cha mubashara (live) ambayo itakuwa ya mtoano itakuwa siku ya Ijumaa,” amesema Sikawa

Mkurugenzi wa masoko na maudhui Startimes Tanzania, David Malisa amesema mchakato wa kupata washiriki 24 ulianza na mchujo wa washiriki 100 ambayo imekuja hivi sasa imekuja na kauli mbiu ‘Najiamini kinoma’.

“Kwanza tumetengeneza ajira kwa vijana kuonyesha uwezo wao, pia kila mshiriki kila siku atakuwa anaingiza fedha kwa siku atakazokuwa anakaa ndani, na za ziada atapata kwa kushinda chalenji ambazo zinafanyika” amesema Malisa