MKEKA WAKO : Samatta atapigwa nyumbani na Spurs ya Mourinho

Friday February 14 2020

samatta atapigwa nyumbani na Spurs ya Mourinho,staa wetu wa Tanzania, Mbwana Samatta,Kombe la Ligi,

 

By Samson Mfalila

ASTON Villa yenye staa wetu wa Tanzania, Mbwana Samatta pamoja na kuwa imefika fainali ya Kombe la Ligi lakini bado ipo taabani kwenye Ligi Kuu England.

Villa ipo kwenye nafasi za mkiani kwenye msimamo wa ligi ikizizidi kwa pointi moja tu timu zilizo katika hatari ya kushuka daraja.

Samatta na timu yake ya Villa wanaivaa Tottenham Hotspur kesho, ambayo inanolewa na kocha mwenye maneno mengi, Jose Mourinho.

Kiukweli Villa ina wakati mgumu kwenye Ligi Kuu England ikiwa imeshinda mechi tatu kati ya 12 ambazo imecheza katika siku za karibuni.

Katika siku za karibuni imekuwa na wakati mgumu kupata matokeo mazuri na jambo la kusitikisha zaidi imekuwa inaruhusu mabao katika kila mechi za karibuni.

Kwa mfano katika mechi 12 ilizocheza karibuni ni timu moja tu ya Norwich, ambayo haijafunga bao dhidi yao.

Advertisement

Katika mechi tano ambazo imecheza hivi karibuni ilijikuta ikifunga bao na wao wakiruhusu bao.

Ingawa Villa pia imejitutumua kwa kushinda mechi mbili kati ya tatu ambazo imecheza nyumbani karibuni.

Kiwango chao cha nyumbani ndio afadhali zaidi ikiwa karibuni imezifunga timu za Norwich na Watford.

Sasa safari hii inakutana na mziki tofauti wa Tottenham, ambayo kwa sasa inanolewa na Mourinho.

Kumbuka kuwa Mourinho ni mzuri sana kwa fomesheni yake ya kupaki basi na pia kusoma timu pinzani.

Ninavyofahamu Mourinho bila shaka atakuwa na `faili’ la uchezaji wa Samatta na kupachika bao kwenye mechi dhidi ya Bournemouth.

Samatta alifungua akaunti yake ya mabao ya Ligi Kuu ya England fasta kwenye mechi dhidi ya Bournemouth baada ya kujiunga na Villa.

Pamoja na kuwa timu yake ilifungwa lakini Samatta alimaliza mchezo huo akiwa na rekodi nzuri tu.

Alipiga bao katika mchezo na Bournemotuh lakini pia asilimia 67 ya mashuti yalilenga goli kwenye mechi hiyo.

Pia alipiga jumla ya pasi 16 kwenye mchezo huo na bila kusahau aliotea mara tatu kwenye mechi hiyo na Bournemouth.

Kumbuka na kuwa ndio ilikuwa mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England tangu atue timu hiyo akitokea Genk.

Sasa kutokana na Samatta alivyoonyesha cheche zake kwenye mechi na Bournemouth bila shaka Tottenham watamweka chini ya ulinzi mkali.

Villa sasa wanakabiliwa na kibarua kizito kwani wanavaana na Tottenham inayowania kuziba pengo lake na Chelsea.

Kiwango cha Tottenham cha ugenini sio kizuri wakiwa wameshinda mechi moja kati ya tano ambazo wamecheza hivi karibuni.

Timu hiyo ina rekodi mbovu sana msimu huu ikiwa imeshinda mechi mbili tu ugenini dhidi ya Wolves na West Ham.

Wakati Ligi Kuu England inaelekea kwenye lala salama imebakiza mechi saba za ugenini.

Tottenham bila shaka itaingia katika mchezo huu ikiweka nguvu katika kuhakikisha inazoa pointi za ugenini.

Kutokana na ukweli ushindai katika mchezo huu ndio utasaidia timu hiyo kwa kiasi kikubwa kutengeneza mazingira mazuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, Tottenham watajipa moyo wa kufanya kwenye mchezo huu kutokana na ukweli kuwa Villa ina beki dhaifu.

Kiuhalisia Samatta na Villa yake wana nafasi finyu kushinda mchezo huu wa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Villa Park na bila shaka Spurs wataibuka wababe kiulaini na kushinda 2-0.

Advertisement