K-Lynn: Mwanamsimbazi katika ‘game’ la Mariah, Madonna

K-Lynn: Mwanamsimbazi katika ‘game’ la Mariah, Madonna

MARA baada ya kukabidhi taji la Miss Tanzania aliloshinda mwaka 2000, K-Lynn aliamua kuchanga karata zake kwenye muziki wa Bongofleva ambapo aliweza kushirikiana na wasanii kama Mr. Blue, Bushoke, Jay Moe, Chid Benzi, Squeezer na wengineo.

Ni miaka zaidi ya 10 tangu ameachana na muziki, lakini nyimbo zake bado zinaendelea kuishi masikioni mwa mashabiki wake na wapenda burudani kwa ujumla. Bongo Music Facts inakudadavulia zaidi kuhusu K-Lyinn na muziki wake;


1. Wimbo wa kwanza kwa K-Lynn kurekodi na kuutoa unaitwa Nalia kwa Furaha ambao alimshirikisha Bushoke. Huo ndio ulimpatia umaarufu zaidi upande wa muziki.


2. K-Lynn alianza muziki mwaka 1997 katika bendi ya Tanzanite - aliimba hapo kama msanii na mmoja wa viongozi kwa kipindi cha takriban miaka miwili na nusu, ndipo akaibukia Miss Tanzania.


3. Wakati anaanza muziki ndoto yake ilikuwa ni kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiingereza kwa sababu aliamini hilo ndilo litamtambulisha duniani kwa haraka lakini soko la Bongofleva halikuruhusu hilo.


4. Wimbo wa mwisho kwa K-Lynn kuurekodi ni ndani ya studio za B’Hits Music Group na ulitoka mwaka 2011 na baada ya hapo akaachana na muziki wa Bongofleva.


5. Mwaka 2008 alichaguliwa kuwania tuzo za KTMA katika vipengele vya Msanii Bora wa Kike na ushindi ukaenda kwa Lady Jaydee, Wimbo Bora wa Kushirikiana (Crazy Over You) ushindi ukaenda kwa ngoma, Habari Ndio Hiyo ya Mwana FA na AY.


6. K-Lynn ni shabiki wa Simba SC hiyo ni sawa Mastaa wa Bongofleva kama Zuchu, Hamisa Mobetto, Mwana FA, Diamond Platnumz, Tundaman na Roma.


7. K-Lynn aliamua kuachana na muziki baada na kujikita upande wa ubunifu wa samani (Interior Design), fani hii ameisomea mtandaoni katika chuo kilichopo Uingereza kwa kipindi cha miaka mitatu.


8. Albamu zake zote mbili alizoachia katika maisha yake ya muziki zimebeba majina ya nyimbo zake maarufu ambazo ni; Nalia kwa Furaha (2004) na Crazzy Over You (2007).


9. Ndoto ya K-Lynn tangu akiwa mtoto ni kuwa mwimbaji, wasanii waliomvutia na siku moja kutamani kuwa kama wao ni Mariah Carey, Madonna na Whitney Houston, wote kutokea Marekani.


10. Ilichukua miaka zaidi ya 10 hadi mrembo mwingine mwenye taji la Miss Tanzania kuingia katika muziki baada ya K-Lynn, huyu ni Genevieve Emmanuel ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2010, aliachia wimbo wake wa kwanza, Nana, Januari 2017.