Hussein Jumbe (7) - apewa kesi ya Ukimwi

ILIPOISHIA

JANA kwenye mfululizo wa simulizi la gwiji wa muziki wa dansi nchini, Hussein Jumbe, tuliona alivyosimulia alivyonaswa kibao kisha kuingiliwa na nyoka nyumbani kwake, ambaye hakuwa anahangaika na wengine isipokuwa yeye tu. Leo tunaendelea kwa kuelezea msala alikuja kupewa juu ya ugonjwa wa Ukimwi...kivipi? Endelea naye...!


AZUSHISHIWA NGOMA

Jumbe anasema ghafla hali yake ilikuwa sio nzuri. Kila ilipokuwa ikifika jioni alikuwa akisumbuliwa na maradhi. Alikuwa akiumwa na kumfanya ashindwe kufanya kazi vizuri.

“Ilikuwa ikifika saa 10 jioni nahisi baridi, mara ikawa homa za jioni, nikawa nameza Panadol mara ikawa sio baridi tena bali maradhi yakahamia miguuni, kuanzia kwenye magoti kuja chini,” anasema.

Jumbe anasema swahiba wake, Meddy Mpakanjia aliwasiliana na Mama Ima akamwezesha kwa nauli na akarudi haraka. “Siku hadi siku hali yangu ya kiafya ilizidi kuwa tete, nikapelekwa hospitali nikapata tiba hali ikawa bado mbaya na ilipofika Oktoba 1999, maradhi ya miguu yakanikamata kisawasawa,” anakumbuka.

Akiwa katika hali hiyo, madai mazito yakasambaa mitaani kuwa mwanamuziki huyo alikuwa ameathirika na Ugonjwa wa Ukimwi. Anasema wana ndugu, mkewe na Mpakanjia wakiwa kwenye kikao cha kufanya maamuzi ya kupata ufumbuzi jinsi ya kumsaidia madai hayo yaliibuka tena kikaoni.

Mmoja kati ya ndugu zangu (jina tunalo) alisema kwenye kikao kwa kuwa mgonjwa ni mwanamuziki na mke wake ni mjamzito wasubiri mkewe atakapojifungua na jibu litapatikana.

“Unajua alichokuwa akimaanisha?” Jumbe alimuuliza mwandishi wa makala haya.

“Hapana,” alijibiwa.

“Sawa, kwa kuwa mke wangu alikuwa mjamzito, yeye alimaanisha atakapojifungua jibu litapatikana kwa ugonjwa huo kudhihirika wazi, ndivyo ilivyokuwa imani ya watu kipindi kile,” alifafanua Jumbe.

Jumbe anasema kikao hicho kilifanyika sebuleni wakati yeye akiwa chumbani kwake na alikuwa akiyasikia maneno yote yaliyokuwa yakizungumzwa na ndugu zake hao.

Mama Imma alikasirika kutokana na tuhuma za mumewe kuambiwa ameathirika akaingia chumbani kutaka kumuonyesha vyeti lakini Jumbe alimzuia.

“Nilimwambia utawaonyesha vyeti watu wangapi? Kunywa maji upunguze hasira,” anasema.

Mpakanjia, alimpeleka Jumbe Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kupimwa Ukimwi na majibu yakatoka kuwa hakuwa na ugonjwa huo. Hata hivyo, daktari akashauri mgonjwa abaki hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi. “Siku tatu nilizolazwa, usiku miguu ilikuwa inawaka moto, magotini ilikuwa mpaka niwekewe kitu kizito, ilikuwa ikifika saa sita usiku lazima niwekewe beseni lenye maji na barafu,” anasema Jumbe.

Anaongeza ilipofika hali hiyo alimwambia mke wake amletee vitabu vyake vitakatifu, Qur’an na Biblia. Anasema ni msomaji mzuri sana wa vitabu hivyo vitakatifu vya dini mbili tofauti, Uislamu na Ukristo. Madaktari waligundua alikuwa na taifodi, alimaliza dozi na kuruhusiwa lakini hali bado ilikuwa tete.

“Mpakanjia alinihamishia kwenye hospitali nyingine ya kulipia daktari mmoja mwenye asili ya Mkoa wa Kagera, alimshauri Meddy anipeleke upande wa pili,” anasema.

Jumbe anakumbuka kipindi hicho chote alikuwa akipata msaada kutoka kwa Mpakanjia, Abbas Abdallah (naye marehemu), Tony Karama (marehemu), Cosmas Chidumule, Ramadhani Mapesa na Hassani Kunyata.

Wengine ni Mwape Njilima ‘Hapendeki’ Shadrack, Kassim Rashid (marehemu) na Mustafa (John) Ngosha (marehemu). “Ilifikia hatua, Chidumule aliikuwa akiniombea kwa jina la Yesu. Mbali na hivyo nilitumia maji yaliyotoka kwa Mwamposa ili kutafuta njia ya kupata nafuu,” anasema.


AVUMISHIWA KUFA

Jumbe anasema siku moja akiwa amejilaza kitandani hali ikiwa haijatengemaa, ilipotimu saa saba mchana, Redio One katika matangazo ya vifo ilitangaza kifo cha mwanamuziki wa zamani wa Bendi ya Ochester Safasri Sound, Mobali Jumbe.

“Na hapa mtaani kwetu kulikuwa na mgonjwa amelazwa Hospitali ya Temeke naye alifariki dunia siku hiyo. Ilipotimu saa nane mchana, gari lililobeba mwili wa marehemu lilikuja mtaani kwetu, basi kwa matukio hayo na la mimi kuugua yalitosha kuamini nimefariki dunia,” anasema.

Anasema siku hiyo mkewe, Mama Ima akiwa anaendelea na shuguli zake uwani, ghafla aliwaona ndugu zake (wanawake) wakiingia wakiwa wanaangua vilio mikono yao ikiwa vichwani. “Mke wangu naye akawapokea kwa kilio, akajua kuna msiba umetokea kwao, wakaja hadi sebuleni, miye niko chumbani. Mke wangu alipowasikiliza kwa umakini akawasikia wakilitaja jina langu,” anasimulia Jumbe.

Jumbe anafafanua awali mkewe alikuwa anajua kuna kilio kimetokea nyumbani na hapo wamekuja kumpa taarifa. Lakini aliposhtuka aliposikia ndugu zake wakilia huku wakilitaja jina langu.

“Akashtuka na kuingia chumbani kuhakikisha kame kweli nimefariki dunia, aliingia huku akiwa ananyata kunifuata pale kitandani. Miye nilikuwa namuona, nikamwita… Mama Immaaa…!”