TASWIRA YA MLANGABOY : Wabunge waisimamie Serikali kutenga bajeti ya timu za taifa

Friday April 3 2020

Wabunge waisimamie Serikali kutenga bajeti ya timu za taifa,Janga la corona,wadau wa michezo,mwanasport,

 

By Andrew Kingamkono

Waswahili wanausemi wao ulipata umaarufu sana hapa jijini Dar es Salaam ule unaosema ‘Dunia simama nishuke…’ kweli dunia imesimama nani wa kushuka nje kuna corona kila kona.

Dunia imesimama kweli kila sekta imeyumba kiuchumi, kijamii na sisi wadau wa michezo tumepigwa TKO baada ya ligi na mashindano mbalimbali yamesimamishwa kwa muda usiojuliana yote kwa sababu ya janga la corona.

Dunia bila ya michezo na burudani nini kitakupa furaha na kusahaulisha shida zako, pigo kwa sekta ya michezo na burudani kumesababisha ulimwengu kuwa sehemu ya ajabu.

Pamoja na yote ni lazima maisha yaendelea hakuna jinsi kwa sababu tunaamini kwa uweza wa Mungu hakuna ubishi kwamba janga hili litapita na kutuacha kwa amani na furaha yetu kama ilivyokuwa kabla ya corona.

Taswira wiki hii inataka kuangalia namna gani serikali na wadau wa michezo wanaweza kutumia kipindi hiki cha kusimama kwa michezo duniani na sisi tukajipanga upya.

Kwa sababu wahenga wanasema ‘kila shari ina heri yake’ naamini Serikali na vyama vya michezo kwa kushirikiana na BMT watakuwa na mpango thabiti wa kutumia fursa hiyo.

Advertisement

Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imefuzu kwa fainali za CHAN2020 zilizohairishwa, pia ipo katika kusaka kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 pamoja na Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon2021).

Pia, wanamichezo wetu wamefuzu kwa Olimpiki wenyewe michezo ya Tokyo2020 Olimpiki imesogezwa mbele hadi mwakani hivyo ni wakati mzuri kwao kupewa maandalizi sahihi zaidi.

Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika mashindano ya kimataifa iwe timu ya Taifa, wanamichezo wetu au klabu zinazotuwakilisha katika mashindano ya Afrika au hata haya ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia.

Zipo sababu nyingi za msingi ambazo zinasababisha michezo ya Tanzania kusuasua na kushindwa kuendelea kimataifa, lakini sababu kubwa ni ukosefu wa fedha na kukosekana kwa programu maalumu za kuendeleza michezo.

Nasema hivyo kwa sababu hebu jiulize swali hili, ipo wapi bajeti ya serikali kwa ajili ya timu za taifa tu, kama kweli tunataka kwenda kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, Kombe la Dunia, Michezo ya Afrika au Olimpiki?

Utaona jukumu hili la timu za taifa limeachwa kwa mashirikisho ambao hutegemea wadhamini tu na fedha wanazopewa na mashirikisho ya dunia kila mwaka, wakati siku zote ni timu ya taifa ni balozi wa nchi na maandalizi yake ya kufuzu mashindano makubwa ni mkakati wa kitaifa.

Tumeshuhudia nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikisaidia kuunga mkono vyama vyao vya michezo kwa kuzitengea bajeti timu za taifa kila mwaka na pia kutenga fedha za kusaidia programu mbalimbali katika nchi zao.

Kutokana na serikali za nchi hizo kuchangia nguvu katika kuendeleza michezo, nchi zao zimekuwa zikifanya vizuri na kupata maendeleo makubwa.

Kwa sababu michezo ni chanzo kikubwa kabisa cha mapato na unahitaji uwekezaji na programu bora ili kuweza kuwa na mafanikio yanayotarajiwa.

Nasema hivyo kwa sababu sasa bunge la bajeti ndio limeanza jijini Dodoma, pamoja na kipao mbele chake kuwa uchaguzi mkuu bado naamini kuna nafasi kwa wabunge wetu kuangalia namna wanavyoweza kusaidia bajeti kwa timu za taifa.

Naamini Wizara ya Michezo na serikali kwa ujumla watakuja na mpango wa kutenga fedha katika kila bajeti ya nchi kwa ajili kusaidia michezo na timu za taifa basi mapinduzi makubwa yatatokea nchini.

Ni wazi kuwa michezo nchini haiwezi kufanikiwa bila serikali kusaidia, ambapo serikali inaweza kusaidia mambo mengi, lakini mojawapo ni kusaidia fedha kwa sababu siku zote lazima uwekeze katika kumtengeneza bingwa kuliko kutegemea vipaji pekee.

Ukiangalia kwa undani nchi zote za Afrika zilizoendelea katika michezo kwa nanma moja au nyingine utakuta kuna nguvu nyingi za serikali za nchi hizo hasa hasa utagundua serikali za nchi zao hutoa fedha na kuboresha miundombinu ya michezo ili kuweza kuwa na programu nzuri za kuendeleza michezo na husaidia timu zao za taifa.

Naamini Spika Job Ndugai na Bunge lake waliona aibu iliyopata Taifa Stars katika fainali za Afcon2019 Misri nadhani sasa ni wakati wao wa kutekeleza kwa vitendo kwa kuhakikisha timu zetu za taifa zinatengewa bajeti kama inavyokuwa katika sekta nyingine.

Naamini Rais John Magufuli na serikali yake wataweza kutengewa bajeti ya timu ya taifa na bajeti ya kuendeleza michezo nchini ili kuongeza pato la Taifa.

Advertisement