MTAA WA KATI : Pep Guardiola msiba haukosi sababu

Muktasari:
Anfield ndicho kilichoonekana hicho. Lakini, Man City hii ya msimu huu, imepoteza kwa Norwich City ugenini. Ilipoteza pia nyumbani Etihad mbele ya Wolves, tena kwa kuruhusu wavu wake kuguswa mara mbili.
MSIBA haukosi sababu wanasema. Pep Gardiola ameondoka Anfield akiwa amepigwa na Jurgen Klopp, lakini bila shaka atamwangushia sababu Mwamuzi Michael Oliver, wasaidizi wake na VAR. Ndicho kinachoonekana kuwa sababu ya Man City kufungwa na Liverpool huko Anfield.
Lakini, ukweli ni kwamba Manchester City ilikwenda Anfield ikiwa imeshakufa. Ilishakufa siku nyingi. Ilikufa wakati ule Vincent Kompany alipoondoka na Guardiola akaweka jeuri ya kutosajili mbadala wake. Ikaja kufa wakati Aymeric Laporte alipoumia kwenye mechi ya Brighton mwezi Agosti.
Ikaja kumalizikia kabisa wiki iliyopita wakati kipa Ederson alipoumia na mwenzake David Silva. VAR na Mwamuzi Oliver vinabaki tu kutajwa kwa sababu msiba unapotokea huwa haukusi sababu.
Anfield ndicho kilichoonekana hicho. Lakini, Man City hii ya msimu huu, imepoteza kwa Norwich City ugenini. Ilipoteza pia nyumbani Etihad mbele ya Wolves, tena kwa kuruhusu wavu wake kuguswa mara mbili.
Hilo lilitosha kutoa ishara kwamba Man City ilikuwa na tatizo kubwa kabla hawajaenda kucheza na Liverpool, timu ambayo hakika imekuwa na kiwango bora kabisa pengine kuliko zote kwenye Ligi Kuu England.
Kwa ukuta wake wa kuungaunga, ukuta uliokosa kiongozi shupavu kama Kompany, ilikuwa lazima iende kukutana na wakati mgumu huko Anfield hasa kwa aina ya washambuliaji waliyokwenda kukutana nao.
Kama unaruhusu kufungwa na washambuliaji wa Wolves na Norwich City, usingeweza kuzuia dhidi ya timu yenye watu kama Mohamed Salah na Sadio Mane pamoja na Roberto Firmino waliokuwa kwenye ubora wao.
Ni wazi kabisa, beki ndicho kitu kilichoimliza Guardiola Anfield na si VAR au mwamuzi.
Guardiola atalalamika kuhusu mchezaji wa Liverpool kushika mpira ndani ya boksi, lakini ukweli wa ubora wa kikosi chake kwa sasa anafahamu mwenyewe.
Beki ya Man City kwa sasa si ile ambayo Guardiola ataketi kwenye sofa lake na kutazama timu yake ikicheza. Kyle Walker na John Stones si watu wa kuwaamini kabisa. Hilo hata Guardiola mwenyewe analifahamu ndio maana amekuwa akimtumia mtu kama Fernandinho kwenye eneo la ulinzi.
Huko Anfield, shida nyingine ilikuwa golini. Kumpoteza Ederson lilikuwa pigo kubwa. Claudio Bravo alidhihirisha kwanini anasugua benchi.
Ndio hiyo. Katika mchezo wa Anfield. Kwenda kuikabili Liverpool ambayo bila ya shaka iliingia uwanjani kwa kupania kupata matokeo, Man City ilipaswa kuwa na kikosi chake kamili. Ilimhitaji Fernandinho kwenye kiungo. Ilimhitaji Ederson golini na ilimhitaji David Silva akicheza pamoja na Kevin De Bruyne.
Lakini, kubwa ilimhitaji beki wake bora kabisa, Laporte uwanjani. Anfield si mahali ambako unaweza kwenda kushinda kirahisi hasa ukizingatia kwamba Liverpool yenyewe inahitaji ushindi kwenye mchezo huo. Barcelona wanaweza kuwa mashahidi wazuri kwa kilichowatokea kwenye uwanja huo, wakati Liverpool wanapoingia kutaka jambo lao.
Hicho ndicho kilichowatokea Man City, ilikuwa lazima ipoteze kwa kikosi chake ilichokwenda nacho, beki akicheza Angelino. Wakati wapinzani wako, wameshusha kikosi kizima kilichobeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya miezi michache iliyopita. Sijui ungehitaji nini cha zaidi kwa Man City ile iliyokwenda Anfield. Tazama hata mashambulizi ya Man City yaliyolenga goli. Mara 18 walizofanya jaribio hilo, mara tatu tu ndiyo shambulizi lao lililenga goli. Wenzao Liverpool kwenye mara zao 12, tano zimelenga goli.
Mashuti matatu ya Man City ndio yamelenga goli, Liverpool wao mashuti tano. Hapo unaweza kuona ni watu gani waliokuwa wakihitaji zaidi kushinda kwenye mechi hiyo na waliokuwa na hitihada kubwa ya kupata matokeo chanya. Jambo jingine, Liverpool ilifahamu wazi kwamba wanacheza na timu ambayo ndiyo inayoweza kusimama kwenye njia yao ya kubeba ubingwa kama ilivyotokea msimu uliopita.
Hivyo ilipoikaribisha Anfield na kuona inakuja kupambana na Man City yenye kikosi dhaifu kuliko wakati wowote ule, iliona huo ni wakati mwafaka wa kupata pointi za kukatisha tamaa zaidi. Sasa pengo ni pointi tisa baina yao na mechi 12 zimechezwa.
Safari bado ndefu, lakini ni ndefu zaidi kwa Man City kuweza kusimama kwenye njia ya Liverpool tena kwa msimu huu. Liverpool ilikuwa bora, ilistahi kushinda.